Tanzania yapania kuendelea kuongoza utalii EAC

SIKU chache baada ya Kenya kukiri Tanzania imewapiku kwa ufanisi katika sekta ya utalii, Serikali imesema imeweka mikakati zaidi ya nchi kuendelea kuongoza kwa idadi kubwa ya watalii katika nchi za Afrika Mashariki.

Hadi mwaka jana, sekta ya utalii ilikuwa inachangia asilimia 17 ya pato la taifa, huku sekta hiyo ikichangia kwa asilimia 12 katika soko la ajira Tanzania.

Kwa sasa, Mbali na mikakati ya kupanua wigo wa vivutio vya utalii imejipanga kuhakikisha waongoza watalii wanapatiwa mafunzo na kusajiliwa kwa lengo la kuhakikisha wanawaongoza watalii kwa ukarimu.

Aidha,nchi imekuwa na mikakati ya kuongeza watalii kufikia milioni mbili mwaka 2020 kwa kuangalia masoko mapya ya watalii kutoka nchi za China, Israel, Urusi ,Australia na nchi za Scandinavia.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Hamza Temba anasema katika kuongeza ukarimu kwa watalii serikali imeanza kusajili waongoza watalii kwa lengo la kuwajengea uwezo na hatimaye kuboresha huduma wanazotoa.

Alisema baada ya kupata taarifa kutoka Kenya kukiri Tanzania kuwazidi kwa utalii wamepokea kama changamoto kuendelea kujiimarisha kwa kuboresha huduma mbalimbali za utalii ikiwemo kuongeza vivutio vya utalii hususan katika Kanda ya Kusini.

Temba alisema katika kufungua utalii wa Kanda ya Kusini ili kuongeza idadi ya watalii na mapato,wamepokea mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia wa Dola za Marekani milioni 150, sawa na takriban shilingi bilioni 340 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Kusimamia Maliasili na Kuendeleza Utalii wa Ukanda wa Kusini.

Alisema tayari wamezindua mradi huo ujulikanao kama REGROW na utaanza katika maeneo ya kipaumbele ambayo ni hifadhi ya taifa ya Ruaha,Mikumi,Udzungwa na pori la akiba la Selous.

Alisema Katika kuongeza idadi ya watalii nchini, Wizara imeendelea kutekeleza shughuli mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya hifadhi, kuboresha miundo mbinu kwenye maeneo ya vivutio, kuanzisha huduma mpya za utalii pamoja na utangazaji.

Alisema juhudi mbalimbali za serikali zimewezesha ongezeko la watalii kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi kufikia 1,284,279 mwaka 2016 sawa naongezeko la asilimia 12.9. Ongezeko hilo limetokana na ongezeko la watalii wa nje kutoka 1,137,182 mwaka 2015 na kufikia 1,284,279 mwaka 2016.

Aidha, mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani bilioni 2 (Sh trilioni 4.4) mwaka 2016.

Akizungumzia ukusanyaji wa maduhuli yanayotokana na ada za leseni ya biashara ya utalii umeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.1 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani bilioni 5.6. mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 36. Sekta ya utalii imeingizia Tanzania dola za Marekani bilioni 2.3 (Sh trilioni 5) mwaka uliopita ikiwa ni zaidi ya mwaka 2016 iliingiza dola za Marekani bilioni 2 (sawa na Sh Trilioni 4.4) huku mwaka 2015 iliingizwa dola bilioni 1.9 (Sawa na sh trilioni 4.18).

Alisema sekta ya Utalii ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi hasa katika sekta za kilimo, mawasiliano, miundombinu, usafirishaji, burudani na uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa watalii. Katika mwaka 2016/2017 sekta ya utalii imetoa ajira takribani 500,000 za moja kwa moja.

Alisema pia kuna mikakati mipya ya kuboresha sekta ya utalii ni pamoja na kuanzisha kwa Tamasha la Mwezi Maalumu la Urithi wa Mtanzania (Urithi Festival) ambao utaadhimishwa Septemba ya kila mwaka. Kuboresha na kuendeleza utalii wa fukwe kwa kuanzisha Mamlaka ya Fukwe.