‘Sikuhudhuria sherehe yoyote isipokuwa msiba’

ALIISHI nyumba mbovu. Mtu yeyote aliyepita nje aliweza kumuona.

Mavazi yake yalikuwa duni sana. Hakuweza kwenda kwenye sherehe yoyote iliyofanyika kijijini kwake. Shughuli pekee aliyoweza kuhudhuria, ilikuwa ni msiba tu. Haya ndiyo yalikuwa maisha ya Hidaya Mjaka; mkazi wa Shehia ya Donge Mnyimbi Unguja.

Mama huyu mwenye mtoto mmoja anayesoma darasa la tano, anapoanza kusimulia alikotoka kimaisha na alipo sasa, anakufanya uvutiwe kumsikiliza hadi mwisho. Kaya yake ni miongoni mwa kaya 104 ambazo zinapokea fedha za awamu ya tatu ya mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf III) chini ya mpango wa uhaulishaji wa fedha za kunusuru kaya masikini.

Mama huyu hupokea Sh 32,000 kila baada ya miezi miwili ikiwa ni ruzuku ya msingi Sh 10,000, ruzuku ya kuwa na mtoto Sh 4,000 na ruzuku ya mwanawe anayesoma shule ya msingi Sh 2,000. Kipindi anatambuliwa kuwa katika kaya maskini alikidhi vigezo vyote vya kaya maskini.

Anajieleza kuwa, aliishi kwenye nyumba mbovu ya tembe iliyoezekwa kwa makuti, mlo wake kwa kutwa ulikuwa mmoja tu. Mtoto wake alikosa mahitaji muhimu ya shule.

“Nyumba niliyoishi wakati huo ilikuwa si nyumba, ilikuwa mbovu matundu kila pahali. Hata aliyepita nje aliweza kuniona. “Mavazi yangu pia yalikuwa makuu kuu kiasi kwamba sikuweza kwenda kwenye sherehe zilizokuwa zikifanyika hapa kijijini. Shughuli niliyoweza kuhudhuria ilikuwa ni msiba tu,” anasimulia mama huyu.

Nilipomtembelea hivi karibuni nje ya nyumba yake nilikuta kifusi cha nyumba yake ya zamani ambayo ameibomoa kupisha ujenzi wa nyumba mpya ambao unaendelea. Anajenga nyumba ya tofali ya vyumba vitatu vya kulala, sebule na choo. Kutokana na kutokuwa na kipato kikubwa nyumba hii inajengwa kwa awamu. Tayari ameshajenga vyumba viwili.

Kimoja cha kulala na kingine ni sebule. Nyumba hii maridadi imeezekwa kwa bati jeupe ambalo linaonesha kuwa vyumba hivyo vimepauliwa siku za hivi karibuni. Anatabasamu kila akizungumza kuhusu jengo hili. Ana furaha moyoni. Ni ndoto ambayo imetimia.

Mama huyu alikuwa na mipango thabiti ya kujikomboa kutokana na ruzuku hiyo aliyopokea na haoni tabu kusema yaliyo moyoni mwake. Anasema kwa maisha aliyoishi hapo awali mambo yalikuwa hayaendi, ilifika wakati alikata tamaa na kujiona kuwa ataishi maisha duni siku zote.

“Mungu si Athumani, Mpango wa TASAF ulifika katika Shehia ya Mnyimbi nami nikatambuliwa kama kaya inayostahili kuwemo kwenye mpango na kupokea ruzuku,” anasema. Je, Sh 32,000 anazopokea kila baada ya miezi miwili, zimewezaje kubadilisha maisha ya mama huyu, ikiwamo kujenga nyumba imara?

Hidaya anasema, “Kila ninapopewa ruzuku yangu shilingi elfu kumi naitumia kwa mahitaji ya mtoto ya skuli (shule). Nanunua vitabu, sare za skuli, viatu na kutoa michango inayotakiwa na mara moja moja nampa pesa kidogo kwa ajili ya kutumia anapokwenda skuli.

