Mwakyembe atoa maagizo mazito TBC

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imesema, Startimes Group wameikubali taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mapendekezo yake yote ikiwa ni pamoja na kuipa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) madaraka inayostahili hivyo kuruhusu uwazi katika uendeshaji wa kampuni hiyo ya ubia.

Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema mjini Dodoma kuwa, Startimes Group pia imeruhusu TBC na wataalamu wake kuingia kwenye mifumo ya TEHAMA ya uendeshaji kampuni hiyo ya ubia ili kuwe na uwiano upande wa wafanyakazi na viongozi wa kampuni hiyo ya pamoja.

Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, pia imeamuliwa kwamba, bodi ya StarMedia ambayo Mwenyekiti wake ni Mkurugenzi Mkuu wa TBC ianze kazi mara moja ya kupitia utekelezaji wa bajeti mpya ya mwaka 2018 na kuchukua hatua stahili kwenye maeneo yote yaliyoanishwa na CAG.

Waziri Mwakyembe amesema, wakati hoja nyingine zikifanyiwa kazi kampuni ya StarMedia itatoa shilingi bilioni 3 kwa TBC kama ruzuku mwaka huu 2018.

"Tumeanza vizuri na tunaamini changamoto zote zilizoainishwa na CAG zitarekebishwa haraka na umma utakuwa ukiarifiwa" amesema.

Amesema, Wizara na taasisi zake inamshukuru na kumpongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Profesa Mussa Assad na wataalamu wake kwa kazi nzuri waliyofanya ya ukaguzi maalum kuhusu uendeshaji wa kampuni ya ubia kati ya TBC na kampuni ya Star Communication Network Technology Ltd ya China iitwayo StarMedia.

Kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe Septemba mwaka 2016 Serikali kupitia Bodi ya Wakurugenzi TBC ilimuomba CAG afanye ukaguzi maalum StarMedia kwa kuwa haikutoa gawio kwa wabia kwa miaka saba mfululizo.

Amesema, wiki iliyopita TBC na Startimes Group walisaini mkataba kuashiria mwafaka mpya katika uendeshaji StarMedia.

“Natumia fursa hii kutoa maagizo mahsusi kwa bodi ya TBC na Mwenyekiti wa Bodi ya StarMedia Tanzania kusimamia kwa karibu na kikamilifu utekelezaji wa hoja zote zilizopo kwenye mkataba huo” amesema Waziri Mwakyembe.

Amesema, Wizara inatarajia kuona uongozi wa TBC ambao umekalia kiti cha StarMedia unasimamia uamuzi huo kwa karibu na kuiongoza kampuni kwa kuzingatia maslahi ya pande zote badala ya kukaa pembeni.

Waziri Mwakyembe amesema, Wizara itafuatilia kwa karibu utekelezaji na haitasita kuchukua hatua kali za kisheria na kinidhamu kwa mtendaji wa upande wowote atakayekuwa kikwazo katika uendeshaji wa kampuni.