Wasichana 48 waacha masomo, waolewa

WASICHANA 48 waliothirika na mimba za utotoni waliokuwa wakipatiwa mafunzo ya stadi za kazi ili waweze kujitegemea wenyewe, wamekatiza mafunzo yao baada ya wanaume waliowapatia ujauzito kuwalipia mahari na kuwaoa.

Inasemekana ni wivu wa kimapenzi ndio uliosababisha wanaume hao kuharakisha kuwalipia mahari wasichana hao na kuwaoa, wakihofia kuwa wakihitimu mafunzo hayo wanaweza kuolewa na wanaume wengine.

Hayo yalibanishwa na Mratibu wa Mafunzo wa Chuo cha Maendeleo ya wananchi(FDC), Fredrick Mwakikoti kilichopo katika Kata ya Chala wilayani humo, ambacho kwa ufadhili wa Asasi ya Plan International inayotekeleza mradi wa kuzuia ndoa za utotoni, kinatoa mafunzo ya stadi za kazi kwa wasichana walioathirika na mimba za utotoni.

"Mwaka jana chuo chetu cha FDC kilisajili wasichana walioathirika na mimba za utotoni 278, kati yao 120 walitoka kata ya Nkandasi na 158 walitoka kata ya Mtenga.

Wasichana 30 kutoka kata ya Nkandasi na 11 kutoka kata ya Mtenga walikatiza mafunzo yao baada ya wanaume waliowapatia mimba na kuwazalisha watoto kuharakisha kuwalipia mahari na kuwaoa,” alisema.

Alisema wasichana hao wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24, wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya ushonaji , ufundi umeme na mapambo kwa miezi mitatu, ili waweze kujiajiri na kuweza kujitegemea wenyewe na kuwatunza watoto wao.