Inayobaki ni kwa ajili ya chakula na kiasi kidogo nilikuwa naweka akiba kwa kuwa nilipanga tangu awali kuboresha makazi yangu.” Kutokana na kudunduliza fedha, zilipofika Sh 100,000 alinunua mifuko ya saruji na mchanga. Alianza kufyatua matofali na kuanza ujenzi hatua kwa hatua. Na sasa amekamilisha hatua ya kwanza ya ujenzi wake wa vyumba viwili.

Kisha akanunua bati na kupaua. Anaeleza kwamba anaendelea kwa mtindo huo huo wa kudunduliza na hatua ya pili ataianza karibuni kwani tayari ameshafyatua matofali ya kutosha. Fedha alizojengea hazikutoka kwenye ruzuku pekee, bali kwenye vyanzo vingine viwili. Hidaya ni mwanachama wa vikundi viwili vinavyojulikana kama vikundi vya hisa vilivyopo kijijini hapo.

Akiba yake aliyoweka kwenye vikundi viwili ambavyo ni mwanachama vimemuwezesha kupata fedha za ziada ambazo zimemrahisishia kazi yake ya ujenzi. Pamoja na kuwa ni mwanachama wa vikundi vya hisa, Hidaya pia ni mkulima na mjasiriamali. Anafanya biashara ya kupika na kuuza vitafunwa vikiwemo visheti, keki, biskuti na maandazi.

“Hapa ninapokaa ni njiani, watoto wanapita hapa wanapokwenda na kurudi kutoka skuli. Naweka vitu hivi barazani kwangu na kuviuza na watoto wananunua. Faida ninayopata kwenye mauzo naiongezea katika akiba yangu ya kununua mifuko ya saruji na kupiga matofali,” anasema.

Mama huyu analo shamba la karibu ekari mbili ambalo amepanda mahindi. Kipindi kilichopita hakuweza kulima katika shamba lake kutokana na changamoto za kipato. Alishughulikia zaidi kutafuta fedha kwa ajili ya kununua chakula kuliko kujihusisha na kilimo.

Kutokana na ruzuku aliyopokea ameweza kumlipa mtu ambaye amemlimia shamba hilo na baadaye ameendelea mwenyewe kulishughulikia shamba hili. Pamoja na ukame uliotawala kwa kipindi kirefu, shamba lake limestawi vizuri sana na mahindi aliyopanda yanaelekea kukomaa. Shamba hili liko katika hali hii kutokana na matunzo.

Mahindi katika shamba hili yamepandwa kitaalamu kabisa na shamba ni safi, limepaliliwa na mazao yamestawi vizuri. Katikati ya shamba hili, Hidaya amechimba kisima cha mkono ambacho anapata maji ya kutosha kumwagilia. Kila asubuhi na jioni mama huyu anachota maji kwa ndoo na kumwagilia shamba lake.

Ana uhakika wa kuvuna mahindi ya kutosha kwa ajili ya chakula na bila shaka atapata ziada ambayo atauza ili kujiongezea kipato. Hidaya amekuwa ni mtu mwenye furaha. Ana mipango ya kujiendeleza na familia yake ya mtoto mmoja. Ruzuku anayopata anasema imemsaidia vya kutosha.

Anashukuru siyo tu Tasaf bali pia, wakazi wenzake wa Shehia ya Donge Mnyimbi waliomuona kwamba anastahili kuwemo kwenye mpango huo. Anaona fahari kwa kutowaangusha kwani ametumia fursa aliyoipata kujikwamua kutoka kwenye hali mbaya ya maisha.

“Namshukuru Mungu, Alhamdulilah (Mungu mkubwa).Nilipofika si haba naweza kusimama kwa miguu yangu mwenyewe. Najua iko siku ruzuku hii itafikia ukomo hivyo nitaendelea kujituma hata wakati huo utakapofika niwe nimeshamaliza ujenzi wa nyumba yangu na kujiendeleza kibiashara,” anasema.

Hidaya anashauri wenzake ambao wanaendelea kupata ruzuku kupitia mpango huo wa kunusuru kaya masikini. “Natoa mwito kwa wenzangu nao watumie vizuri fursa tuliyopewa na watie bidii katika shughuli zao na wawe na kitu cha kujivunia kwamba walipowezeshwa walijiongeza na kujitoa kwenye umaskini.”

