Waziri amsimamisha meneja, avunja bodi

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amemsimamisha kazi Meneja wa Kitengo cha Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU), Dr Milali Machumu kwa tuhuma za kushindwa kusimamia ipasavyo kitengo chake.

Maamuzi hayo yamekwenda sambamba na kuivunja Bodi ya Wadhamini baada ya Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuainisha mapungufiu 24 ambayo yanahusu kitengo hicho. “Taarifa ya Ukaguzi wa Ufanisi katika Usimamizi wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu umebainisha udhaifu katika usimamizi wa hifadhi za bahari na maeneo tengefu,” Waziri Mpina amewaeleza wanahabari mjini Dodoma leo.

Amemwagiza Katibu Mkuu wa Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuunda kamati ya uchunguzi juu ya utendaji wa meneja aliyesimamishwa. Ameendelea kueleza kuwa udhibiti duni wa matumizi ya rasilimali za bahari katika maeneo tengefu ya bahari na kuongeza, “hifadhi za bahari za Tanga na Mtwara hazikuzingatia kanuni za utoaji wa vibali vya matumizi ya serikali. Waziri Mpina amesema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kulinda rasilimali za nchi na kusisitiza idara chini ya wizara yake kuhakikisha kuwa weledi unakuwepo.