Yanga ilikimbiza mwizi kimyakimya

PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara linafungwa leo, baadhi ya timu zikitarajiwa kucheza kwa presha ya kushuka daraja, nyingine zikiwa zimeshajihakikishia kubaki msimu ujao huku Yanga na Simba zikitarajiwa kutazamwa zaidi jinsi zitakavyomaliza ingawa kwa uhalisia ni kama Yanga imeshakuwa bingwa.

Wakati ligi inaanza Agosti mwaka jana kuna timu zilianza kwa kasi kubwa na kutazamiwa kuleta mapinduzi makubwa. Lakini kwa kadiri siku zilivyosogea taswira halisi ilianza kuonekana na hivi ndivyo ilivyokuwa. Yanga, Simba Yanga ambayo ni kama imeshakuwa bingwa kwa pointi 68 katika michezo 29 aliyocheza, haikupewa nafasi kubwa ya kutetea taji lake kwani ilianza ligi vibaya wachezaji wakionekana wachovu na hata ushindi wao ulikuwa ni kama wa kubahatisha kwa baadhi ya mechi za mwanzo wa msimu.

Wengine wakisema kuwa labda kwa sababu walishiriki michuano ya kimataifa bila kupumzika na kukutana na ligi ni sababu ya wachezaji kushindwa kucheza kwa kiwango cha juu kama ilivyokuwa msimu uliopita. Mchezo wa kwanza Yanga ilishinda mabao 3-0 dhidi ya African Lyon lakini haitakaa isahau kipigo bao 1-0 dhidi ya Stand United kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga ambacho kiliwaumiza.

Kingine ni kile kilichowakuta Mbeya kwenye uwanja wa Sokoine walipofungwa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City. Vipigo hivyo vilisababisha watu kuinyooshea mkono timu hiyo kuwa haikuwa vizuri msimu huu. Mbaya zaidi Yanga licha ya kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu msimu huu, walikumbwa na majanga. Kwa mfano tatizo la wachezaji kukosa mishahara hasa baada ya Mwenyekiti wao, Yusuf Manji ambaye alikuwa ndio kila kitu, kujiweka pembeni kuihudumia timu hiyo.

Pia, walikwenda kushiriki michuano ya kimataifa kwa kusuasua hali iliyofanywa kushindwa kufanya vizuri kama ilivyokuwa msimu uliopita na hapo ndipo hisia za miamba hiyo kushindwa kutetea ubingwa wao zilipoibuka zaidi. Pamoja na changamoto nyingi walizopitia bado walifarijiana na wachezaji wao walijitahidi kupambana na leo kufikia ndoto yao ya kutetea taji la ligi kwa mara ya tatu. Yanga inatarajia kucheza na Mbao leo, mechi ya mwisho ya kufunga msimu kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Utakuwa mchezo wa kisasi baada ya Mbao kuiondosha Yanga kwenye michuano ya kombe la FA kwa kuifunga bao 1-0 kwenye uwanja huohuo wa CCM Kirumba. Katika mechi ya kwanza ya ligi, Mbao ililala kwa mabao 3-1. Lakini pia, iwapo Yanga itashinda kuna uwezekano mkubwa wa kuishusha Mbao FC daraja. Yanga leo ni kama haina cha kupoteza katika mechi hiyo kwa matokeo yoyote yale kutokana na hazina ya mabao iliyojiwekea.

Ili ikose ubingwa, Simba italazimika kuifunga Mwadui mabao 8-0 huku ikiiombea Yanga ifungwe mabao 5-0 na Mbao, jambo ambalo kiuhalisia ni gumu kutokea kutokana na mwenendo wa timu hizo katika mechi zake tangu kuanza kwa ligi, na hivyo kete ya ubingwa bado inabaki kwa Yanga. Mabingwa hao watetezi wapo kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 68, juu ya Simba yenye pointi 65.

Lakini Yanga bado ina jeuri ya kuwa bingwa hata kama Simba itashinda na yenyewe kufungwa, kwa vile Simba haijawahi kushinda zaidi ya mabao matatu katika mechi zake tangu ligi ilipoanza, hivyo suala la kuifunga Mwadui mabao manane leo litazua maswali mengi. Aidha, Mbao FC ni timu isiyotabirika. Ilianza vizuri ligi na imekuwa ikizikazia timu kubwa kuliko zile zinazolingana uwezo. Pia, inapokuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani CCM, Kirumba haikubali kufungwa kiurahisi.

Mbao inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 30. Salama yake leo ni ushindi tu ili isishuke daraja kwa vile haijapishana pointi nyingi na timu zilizo chini yake, Ndanda na Toto Africans. Ndanda ina pointi sawa na Mbao ikiwa nafasi ya 14 na Toto ni ya 15 ikiwa na pointi 29, kwa maana hiyo, timu yeyote itakayokosea hesabu zake za mwisho inaweza kushuka daraja na moja ikipatia inaweza kubaki ligi ya msimu ujao.

Leo, zinahitajika timu mbili zitakazoungana na JKT Ruvu kuhitimisha timu tatu zitakazoshuka daraja, kama kanuni zinavyosema. Ruvu ilishashuka muda mrefu. Kwa upande wa Simba, hakuna aliyetarajia kinachoonekana leo. Wekundu hao walikuwa wakipewa uwezekano mkubwa wa kuchukua taji la ligi baada ya kuanza msimu vizuri kabla ya baadaye kuvurunda. Simba ilikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tatu kwa muda mrefu kabla ya kupunguzwa kasi katika mechi zake za kanda ya Ziwa na hivyo kupoteza hesabu zake.

