RIADHA KIMATAIFA: Sasa ni zamu ya Tanzania

‘SASA ni zamu yetu’. Huo ni usemi unaotumiwa sasa na Riadha Tanzania (RT) ukiwa na maana kuwa, sasa ni zamu ya Tanzania kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Wanariadha wa Tanzania sasa wameanza kurejea kwa nguvu katika mashindano mbalimbali ya kimataifa baada ya muda mrefu wa kupotea kwao.

Wanariadha wa Tanzania walikuwa hawapati mialiko ya maana katika mbio kubwa kutokana na kufanya vibaya kwa muda mrefu. MASHINDANO YA VIJANA Tanzania mwaka huu ilikuwa mwenyeji wa mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia Mei 13 na 14.

Nchi za Ukanda wa Tano ziko 11 lakini katika mashindano hayo mwaka huu zilishiriki saba, ikiwa ni zaidi ya nusu ya timu zote. Nchi zilizoshiriki ni pamoja na wenyeji Tanzania, Zanzibar, Kenya, Eritrea,Sudan, Sudan Kusini na Somalia wakati Djibout, Ethiopia, Rwanda na Uganda hazikushiriki kwa sababu tofauti.

Kiujumla ukiondoa kasoro chache za hapa na pale, mashindano hayo yalifanyika kwa mafanikio makubwa na kumwagiwa sifa karibu na washiriki wote. TIMU YA TAIFA TANZANIA Timu ya taifa ya Tanzania iliundwa na wanariadha 23, ambapo 12 walikuwa wanaume na 11 wanawake, ambao walishiriki katika michezo mbalimbali.

Wanariadha wa Tanzania walifanya vizuri katika mashindano hayo baada ya kukosa kidogo tu nafasi ya kwanza iliyochukuliwa na Kenya huku wao (Watanzania) wakimaliza katika nafasi ya pili.

Ni kweli Tanzania ilikosa kidogo tu nafasi ya kwanza kwani kama ingeweza kutwaa medali ya dhahabu katika mchezo wa mwisho wa kupokezana vijiti kwa wavulana, ingeipita Kenya.

Timu hiyo ilipiga kambi katika hosteli za Filbert Bayi zilizopo Mkuza, Kibaha mkoani Pwani, ambapo walipata huduma zote muhimu. Wachezaji na makocha wa timu hiyo wanakiri kuwa kuanzia malazi, sehemu ya kufanyia mazoezi kama gym hadi chakula, vyote vilikuwa vizuri.

Kocha wa timu hiyo Robert Kalhae anasema kuwa kambi ilikuwa nzuri iliyokamilika katika kila idara kuanzia malazi, chakula, vifaa vya mazoezi na utulivu ulikuwa wa hali ya juu. USHINDI WA TANZANIA Tanzania katika mashindano hayo ilitwaa medali saba za dhahabu, medali za fedha saba na shaba mbili, ambapo jumla ya medali zote walizotwaa ni 18.

Wakati Kenya wenyewe katika ushindi wa jumla walitwaa medali za dhahabu nane, fedha nne na saba tatu, zikiwa jumla ya medali 15 na kutwaa nafasi ya kwanza. Kwa upande wa wanawake, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza baada ya kutwaa jumla ya medali 12 zikiwemo tano za dhahabu, nne za fedha na tatu za shaba.

Kenya kwa upande wa wanawake, wenyewe walikuwa wa pili baada ya kujipatia medali nne za dhahabu, tatu za fedha na mbili za shaba, wakikamilisha jumla ya medali tisa. Kwa wanaume, Tanzania kwa upande huo ilimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kutwaa medali mbili za dhahabu, tatu za fedha na moja ya shaba wakiwa na jumla ya medali sita.

Kenya wenyewe kwa upande huo walimaliza katika nafasi ya pili huku wakitwaa medali nne za dhahabu, moja ya fedha na moja ya shaba wakiwa na jumla ya medali sita. Zanzibar ndio walioongoza kwa upande wa wanaume baada ya kupata jumla ya medali nane, zikiwemo nne za dhahabu, tatu za fedha na moja ya shaba.

WALIONG’ARA ZAIDI

Wanariadha wawili wa Tanzania, Donat Nagabona na Rose Seif waling’ara zaidi katika mashindano hayo baada ya kutwaa medali nne na tatu katika michezo tofauti tofauti. Nagabona alitwaa jumla ya medali nne, zikiwemo tatu za dhahabu katika mbio za kupokezana vijiti za meta 4x100 na 4x400 na zile za meta 200 wakati medali ya fedha aliipata katika mbio za meta 400.

Naye Seif alipata medali tatu za dhahabu katika michezo ya kuruka juu, mbio za meta 400 na zile za kupokezana vijiti za meta 4x100 na meta 400. Wachezaji hao pamoja na wengine wa Tanzania walifanya vizuri katika mashindano hayo, ambayo yalifanyika kwa mafanikio