Uchaguzi wa wabunge Septemba

RAIA wa Rwanda watapiga kura Septemba mwaka huu kuwachagua wabunge.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Charles Munyaneza, amesema uchaguzi huo utafanyika Septemba 2 na 3 mwaka huu.

Alisema wawakilishi wa viti maalumu kama vijana, wanawake na watu wenye ulemavu watachaguliwa Septemba 4.

Alieleza kuwa bunge linakuwa na wawakilishi 80 kati yao 53 wanapatikana kutoka vyama vya siasa, 24 wawakilishi wa wanawake (wakichaguliwa kupitia baraza la wanawake, wawili wakiwalisha vijana na mmoja watu wenye ulemavu.

Alisema wagombea binafsi wanaruhusiwa kugombea nafasi hizo. Munyaneza alisema raia wa Rwanda wanaokaa nje ya nchi watachagua wawakilishi wao Septemba 2 wakati wananchi wa nchi hiyo watafanya uchaguzi Septemba 3.

Alisema watapokea majina ya wagombea Julai 12 mpaka 25 na watakaoidhinishwa watatangazwa Agosti 6 huku kampeni za wagombea zitaanza Agosti 13 na kumalizika septemba 1 na matokeo kutangazwa Septemba 16.

Alisema maandalizi ya uchaguzi huo tayari yameanza ikiwemo kuhakiki daftari la wapigakura kwa kuwaondoa waliofariki na waliohama makazi yao ili waweze kupiga kura. Inatarajiwa watu milioni 7.1 watapiga kura mwaka huu baada ya kuandikishwa wapigakura wapya 200,000.

Munyaneza alisema wanatarajia kuanza kutoa elimu ya wapigakura kwa kuandaa timu maalumu kwa kuanza katika ngazi ya taifa mpaka vijijini huku uchaguzi huo unatarajia kutumia kwa wastani wa fedha za Rwanda Rfw bilioni 5 na Rfw bilioni 6.