CAG: Matibabu nje ya nchi kaa la moto

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad amesema ongezeko la deni la matibabu ya nje limepanda kutoka Sh bilioni 28.60 kiasi kilichoripotiwa Juni 30, 2017 hadi Sh bilioni 45.73 kufi kia Desemba 31, 2017.

CAG alisema ongezeko hilo ni asilimia 60.71 na akaishauri serikali kulifuatilia kwa makini ili kupunguza mzigo wa madeni na kuzilipa hospitali kwa wakati. CAG aliyasema hayo alipokuwa akiwasilisha bungeni jana ripoti za ukaguzi zilizofanywa na ofisi yake kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mwaka jana. Akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, CAG alisema ripoti za ukaguzi zinahusu ripoti ya Serikali Kuu (CG), Mamlaka ya Serikali ya Mitaa (LGA), mashirika ya umma, miradi ya maendeleo na ukaguzi wa ufanisi na ripoti 10 zainazohusu ukaguzi wa ufanisi katika sekta mbalimbali.

Akizungumzia deni la Taifa, CAG alisema deni hilo linahimilika hadi sasa, lakini akaomba serikali kuongeza umakini katika ukopaji wake kwani linazidi kuongezeka. “Hadi Juni 30, mwaka jana, deni la Taifa lilikuwa Sh trilioni 46.08 ambapo mwaka uliotanguliwa lilikuwa trilioni 41.03, ikiwa ni ongezeko la Sh trilioni 5.04 sawa na asilimia 12. Aidha, deni la ndani lilikuwa Sh trilioni 13.33 na deni la nje trilioni 32.75,” alisema. Kuhusu hati mbalimbali zilizotolewa kwenye taasisi hizo, CAG alipongeza kwa kuongeza idadi ya hati zinazoridhisha kufikia 471 kati ya 527 sawa na asilimia 90.

Ofisi yake pia imebaini kwamba mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yamechangiwa kushuka kutokana na kuwepo kwa kesi za muda mrefu katika Mamlaka za Rufaa za Kodi zinazofikia Sh trilioni 4.44. Profesa Assad alisema Sh milioni 732.63 zilizotakiwa kutolewa na kampuni za madini ili kuchangia mfuko wa maendeleo wa madini, na hazijatolewa na migodi ya Buzwagi kinyume cha makubaliano. Alisema katika ukaguzi wao kwa Shirika la Uzalishaji Maji la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA- JKT) walibaini kwamba kuna madeni ya muda mrefu ya Sh bilioni 40.04 ambayo hayajakusanywa kutoka kwa wakulima waliokopeshwa matrekta na vifaa vya kilimo.

CAG alisema ukaguzi wao pia ulibani kwamba Sh bilioni 219.47 zilitolewa na serikali kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni, wakandarasi na watoa huduma mbalimbali waliotoa miaka ya nyuma, ofisi yake inashauri, madeni ya miaka ya nyuma yaingizwe kwenye bajeti ya mwaka inayotarajiwa kulipwa ili kuepuka kuathiri utekelezaji wa bajeti. Kuhusu ukaguzi kwenye LGA, Profesa Assad alisema fedha ambazo zilitakiwa kutolewa na serikali kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo katika serikali za mitaa nyingi hazijakwenda.

Alitoa mfano wa fedha za maendeleo ambazo zilitakiwa kutolewa katika halmashauri 167, ambazo zaidi ya Sh bilioni 532.21 sawa na asilimia 51 hazikutolewa, jambo ambalo linasababisha miradi mingi ya maendeleo kutokamilika na kuongezeka kwa madeni katika mamkala hizo. Lakini pia Mamlaka za Serikali za mitaa 20 hazikupokea Sh bilioni 3.53 ambazo zilitakiwa kupokea kutoka kwa wakala ambayo ni sehemu ya mapato ya ndani yaliyokusanywa na wakala hao hivyo kuathiri utekelezaji wa shughuli za mamlaka za mitaa.

Sambamba na hilo, pia vitabu 379 vya kukusanyia mapato kutoka katika mamlaka 21 havikuwasilishwa, licha ya kuombwa kufanya hivyo, kitendo ambacho hakiwezi kuthibitisha ni kiasi gani cha mapato kilichokusanywa kupitia vitabu hivyo. Ofisi yake pia ilibaini kwamba Mamlaka za serikali za mitaa 116 zina kesi mahakamani zaidi ya 1,111 zenye madai ya Sh bilioni 186.44 za wadai mbalimbali, na hivyo zikishindwa zitalazimika kulipa fedha hizo na hivyo kuathiri utoaji endelevu wa huduma kwa jamii. Pamoja na CAG kuwasilisha ripoti hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe wakati akiahirisha mkutano na waandishi wa habari uliopangwa kufanyika baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa, alisema mawaziri mbalimbali walioguswa na ripoti hizo watatoa majibu ya hoja zote zilizoibuliwa kwenye ripoti hiyo leo.