NEC yamjibu Mbowe Mawakala Chadema

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezitolea ufafanuzi tuhuma za Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alizotoa kwa NEC zihusuzo uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni unaofanyika leo.

Mbowe akiongozana viongozi wa chama hicho walienda ofi si za NEC wakimlalamikia msimamizi wa uchaguzi huo kukataa kuwaapisha mawakala wa ziada wa upigaji kura wa Chadema ambao ni asilimia 15 ya mawakala wote wanaohitajika kwenye vituo 613 vya uchaguzi.

Akitolea ufafanuzi hoja hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima alisema, kwa mujibu wa kifungu cha 57(1) (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kila Chama cha Siasa kilichopata ridhaa ya kuweka wagombea, kinaweza kuteua wakala mmoja wa upigaji kura kwa kila kituo ndani ya jimbo, hivyo hoja ya kukataliwa kuapishwa kwa wakala wa Chadema siyo kweli.

Aliongeza, Kanuni ya 48(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 inakitaka kila Chama cha Siasa kinachoshiriki katika Uchaguzi siyo zaidi ya siku saba kabla ya siku ya kupiga kura kiwasilishe kwa maandishi kwa Msimamizi wa Uchaguzi majina ya Mawakala, anwani zao na vituo walivyowapangia. Pia akasema kifungu cha 57(3) cha Sheria tajwa, kimeweka utaratibu na mazingira ambayo wa Chama kilichosimamisha Mgombea kuweka wakala mbadala wa upigaji kura.

Akizungumzia kuhusiana na hoja ya pili iliyotolewa na Chadema ya kuwa Msimamizi wa Uchaguzi amekataa kuwaruhusu na Viongozi wa Chadema kuwa Mawakala wa upigaji kura na kwa maana hiyo msimamizi huyo ataichagulia Chadema mawakala wa upigaji kura.

Kailima alisema kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 48(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 vimeweka utaratibu wa muda wa kuwasilisha orodha ya mawakala na muda wa kuwaapisha kuelekea siku ya Uchaguzi. Alisema: “Kwa maana hiyo, siku ya kuwasilisha na kuapishwa mawakala ilikuwa tarehe 10 Februari, 2018.

Hivyo, kupokea na kuwaapisha mawakala wengine itakuwa ni kinyume cha masharti yaliyowekwa chini ya kifungu na kanuni niliyoitaja”. Pia kuhusiana na hoja ya tatu ya kuwa Mawakala wa upigaji kura wa Chadema hawajapewa nakala za hati zao za kiapo cha kutunza siri, Kailima aliweka wazi kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 48(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 kila Wakala wa Upigaji kura anapaswa kuapa kiapo cha kutunza siri katika Fomu Na. 6 kabla ya kutekeleza wajibu wake katika kituo cha kupigia kura.

“Kwa takwimu zilizopo jumla ya vituo vya kupigia kura ni 613 na jumla ya Vyama vya Siasa 12 vinashiriki katika uchaguzi huo. Kwa kuwa kila Wakala mmoja alijaza nakala mbili za Kiapo cha kutunza siri, hapo unazungumzia uwepo na viapo 14,712,” alisema. Kanuni ya 48(3) ya Kanuni tajwa, Wakala wa Upigaji Kura atapaswa kupewa barua na Msimamizi wa Uchaguzi ya kumtambulisha kwa Msimamizi wa Kituo cha kupigia kura.

Hapa unazungumzia nakala 22,068 kwa sababu, nakala moja atapewa wakala, nakala itabaki kwenye jalada kwa kumbukumbu na nakala itapelekwa kwa Msimamizi wa Kituo kwa urahisi wa rejea. Aliongeza Msimamizi wa Uchaguzi ameanza kutoa nakala hizo za Viapo kwa Wawakilishi wa Vyama vyote vinavyoshiriki Uchaguzi mdogo ili wawapatie Mawakala wa Vyama husika.

Chadema pia ililalamika kuwa, Msimamzi wa Uchaguzi amewaelekeza Mawakala kuwa na vitambulisho vya Mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Hati ya Kusafi ria na Kitambulisho cha Kitaifa ili kuwatambulisha, hoja ambayo Kailima alifafanua kwa kusema wanaweza kitumia vitambulisho vya Taifa, Hati ya Kusafi ri na Leseni ya Udereva kupiga kura.

Kailima aliikataa hoja ya tano ya Chadema ya kuwa msimamizi wa Uchaguzi hajatoa na kuweka wazi kuhusu kituo kikuu cha majumuisho ambapo alisema NEC iliandika barua yenye kumbukumbu Na KMC/ U.21/06/119, Februari 14 mwaka huu kuvijulisha kuwa kituo cha majumuisho ya hesabu za kura ni Biafra ambapo yataanza sa 12:00 jioni siku ya uchaguzi.