Bandari Dar yawakosha wabunge wa EAC

WABUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wameridhishwa na utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia wateja wake. Kiongozi wa timu hiyo ya Wabunge, Wanjiku Muhia ambaye ni Mbunge kutoka Kenya alisema kwamba, ujumbe wao upo nchini kwa ajili ya kujifunza kwa kutembelea baadhi ya taasisi na miradi kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kuridhishwa kwa wabunge hao, kulitokana na ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam kutokana na taarifa iliyotolewa kwao na Kaimu Meneja wa Bandari hiyo, Freddy Liundi. Liundi aliwaeleza wabunge hao kuwa kiwango cha mizigo inayosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi jirani kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 4.6 kwa mwaka kutoka tani milioni 4.37 mwaka 2013 hadi tani milioni 5.23 mwaka 2017.

Alisema, katika kipindi cha miaka mitano, kiwango hicho cha mizigo inayosafirishwa kwenda nchi jirani kimekuwa kikikua kwa viwango tofauti. Kwa mujibu wa Kaimu Meneja huyo wa Bandari, katika kipindi hicho cha miaka mitano wastani wa ongezeko la mizigo ya Zambia kilikuwa asilimia 2.4, Rwanda asilimia 11.8, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) asilimia 1.3, Burundi asilimia 4.4, Uganda asilimia 2.6 na Malawi asilimia 19.3.

“Bandari ya Dar es Salaam inahudumia nchi nane …. Nchi hizo ni Zambia, Malawi, Msumbiji, DRC, Burundi, Rwanda, Uganda na Zimbabwe, ambazo kwa pamoja zina idadi ya watu zaidi ya milioni 200,”alieleza Liundi mbele ya wabunge hao. Alisema, ufanisi wa Bandari hiyo, unatokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuiboresha kama vile kuongeza ulinzi kwa kutumia kamera (CCTV), uzio wa umeme pamoja na kutumia vyombo vyote vya ulinzi na usalama.

Kuhusu namna mizigo inavyosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, Liundi alisema kuwa, asilimia 99 ya mizigo hiyo husafirishwa kwa barabara na asilimia moja tu husafirishwa kwa njia ya reli.

Kutokana na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na maboresho ya reli iliyopo, mmoja wa wabunge hao alitaka kujua ni kwa namna gani wafanyabiashara ya malori watakavyoathirika mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo.

Akijibu hoja hiyo, Liundi alisema kuwa wafanyabiashara wa malori hawataathirika kwa kuwa hata wao wenyewe huathirika kutokana na malori yao kuharibika kwa kubeba mizigo mizito, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo pia itakuwa nafuu kwao. “Wafanyabiashara wa malori wanajisikia vizuri tu kwa kujengwa kwa reli hiyo. Wanafahamu si mizigo yote husafirishwa kwa barabara kama vile koili, mabati, vyuma na mitambo mikubwa ya miradi kwa kuwa inaua magari yao lakini pia matumizi ya mafuta huwa ni makubwa.

“Kuna mizigo kama vile televisheni, kamera, vitu vya kielektroniki kama vikisafirishwa kwa njia ya reli inakuwa hasara lakini ni faida kama vikisafirishwa kwa barabara,”alisema Liundi. Aidha, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha nchini, Stephen Ngatunga, aliwaomba Wabunge hao kuhakikisha sheria ya Mwaka 2015 inayotaka leseni ya watoa huduma hiyo kuwa ya miaka mitatu badala ya mwaka mmoja, inatekelezwa. Ngatunga aliwaambia wabunge hao kuwa wanapaswa kuzingatia maslahi ya watoa huduma ya forodha wa Afrika Mashariki badala ya kukumbatia wageni.

Alisema kuwa baadhi ya sheria za forodha zinawakandamiza watoa huduma wazawa. Akijibu hoja hiyo, kiongozi wa timu hiyo ya wabunge, Muhia alisema kuwa, jambo hilo litafanyiwa kazi ili kuboresha mazingira ya wafanyabiashara ndani ya EAC. Imeelezwa kuwa, timu hiyo ya wabunge 24 kutoka nchi sita wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianza ziara zake Jumatatu wiki hii katika Ukanda wa Kati na wameshatembelea Zanzibar na Dar es Salaam; baada ya hapo watakwenda Dodoma, Kahama, Ngara, Bujumbura na Kigali.

Muhia alisema kuwa, pia walipata fursa ya kutembelea Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki iliyopo Zanzibar. Alisema, Tume hiyo ni muhimu kwa kuwa Kiswahili kinasaidia katika kurahisisha shughuli za kibiashara katika eneo la mawasiliano. Kwa mujibu wa Muhia, Bunge la Afrika Mashariki liko kwenye mchakato wa kupitisha sera itakayokitambua Kiswahili kama fursa muhimu ya kuziunganisha nchi wanachama wa Jumuiya hiyo katika masuala mbalimbali lakini hasa biashara. Kwa upande wake, Josephine Lemoyan Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania alisema kuwa, Bunge hilo pamoja na mambo mengine lina jukumu la uwakilishi, usimamizi wa rasilimali hasa bajeti na miradi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kufikia malengo ya jumuiya.