Anaendelea kushauri, “Wafuate ushauri tunaopewa na wanakamati kuhusu matumizi mazuri ya fedha na wasisahau kuweka akiba na kuanzisha miradi ya ujasiriamali kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kujikwamua.”

Simulizi ya Hidaya inadhihirisha ukweli kwamba, penye nia pana njia. Nidhamu katika matumizi ya fedha huwewezesha aliye na kipato cha chini kufanya mambo makubwa ya kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba, kuanzisha miradi ya ujasiriamali na ufugaji wa kuku, bata, mbuzi, sungura.

Hidaya anadhihirisha, si lazima kuwa na mamilioni ya fedha kuwa na hali bora, bali yote yamewezekana kwa kuwa na malengo na nidhamu katika matumizi ya fedha. Funzo linaloendelea kupatikana ni pamoja na jamii kuondokana na dhana kwamba fedha zinazotolewa na TASAF hazisaidii chochote.

Wanaodai kwamba fedha hizo tegemezi, wanapaswa warejee kwa mama huyu wapate majibu sahihi. Watakubaliana kuwa ruzuku kwa kaya maskini ni kichocheo na si mshahara. Inalenga kuwezesha kaya maskini zilizo katika mazingira magumu, zimudu mahitaji ya msingi hususani chakula, malazi na huduma za afya.

Hidaya ni sehemu ya walengwa wengi wa mpango huu wa kunusuru kaya masikini ambao kabla ya kupokea ruzuku ya Tasaf, waliishi kwa kutegemea misaada na huruma ya majirani na wasamaria wema. Wazee na watoto ndio walioathirika zaidi kwani hawakuwa na uwezo wa kufanya kazi kuweza kupata mahitaji muhimu.

Walengwa wengi wana simulizi tofauti za kusisimia, kushangaza na nyingine za kuhuzunisha zinazoweza kumfanya msikilizaji atoe machozi. Mathalani, kitendo cha Hidaya kukosa hata fursa ya kushiriki kwenye sherehe mbalimbali isipokuwa misiba, ni simulizi za zinazosababisha kutoa machozi.

Lakini furaha inakuja pale walengwa hawa wanaposimulia mafanikio huku wakishangilia kuwa Tasaf amekuwa mkombozi kwa maisha yao. Wametoka kwenye maisha duni na kujikwamua kimaisha. Taabu na shida zimebaki kuwa historia. Hata hivyo, siri ya mafanikio yote haya ni nidhamu katika matumizi ya fedha na kufuatilia ushauri unaotolewa mara kwa mara na wataalamu kila siku ya kupokea malipo.

Mipango ya uhawilishaji fedha sio kitu kigeni duniani. Utekelezaji wa mipango hii ulianza zaidi ya miaka 10 iliyopita na ilianza taratibu na sasa ni mipango mikubwa ambayo inafahamika kote duniani. Ikiachwa Tanzania, nchi nyingine katika Afrika zinazoendesha mpango huu ni pamoja na Nigeria, Afrika Kusini, Lesotho, Zambia, Ethiopia na Malawi.

Vile vile nchi za Amerika ya Kusini kama Mexico na Brazil zinaendesha mpango wa uhawilishaji fedha kama njia mojawapo ya kunusuru kaya maskini. Mipango hii hutoa ruzuku au chakula kwa kaya maskini kwa masharti ya kupeleka watoto shuleni au kliniki kwa ajili ya chanjo.

Mpango ulipoanzishwa nchini, ulichukuliwa kuwa utajenga utegemezi kwa kaya maskini. Lakini kumbe, kaya husika zimekuwa zikipewa stadi za ujasiriamali, zikihamasishwa kuweka akiba na hatimaye kuanza kutekeleza miradi ya kuongeza kipato.

Walengwa wa mpango huu, wanafahamu kwamba ruzuku wanayopokea itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mitano kabla ya kuondolewa na kupisha