Tutaendelea kumuenzi Sokoine - Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kusimamia maadili ya utumishi wa umma ili kuenzi fikra za Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Moringe Sokoine.

“Tutaendelea kusimamia maadili ya utumishi wa umma kwa kuzingatia yale yote ambayo Mheshimiwa Sokoine aliyaanzisha,” amesema. Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi waliohudhuria ibada ya Kumbukumbu ya miaka 34 ya kifo cha Sokoine, iliyofanyika kijijini kwake Engwiki, kata ya Monduli Juu, wilayani Monduli, mkoani Arusha.

Ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Josephat Lebulu, ilihudhuriwa na viongozi wa dini wa wilaya, viongozi wa Serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha na baadhi ya wabunge. Majaliwa alisema Sokoine alikuwa adui wa wahujumu uchumi na alihakikisha uchumi wa nchi unakua kwa maslahi ya Watanzania wote. “Mungu alitupa hazina iliyong’ara na kuangaza.

Sote tuendelee kuangaza kwa kutenda mema na kuendeleza yale yote aliyoyaanzisha mpendwa wetu. “Katika maisha yake, hakuwa na ubinafsi, uroho, wala tamaa ya kujilimbikizia mali. Hili ni jambo la kuigwa na sisi viongozi wa umma. Nasi tulioko kwenye nafasi hizi za uongozi, tumuombe Mungu atuwezeshe tutende yale aliyoyaanzisha,” alisisitiza.

Alitumia fursa hiyo kuwafikishia wanafamilia na wananchi waliohudhuria ibada hiyo salamu kutoka Rais John Magufuli na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Mapema, akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria ibada hiyo, Askofu Lebulu alimuelezea Sokoine kuwa ni kiongozi aliyechapa kazi kwa bidii, mwenye uzalendo, aliyeongozwa na upendo na uwajibikaji kwa wananchi anaowaongoza. Akitoa shukrani kwa niaba ya familia, msemaji wa familia ya Sokoine, Lembris Kivuyo alisema wanaishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo imekuwa karibu sana na familia hiyo tangu Sokoine alipofariki dunia.