355,000 kuwahukumu wagombea K’doni, Siha

WAPIGA kura 355,131 waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la wapiga Kura, wanatarajiwa kupiga kura kuwachagua wabunge katika majimbo mawili pamoja na madiwani katika Kata nane Tanzania Bara, katika uchaguzi mdogo unaofanyika leo.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage alisema uchaguzi huo unafanyika baada ya kampeni za uchaguzi huo kukamilika jana. Kutakuwa na vituo vya kupigia kura 867. Alisema uchaguzi huo unafanyika katika majimbo mawili ya Kinondoni katika Jiji la Dar es Salaam na Siha mkoani Kilimanjaro pamoja na uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nane za Isamilo iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Madanga iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.

Alizitaja Kata nyingine kuwa ni Donyomuruak, Gararagua na Kashashi za Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Buhangaza iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Mitunduruni iliyoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida na Kanyelele iliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.

Alisema upigaji kura utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, isipokuwa katika baadhi ya maeneo ambapo vituo hivyo vimesogezwa pembeni kidogo ili kuvipa hadhi ya Vituo vya Kupiga Kura na pia kutokana nasababu nyingine za msingi kulingana na mazingira ya maeneo husika.

Aidha alisema vituo vinafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni na iwapo, wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefi ka kabla ya saa 10 na hawajapiga kura, hao wataruhusiwa kupiga kura.

Hata hivyo alisema, Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 61(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, pamoja na kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao za kupigia kura au zimeharibika au zimechakaa watumie Pasi ya Kusafi ria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Alisema wakati wa upigaji kura na kwa kadri itakavyowezekana kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga na wazee na mpiga kura mwenye ulemavu wa kutoona, ataruhusiwa kufi ka kituoni na mtu atakayemchagua mwenyewe kwa ajili ya kumsaidia kupiga kura yake. Wakizungumzia mwenendo wa kampeni hizo pamoja na uchaguzi baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo pamoja na wagombea walisema kuwa wamejipanga kushinda.

Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema tayari wameshashinda hadi sasa kwa kuwa idadi ya wanachama walio nao ni zaidi ya wapigakura na kusisitiza kwamba wana wagombea makini ambao wanajua serikali ya Awamu ya Tano inataka nini. Kwa upande wake, Mgombea wa Jimbo la Kinondoni kupitia CCM, Maulid Mtulia katika kipindi cha kampeni za chama hicho amekuwa akiahidi kuboresha makazi ya wananchi wa Kinondoni, kusimamia ukarabati wa shule, sambamba na kuahidi kutengeneza fursa za ajira kwa vijana na wanawake kupitia fedha ambazo hutolewa na Halmashauri.

Mgombea Ubunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Salum Mwalimu amekuwa akinadi sera za chama hicho huku akiahidi katika mikutano mbalimbali ya kampeni na kuahidi kuzitetea fedha za wanawake na vijana sambamba na kuboresha Mto Ng’ombe ambao umekuwa ukisababisha mafuriko ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya Kinondoni.

Kwa upande wake, mgombea wa Jimbo la Kinondoni kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Rajabu Juma aliwaomba wananchi wa Kinondoni kura ili kuwaletea maendeleo kwa kuwa waliyemchagua awali alikisaliti chama hicho kwa maslahi yake binafsi. Naye mgombea wa jimbo hilo kupitia TLP, Dk Godfrey Malisa amewataka wananchi kumchagua ili kuwaletea maendeleo ya kweli na kuahidi kwamba atakuwa mbunge asiyeyumba yumba kama wa vyama vingine.

Kufanyika kwa uchaguzi huu kunatokana na wabunge wa majimbo hayo kujiuzulu kutoka vyama vya upinzani kwa kile walichoeleza kumuunga mkono Rais John Magufuli kutokana na utendaji wake. Hata hivyo baadhi ya wananchi wamesema kuwa kwa sasa wanachosubiri ni kupiga kura na kumchagua mtu ambaye wanaamini anaweza kuwaletea mabadiliko, hasa katika masuala ya maendeleo.

Mkazi wa Kinondoni Shamba, Juma Said alisema wanachosubiri wao ni kutumia haki yao ya kikatiba na kuhakikisha kwamba wanahimizana kuwahi ili kuchagua mgombea ambaye wanaamini atawaletea maendeleo “Kura yangu ni siri ila mimi nitamchagua mtu ambaye ninaamini ataleta maendeleo katika maeneo yetu, mfano sisi tunakabiliwa na tatizo la maji, hivyo tunachotaka ni mtu sahihi ambaye ataweza kututatulia kero hii,” alisema. Naye Juliana Joseph, mkazi wa Ndugumbi alisema wanawake hasa wanaofanya biashara ndogo ndogo wamekuwa wakinyanyasika hivyo wanachoangalia ni kumpa kura mtu ambaye wanaamini atawasaidia kuwawekea mazingira mazuri ya biashara.