Mji wa Serikali kutumia maji lita mil.3 kwa siku

 MJI wa Serikali utakaojengwa Chamwino mkoani Dodoma, utahitaji maji lita za ujazo milioni tatu kwa siku kwa ajili ya matumizi ya ofisi za serikali, mabalozi na makazi ya viongozi.

Takwimu hizo zilitolewa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isaac Kamwelwe baada ya kutembelea visima vya maji viwili vilivyochimbwa kwa ajili ya kupeleka maji kujenga ofisi na makazi hayo.

Katika ziara hiyo, Waziri Kamwelwe alifika mahali utakapojengwa mji huo na ambako tangi kubwa la kupokea maji kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vikiwemo visima na mabomba litajengwa.

Alisema ofisi za Ikulu, mabalozi, wizara na taasisi nyingine za serikali zitakazojengwa hapo zitahitaji maji takribani mita za ujazo milioni tatu kila siku na wizara yake imejipanga kuhakikisha zinapatikana.

Wizara yake kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa), ilijiandaa mapema kwa kuweka akiba ya mabomba na kuchimba visima kupitia Mamlaka ya Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA) ili kupata maji ya kusambaza kwa ofisi na makazi ya watumishi wa Ikulu.

Katika kuhakikisha Ikulu inakuwa na maji ya kutosha, Kamwelwe alisema Duwasa ilikuwa imejiandaa kwanza kwa kuweka bomba la akiba katika eneo la Mailimbili ambalo linapokea maji kutoka kwenye chanzo cha Nzakwe na hilo litapeleka maji moja kwa moja Makao Makuu ya Serikali, Chamwino, Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, David Pallangyo alisema mamlaka yake ipo tayari katika kuhakikisha maji yanapatikana kwani kwa sasa inazalisha mita za ujazo za kutosha hadi kusambaza katika eneo la Ikulu.