Hatua ya kuzawadia askari weledi ni ya kupongezwa

MIONGONI mwa watumishi wa umma wanaofanya kazi kubwa, ngumu na wakati mwingine kwenye mazingira hatarishi ni askari wa Jeshi la Polisi.

Kazi ya kulinda raia na kupambana na wahalifu, wakati mwingine wakiwa na silaha nzito au hata mafunzo ya kijeshi ni kazi hatari sana na zipo taarifa ambazo tumeshuhudia askari wakipoteza maisha katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Wengi bado wanakumbuka tukio la Agosti mwaka jana wakati watu zaidi ya saba wanaosadikiwa kuwa majambazi walipowavamia askari polisi wanne na kuwaua pamoja na kujeruhi raia wawili baada ya watuhumiwa hao kuvamia eneo la Benki ya CRDB, tawi la Mbande lililopo Temeke, Dar es Salaam.

Na tukio la karibuni zaidi kati ya mengi ni lililojiri mwezi uliopita ambapo ofisa upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC-CID), Peter Kubezya aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akijaribu kupambana na wahalifu. Bila shaka ni kwa kutambua ugumu wa kazi hizo huku likilenga kunyanyua morari zaidi wa utendaji kazi, hivi karibuni Jeshi hilo liliwazawadia askari polisi 30 wa mkoa wa Mwanza kutokana na utendaji kazi uliotukuka.

Katika hafla hiyo ya kukumbukwa, Inspekta Jenerali wa Polisi, Ernest Mangu, aliwatunuku vyeti, fedha, mifuko ya saruji na Sh 500,000 taslimu askari hao kutokana na ushiriki wao katika kudhibiti matukio ya uhalifu. Hafla hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya polisi Mabatini ilihudhuriwa pia na maofisa wa ngazi za juu za jeshi hilo wa mkoa, askari polisi wa kawaida na wananchi.

Askari polisi hao pia walikabidhiwa vyeti, vitenge jozi mbili na seti ya vyombo vya chakula, vitu vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 30. Askari waliokabidhiwa zawadi hizo walitoka katika wilaya zote za mkoa wa Mwanza; Ukerewe, Nyamagana, Ilemela, Kwimba, Magu na Sengerema.

Huu ni mfano mzuri wa kuigwa uliooneshwa na Jeshi la Polisi nchini kwa kuwajali askari waliofanya vizuri kwa kuwatambua na kuwapa motisha wa fedha na zawadi, ambayo itawapa hamasa zaidi ya kufanya kazi. Baadhi ya Maaskari Polisi waliokabidhiwa vifaa na zawadi hizo ni Sgt John Ndomba (FFU), D/Sgt John Mpangala na D/ Cpl Samson Barnabas, wote kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO).

Halikadhalika, Sgt Mwajabu Bakari kutoka Kikosi cha Polisi Reli, D/Sgt John Waryoba kutoka Misungwi, D/Sgt Khadija Mtekateka- (Ofisi ya RCO), D/Sgt Nyasako Eseko na Sgt Hemed Mngoe wote kutoka wilayani Kwimba walizawadiwa pia.

Wengine waliokabidhiwa zawadi hizo ni Sgt Manase Simiyu na Koplo Flomena Masali kutoka Magu, Koplo Shaaban kutoka Ilemela, Koplo Clement Sambaa- Sengerema, Koplo Thomas Marwa kutoka ofisi ya RPC, Koplo Mswadiku Kempanju kutoka Ukerewe na D/Cpl Wilson Manyama kutoka Misungwi.

Akikabidhi zawadi na vifaa hivyo, IGP Mangu alisema Jeshi la Polisi limetoa zawadi kwa askari hao, ikiwa ni utaratibu wa jeshi hilo kutambua na kuthamini mtumishi wake pale anapokuwa amefanya kazi nzuri kwa kuzingatia kanuni na taratibu za utendaji kazi.

“Askari wetu anapofanya kazi vizuri tunamtambua kwa kumpatia zawadi na cheti. Tunafanya hivi ili iwe chachu kwa maaskari wengine, na sisi viongozi kazi yetu ni kuwajengea ujasiri maaskari wetu waweze kufanya kazi kwa kuwapa motisha,” alisema.

Anasema ni matumaini yake kuwa askari ambao hawakupata zawadi hizo ni wakati wao pia wa kuonesha utendaji kazi bora ili wawe kwenye orodha ya polisi watakaopata zawadi katika kipindi kijacho. Mangu pia anawapongeza wakazi wa mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano mzuri wanaoutoa kwa jeshi la polisi na kufanikiwa kudhibiti matukio ya uhalifu mkoani humo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi naye aliwapongeza askari hao kwa kufanya kazi vizuri kwa kuzingatia maadili ya jeshi la polisi. “Kwa namna ya pekee namshukuru sana Mkuu owa Jeshi la Polisi IGP Mangu kwa zawadi hizi alizotupatia,” alisema.

Alisema dhamira yake ni kuhakikisha kuwa jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linaendelea kutekeleza majukumu kwa kuzingatia weledi na misingi ya kazi, bila ya kumuonea raia.

Hata hivyo, alichukua wasaa huo kuwakumbusha wakazi wa mkoa wa Mwanza kuendelea kutoa taarifa za kiuhalifu ofisini kwake, ili kuwezesha kukamatwa kwa wahalifu zaidi kwani ni namna nzuri ya kutoa fursa ya wananchi kufanya shughuli za kiuchumi kwenye mazingira salama.

Kwa upande wake askari E2687, Koplo Shaabani Siyunga kutoka Ilemela alimshukuru Inspeka Jenerali Mangu kwa zawadi aliyompatia na kwamba anajisikia furaha na ataongeza juhudi zaidi katika kazi. “Namuomba Afande IGP aendelee na mtindo huu wa kutupatia zawadi kwa sababu unatupatia ari na hamasa ya kufanya kazi,” alisema.

Askari mwenye namba WP 3331 Sajenti Nyasato Makongoro kutoka wilayani Kwimba alimshukuru kwa kupatiwa zawadi ambazo pia alisema zitamungezea morali wa kazi.

Naye mfanyabiashara wa vyombo, Shija Kamalija (Vunjabei) ambaye alitoa zawadi ya seti 30 ya vyombo ya chakula zenye thamani ya Sh milioni 2.5, alisema ametoa zawadi hiyo kwa jeshi la polisi kutokana na kazi nzuri ya kudhibiti uhalifu na vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.

Baadhi ya wananchi walioongea na mwandishi wa makala haya, mbali na kupongeza hatua hiyo ya zawadi iliyofanywa na jeshi hilo, walisema siku hizi Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi nzuri huku likiwa karibu na wananchi kuliko huko nyuma. “Zamani jamii ililiona jeshi la polisi kama chombo cha hatari kwao cha kuwanyanyasa.

Hii ilitokana na baadhi ya askari kufanya kazi bila kuzingatia maadili huku wakitumia upolisi wao kunyanyasa wananchi,” alisema mmoja wa waliohudhuria hafla hiyo, James John, mkazi wa Mabatini. Alisema kuanzishwa kwa Mpango wa Polisi Jamii kulisaidia sana kulisogeza jeshi hilo karibu na wananchi na ndio maana kwa sasa linapata taarifa nyingi za wahalifu.