Timu hiyo inayosaka ubingwa bila mafanikio kwa karibu mwaka wa tano sasa, ilikosea hesabu ilipofungwa mabao 2-1 na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kabla ya kutoka suluhu na Toto. Kama hesabu za Simba zingeenda vizuri, ilihitaji pointi tisa za kanda ya Ziwa kutangaza ubingwa, kwa maana ya mechi dhidi ya Kagera, Toto na Mbao, lakini iliambulia pointi nne na ndio ikawa chanzo cha kupotea kwani mpinzani wake Yanga aliongeza mwendo kwa kushinda mechi zake tena kwa mabao mengi.

Simba inatarajia kumaliza dhidi ya Mwadui FC katika mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mechi ambayo kwa hakika ahiitaji nguvu nyingi kwani kiuhalisia haiwezi kuwa bingwa hata ikishinda, na haina uwezo wa kufunga mabao zaidi ya matatu, hivyo mechi hiyo inahitaji ushindi ili kulinda heshima na si kingine. Pengine hesabu za Simba zilianza kupotea tangu ilipopoteza mechi yake ya 14 kwa kufungwa bao 1-0 na African Lyon, baada ya kucheza mechi 13 mfululizo bila kupoteza.

Kufungwa huko kuliwaathiri Simba kwa kiasi fulani kwani ushindi mfululizo ulionyesha matumaini kuwa baada ya kukosa ubingwa wa ligi misimu minne, sasa wanahitaji lakini kwa bahati mbaya mambo yalikwenda tofauti na ilivyotabiriwa. Ni kama African Lyon waliwaharibia kwani walipokwenda Mbeya wakafungwa tena mchezo dhidi ya Tanzania Prisons mabao 2-1. Kufungwa huko kukaanza kupunguza pengo la pointi kutoka kwa wapinzani wake Yanga na Azam ambao waliachwa mbali.

Azam FC Azam FC inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi 52 ilishindwa kuendana na kasi ya Yanga na Simba. Timu hii msimu huu haikuwa vizuri kama ilivyotarajiwa mwanzoni mwa msimu licha ya kuwa ilifanya matumizi makubwa ya fedha kwenye usajili. Timu hii pamoja na jitihada za kubadilisha Makocha wakiondolewa Wahispania na wa sasa ni Mromania bado hakuna mabadiliko yoyote. Kutokana na ubovu wake, hakuna ilichoambulia zaidi ya kubaki salama kwenye nne bora.

Haina nafasi yoyote ya kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kupoteza pia, kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (FA). Kagera Sugar Ukilinganisha msimu huu na ule uliopita mambo ni to- fauti. Kagera imeimarika vizuri na kumaliza kwenye nne bora. Mchezo wa mwisho wanatarajia kucheza dhidi ya Azam FC. Yeyote akishinda au kufungwa wataendelea kubaki kwenye nafasi hizo za juu. Kocha Mecky Maxime amekuwa mbunifu na muibuaji wa vipaji.

Amesaidia timu hiyo kurudi katika kiwango bora msimu huu baada ya ule uliopita kunusurika kushuka daraja. Mtibwa Sugar Ilianza vizuri msimu lakini baadaye ikajikuta kwenye wakati mgumu. Baada ya kuondoka aliyekuwa Kocha wao wa muda mrefu Maxime, iliyumba kidogo lakini ikarudi ikiwa chini ya Kocha Salum Mayanga kabla ya kuondoka na kujiunga na timu ya taifa. Mtibwa baada ya kukabidhiwa Zuberi Katwila ilicheza kwa kuyumba na kushinda michezo michache.

Lakini bado wanajivunia kubaki nafasi ya tano ambayo imewahakikishia nafasi ya kurudi msimu ujao. Leo inatarajia kucheza dhidi ya Toto Africans ambao wako hatarini kushuka daraja. Mtibwa haina cha kupoteza hivyo presha kubwa itakuwa kwa Toto wanaohitaji ushindi kubaki salama. Toto ina pointi 29 hivyo, ikishinda itafikisha jumla ya pointi 32. Ruvu Shooting, Mwadui, Stand United, Mbeya City na Prisons Timu hizo zina nafasi ya kubaki. Ruvu leo itacheza dhidi ya Stand United.

Zote ziko salama isipokuwa kila mmoja akishinda ni kwa ajili ya kuweka heshima zaidi. Tanzania Prisons yenye pointi 34 dhidi ya African Lyon yenye pointi 31. Timu yenye presha ni Lyon ambayo inahitaji pointi zaidi kujihakikishia nafasi ya kubaki kwenye ligi. Pointi 31 hazitoshi kumuweka salama. Iwapo itapoteza basi itakuwa kwenye nafasi ya kushuka daraja. Mbeya City yenye pointi 33 itachuana na Majimaji yenye pointi 32. sare huenda ikawabeba wote kuendelea kubaki salama kwenye ligi.

Lakini Majimaji ikifungwa itakuwa zaidi hatarini. Mwadui yenye pointi 35 tayari imeshavuka hatari. Ishinde au ifungwe haina cha kupoteza. Inacheza na Simba ambao wanahitaji pointi tatu za heshima kulingana na Yanga. Hatarini Kama ambavyo nimesema huko juu timu ambazo ziko hatarini ni Majimaji, African Lyon, Mbao, Ndanda na Toto Africans.

Tayari JKT Ruvu imeshashuka daraja hivyo inasubiri timu mbili kuungana nazo. JKT Ruvu inatarajia kucheza mchezo wa mwisho dhidi ya Ndanda FC yenye pointi 30. Kwa hivyo, Ndanda ni wazi kuwa inapewa uwezekano wa kushinda mchezo huo na kujinusuru kwenye hatari.