Mkaa nchini bado tishio kubwa kwa misitu

MAHITAJI ya mkaa na kuni nchini kwa sasa yanakadiriwa kufikia mita za ujazo milioni 62 kwa mwaka ambayo yanazidi kiwango cha kitaifa cha upatikanaji wa nishati hiyo kwa uendelevu.

Kiwango kinachotakiwa ni mita za ujazo milioni 43 na hivyo kuna ongezeko la mita za ujazo milioni 19 zaidi ya kiwango kinachotakiwa kuvunwa kwa mwaka. Kwa sasa mkaa ulio mwingi huzalishwa kwa kutofuata sheria na taratibu katika misitu ya hifadhi na misitu ya ardhi za vijiji ambayo haina mipango endelevu ya uvunaji. Kutokana na kukosekana kwa mipango ya uvunaji wa miti ya kutengeneza mkaa, shughuli hii imekuwa mojawapo ya chanzo kikubwa cha ukataji na uharibifu wa misitu.

Juhudi zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wadau wengine wa mazingira za kuzuia uzalishaji wa mkaa zimekuwa hazina mafanikio makubwa kwa sababu ya kukosekana kwa nishati mbadala ya kupikia kwa watu waishio mijini. Pamoja na matumizi ya nishati mbadala na majiko banifu yanayoendana na matakwa ya sera, wataalamu wanakiri kuwa mikakati hii haitoshi kukidhi mahitaji ya nishati katika miji mingi inayokuwa ingawaje miti ya kupanda inaweza kutoa suluhisho la upatikanaji wa miti kwa ajili ya nishati.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) unaotekeleza Mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa Tanzania kuhusu mfumo wa uzalishaji mkaa endelevu. Katika hotuba yake ya siku ya kitaifa ya upandaji miti Aprili mosi mwaka huu ( 2017), mkoani Morogoro, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe anasema, iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kupata nishati mbadala, matumizi ya mkaa nchini yataongezeka.

Kaulimbiu ya upandaji miti kitaifa mwaka huu ni: “Panda miti, Tunza Misitu upate Nishati”. Waziri anasema kaulimbiu hiyo ni zaidi ya kupanda miti na inaelekeza kuweka uzito wa kutosha katika suala zima la kutunza miti yote inayopandwa na pia misitu ya asili tuliyonayo. Profesa Maghembe anasema kwamba ongezeko la matumizi ya mkaa litafikia hadi tani milioni 4.6 ifikapo mwaka 2030 kutoka tani milioni 2.3 zinazokadiriwa kutumika nchini mwaka 2012.

Anasema nchi yetu ina vyanzo mbalimbali vya nishati kwa matumizi ya wananchi lakini nishati itokanayo na miti inafanya matumizi yanayofikia asilimia 85. Profesa Maghembe anasema nishati itokanayo na bidhaa za petroli ni asilimia 9.3, umeme ni asilimia 4.5 na makaa ya mawe na vyanzo vingine ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote. Anasema matumizi ya mkaa yamekuwa wakiongezeka siku hadi siku kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukuaji wa kasi wa miji yetu na ongezeko la watu, bei kubwa pamoja na uhaba wa nishati mbadala sambamba na umeme na gesi.

Profesa Maghembe anaonya hata hivyo kwamba hali hii ya matumizi makubwa ya mkaa itasababisha kupungua kwa eneo la misitu nchini na kuathiri maisha ya wanadamu na wanyama. Anasema mahitaji yetu ya nishati yanategemea nishati itokanayo na misitu, hivyo hatuna budi kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba nishati hii inaendelea kupatikana lakini katika misingi bora na endelevu kwa kuhakikisha misitu inaendelea kuwepo.

Profesa Maghembe anasema kitendo cha kupanda na kutunza misitu kitatuhakikishia upatikanaji endelevu wa huduma zote za kiikolojia zinazotokana na misitu, ikiwemo maji kwa matumizi ya nyumbani, viwanda, kilimo na uzalishaji wa nishati ya umeme. Huduma nyingine anasema ni mazao yatokanayo na misitu kama asali, dawa, uyoga, kutunza rutuba ya udongo pamoja na uboreshaji wa mifumo ya hali ya hewa itakayosaidia kutuepusha na matatizo yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.

