Majaliwa aamuru Takukuru kumkamata mkandarasi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale kumkamata mkandarasi wa kampuni ya Palimon baada ya kushindwa kukamilisha mradi wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 2.06 wilayani Kwimba.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi na wananchi kwenye kijiji cha Igumangobo wilayani Kwimba. Mkandarasi huyo alianza ujenzi wa mradi huo Oktoba 28, 2013 na alitakiwa kukamilisha Mei 28, 2014.

Waziri Mkuu alisema kitendo cha mkandarasi kutokamilisha mradi huo kwa wakati licha ya kupewa fedha hakivumiliki, hivyo amemtaka Kamanda wa Takukuru kutafuta popote alipo na kumuhoji.

Alitoa agizo hilo baada ya malalamiko ya wananchi wa vijiji vya Mhande, Shirima na Izizimba ‘B’ ambao mradi huo unatekelezwa katika vijiji vyao. Wananchi hao walimuomba Waziri Mkuu awasaidie ili mradi wao ukamilike na wao wapate huduma ya maji.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kwimba kutotumia fedha za miradi ya maendeleo kulipana posho. Waziri Mkuu alisema watumishi wahakikishe wanawahudumia wananchi ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri matumizi ya fedha za maendeleo.

Alisema wilaya hiyo imegeuka kama shimo la kuteketeza fedha za serikali kwa sababu miradi mingi inayotekelezwa haikamiliki, hivyo ameitaka ijipange. Alitolea mfano wa Sh milioni 94 za ujenzi wa mradi wa kliniki ya mifugo ambayo haijakamilika.