Serikali kufunga mageti ya hifadhi kieletroniki

SERIKALI imesema, sasa itafunga mageti ya kielekroniki katika maeneo ya hifadhi ili kuhakikisha inaondoa wababaishaji. Inachukua hatua hiyo baada ya kuanzisha utaratibu mpya wa usajili wa magari yanayofanya biashara ya utalii nchini.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangala amesema, kutakuwa na mageti ya kielekroniki katika maeneo yote ya hifadhi hivyo wale ambao hawatasajiliwa na kupewa namba maalumu, hawataweza kuingiza magari. Dk Kigwangala alisema, magari yote yameanza kusajiliwa kwa utaratibu mpya wa kielekroniki ili yapewe namba maalumu hivyo kama kuna gari halina namba ya utambulisho, halitaingia.

“Gari halitapita kama halina tag maalumu, na mageti haya ya kielekroniki unaweza usiyaone lakini yatakuwepo, kama gari halitasoma hutaweza kuingia katika hifadhi,” alisema. “Watu wanaofanya biashara kinyemela huko tunakokwenda hawataweza kufanya biashara tena, tunafunga kabisa biashara ya kihuni, hivyo atafanya biashara kama amesajiliwa,” alisema.

Alisema, mfumo huo utasaidia kuhakikisha magari yote yatakayofanya biashara ya utalii yanalipa tozo zote za serikali pamoja na kodi. “Tulichofanya ni kufanya mchakato wa mabadiliko ya kanuni ambapo tumeshusha vigezo. Sasa hata mtu mwenye gari moja atasajiliwa na kufanya biashara, na viwango hivi vipya vilianza kutumika mwaka huu,” alisema.

Alisema, katika utaratibu huo mpya ambao leseni mpya zimeanza kutolewa Februari Mosi, mfanyabiashara mdogo atatakiwa kulipa dola za Kimarekani 500 na serikali imefanya hivyo ili nao waweze kufanya biashara hiyo ya utalii.

Alisema kulikuwa na malalamiko ya muda mrefu juu ya kiwango kilichowekwa cha malipo ya dola 2,000 kwa magari yanayofanya biashara ya kubeba watalii kilibagua magari machache. Ilidaiwa kiwango hicho kilikuwa kinawatenga wale wadogo kwani mtu alipaswa kuwa na magari matano kwa mujibu wa sheria ingawa baadaye waliambiwa angalau yawe matatu.