Pamoja na hayo anasema, ipo haja ya kuweka suala la ulinzi wa misitu kuwa agenda ya kudumu katika shughuli zote za maendeleo katika mikoa, wilaya na vijiji na mkakati muhimu mmoja wapo ni kushirikisha jamii kama sera ya misitu inavyohimiza. Waziri Maghembe anatoa mwito kwa kusema ili kufanikisha upandaji miti nchini, kila familia ianzishe bustani ndogo ndogo za miche ya miti kwa ajili ya kupanda mashambani na kwa kufanya hivyo ni rahisi kuituza miche hiyo kwa kutumia maji kiasi kidogo.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, anasema ili kuweza kunusuru uharibifu wa misitu nchini anashauri mamlaka inayosimamia matumizi ya gesi nchini kujikita kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali kuhusu matumizi bora na sahihi ya gesi. Chonjo anasema, wananchi wengi waishio mijini na vijijini hawana uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya gesi na kwamba wapo wanaoogopa kuitumia.

Chonjo pia anaiomba wizara hiyo kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya majiko banifu kwa lengo la kunusuru misitu na kupitia upya sheria zake hasa ya matumizi ya misumeno ya moto inayoangamiza miti hasa vijijini kuonekana hazileti manufaa kwa wahalifu. Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen anasema mkoa huo inakabiliwa na athari za uharibifu wa mazingira hasa misitu ya asili.

“Ni vyema sasa wananchi tutunze misitu kwa ajili ya uhai wa mkoa wetu na taifa kwa ujumla, kwani sifa iliyokuwepo miaka ya 70 hadi 80 ilikuwa ni maji yatiririka milimani mwaka mzima. Sifa hii imetoweka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata misitu,” anasema Dk Kebwe. Pamoja na changamoto hizo anasema, upandaji wa miti kimkoa tawimu zimeonesha mwaka 2014/2015 miti milioni 4.4 ilipandwa lakini iliyoweza kuendelea kukua ni milioni 3.3 sawa na asilimia 73 ya iliyopandwa.

Katika mwaka 2015/2016 anasema jumla ya miti milioni 5.7 ilipandwa na iliyoweza kukua ni milioni 4.2 sawa na asilimia 74 ya miti yote iliyopandwa kipindi hicho, wakati mwaka 2016/2017 miti iliyokwishapandwa ni 280,000 na bado kazi hiyo ienaendelea. Mtendaji mkuu Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo anasema wakala unatambua wajibu wake wa kusaidia nchi kukabiliana na changamoto ya ukame ambao umekuwa tishio katika miaka ya hivi karibuni.

Profesa Silayo anasema, Wakala unaunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na janga la uharibifu wa mazingira ya misitu kwa kuanza kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya misitu inayosimamiwa. Anasema wakala umetoa utaalamu kwa wananchi na wadau mbalimbali wanaopanda miti maeneo yao na pia kuwapanga mameneja wa wilaya katika wilaya zote za Tanzania Bara.

Profesa Silayo anasema kwa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro wakala unasimamia msitu wa Serikali wenye ukubwa wa hekta 12,950 sawa na zaidi ya ekari 31,000 ukiwa na mpaka wa urefu wa kilometa 38.6 . Anasema msitu huo ulianzishwa Julai 17,1953 zamani ukijulikana msitu wa kuni Morogoro, na katika siku ya upandaji miti kitaifa wananchi wa wilaya ya Morogoro, Mvomero kwa kushirikiana na viongozi wa serikali walipanda jumla miti 1,200 eneo la ukubwa wa ekari moja.

Anasema TFS na wadau wake wameshapanda miti eneo la ukubwa wa ekari 125 sawa na hekta 50 ambalo limeandaliwa kupandwa miti kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 na kufikia Aprili mosi mwaka huu miti 55,000 imepandwa.

Profesa Silayo anasema msitu huo una bionuai nyingi za wanyamapori, ndege na miti ya asili kama mipingo na milama pamoja na aina nyingi za mimea inayopelekea eneo hilo kuhifadhiwa na pia ni ushoroba wa wanyamapori.