Costech yataka matokeo Shirika ya tafiti yasaidie jamii

MKURUGENZI wa Sayansi ya Uhai kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Profesa Mohammed Sheikh, amesema jukumu la wanasayansi ni kuipelekea jamii tafi ti zenye matokeo chanya ili zisaidie katika maendeleo.

Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati watafiti walipokuwa wakitoa matokeo ya tafiti zao na kuangalia jinsi ya kuziboresha ili kuziweka kwenye lugha rahisi itakayoeleweka kwa wanajamii wa ngazi zote. Alisema, kutokana na matokeo hayo chanya yaliyopatikana, serikali inapaswa kuendelea kutoa pesa kwa watafiti hao ili matokeo ya tafiti hizo yalete tija kwa umma.

“Jukumu la watafiti ni kupeleka tafiti kwa jamii, lakini mahali fulani tunajisahau. Kama agenda ya kitaifa ilivyo tunataka kutumia utafiti kuleta maendeleo endelevu kwa Mtanzania hivyo tafiti zetu zisiishie kabatini,” alisema.

Naye Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi za kwenye Maji na Teknolojia za Uvuvi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Samwel Limbu alisema nchi nyingi zimeendelea kutokana na tafiti wanazozifanya na kwamba, hata Tanzania haiwezi kuendelea bila tafiti. Mtafiti Mkuu Kiongozi wa Costech, Dk Khadija Malima, alisema tume haiko tayari kusaidia tafiti ambazo hazitakuwa na matokeo chanya.