Gesi asilia kusambazwa Dar kwa 1,000/- kwa siku

KATIKA kuimarisha usambazaji na matumizi ya gesi asilia majumbani na kwenye magari, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuanzia mwaka huu litaanza kushirikiana na kampuni binafsi ili kusambaza nishati hiyo majumbani, ambapo familia ya watu watano watalipia Sh 1,000 kwa siku.

Mpango huo ambao katika awamu ya kwanza, utaanza katika Jiji la Dar es Salaam utagawanywa katika kanda tatu za Ilala, Kinondoni itakayounganishwa na Ubungo na pia Temeke itakayounganishwa na Kigamboni. Aidha imeelezwa kuwa kampuni itakayoshinda zabuni hiyo, itawekeza, kujenga, kuendesha na kuuza kwa wateja gesi hiyo ya asilia chini ya makubaliano yatakayowekwa katika mkataba na baada ya kampuni hiyo kurudisha fedha yake na faida, miundombinu hiyo itarejeshwa serikalini katika Shirika la TPDC.

Mtafiti wa Mkondo wa Chini wa TPDC, Arstides Kato alisema Dar es Salaam kuwa kampuni mshindani, inatakiwa kuwa na uwezo wa kifedha na teknolojia katika kuwezesha kusambaza kwa wananchi gesi hiyo nafuu, ambayo inaelezwa kuwa familia ya watu watano, itakuwa inalipa gharama ya Sh 1,000 tu kwa siku sawa na Sh 30,000 kwa mwezi. Kato alisema mpaka sasa utaratibu wa maandalizi hayo, unaendelea vizuri na sasa upo katika hatua za juu serikalini, kabla ya kuanza utekelezaji baadaye mwaka huu.

Kato alisema baada ya Dar es Salaam, mikoa itakayofuata katika kuunganishiwa gesi ya matumizi ya majumbani, itakuwa ni Lindi na Mtwara kutokana na mikoa hiyo kuwa tayari ina miundombinu ya bomba na hivyo kuwa rahisi kwa wananchi kuunganishiwa. Alisema baada ya kumaliza maeneo hayo, lengo la TPDC ni kuhakikisha gesi asili kwa matumizi ya nyumba inasambazwa nchi nzima, ambapo utafanyika upembuzi yakinifu wa namna wa kupeleka gesi hilo nchi nzima. Alisema licha ya gesi hiyo kuwa nafuu kwa matumizi, pia haiharibu mazingira, kwani inatoa kiwango kidogo cha gesi ukaa na si rahisi kulipuka, kama ilivyo gesi inatotumika kwa sasa majumbani.

Alisema tayari wapo wakazi wa maeneo ya Mikocheni, wanatumia gesi hiyo ya asili baada ya kuunganishiwa kutoka katika bomba dogo la kutoka Ubungo kwenda Mikocheni, lenye ukubwa wa nchi 12 na urefu wa kilometa 6.2. Alisema katika bomba hilo, nyumba 70 zimeunganishiwa gesi asilia kwa ajili ya kupikia. Alisema pia vipo viwanda vitano na kituo kimoja cha kujaza gesi katika magari 60, ambayo tayari yamefanyiwa matengenezo ya kutumia gesi asilia. Wakati huo huo, alisema hadi sasa zipo taasisi mbili za kubadilisha magari na kuyafungia mfumo wa gesi asili, ambazo ni Taasisi ya Bicco iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT).