Wazawa wakimbiza msimu huu

MISIMU kadhaa iliyopita ilikuwa ikionyesha taswira kuwa wachezaji wa nje wana uwezo kuliko wa ndani hasa katika suala la upachikaji wa mabao. Kitendo hicho kilionyesha wazi kuwa washambuliaji hata mawinga wa ndani hawawezi kutamba mbele ya wachezaji wa kigeni.

Kumbe sasa wamebadilika na kuonyesha dhahiri kuwa wachezaji wa ndani wanajifunza kutoka kwa wale wanaotoka nje. Tayari wanatambua nini maana ya ushindani katika kupachika mabao. Katika orodha ya wanaoongoza kwa kufunga mabao imetawaliwa na wachezaji wa ndani huku wale wa nje wakiwa wachache. Ingawa bado hakuna anayejua nani ataibuka mfungaji bora msimu huu, kwani baada ya mechi za leo itajulikana atakayeondoka na kiatu cha dhahabu.

Mpaka sasa winga Simon Msuva anashikilia usukani wa ligi akiongoza kwa kufunga mabao 14. Mchezaji huyu alianza kufanya vizuri msimu wa mwaka juzi baada ya kuibuka mfungaji bora kwa mabao 17. Pengine kama Msuva angecheza mechi iliyopita dhidi ya Toto Africans na kufunga angeongeza mabao lakini kutocheza kwake kulimpa nafasi zaidi Amisi Tambwe aliyefunga bao pekee katika mchezo huo.

Pia, Yanga inatarajia kucheza leo dhidi ya Mbao FC ya Mwanza. Huenda Msuva kama atacheza akafunga na kuendelea kuongoza katika orodha lakini itategemea na wapinzani wake kama nao watashinda katika michezo yao kutegemea na idadi ya magoli. Kuna uwezekano mkubwa wa Msuva kushushwa katika nafasi hiyo ya kuongoza katika upachikaji mabao kama mpinzani wake Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting atapata nafasi ya kufunga katika mchezo wa leo.

Mussa anashika nafasi ya pili akiwa ameifungia timu yake mabao 13. Mchezaji huyo amekuwa tishio na anakuja kwa kasi ya ajabu. Timu yake itacheza leo dhidi ya Stand United ukiwa ni mchezo wa mwisho wa msimu utakaochezwa kwenye uwanja wa CCM, Kambarage, Shinyanga.

Ikiwa ataibuka mfungaji bora msimu huu atakuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kutoka timu nyingine nje ya Simba, Yanga na Azam tangu ilipowahi kutokea kwa Abdallah Juma mwaka 2006 alipoibuka mfungaji bora akitokea Mtibwa Sugar. Juma aliyekuwa mchezaji wa Mtibwa Sugar aliwahi kuongoza kwa kufunga mabao 20.

Ndiye mchezaji pekee wa Tanzania aliyefunga mabao mengi kwa kuhesabu kuanzia mwaka huo 2006. Kwa wachezaji wa nje waliovunja rekodi yake ni Mrundi Tambwe msimu uliopita aliyefunga mabao 21. Mchezaji anayefuatia ni Mbaraka Yusufu wa Kagera Sugar. Hiki ni kipaji kingine kilichokuja kwa kasi msimu huu. Mshambuliaji huyo ameifungia timu yake mabao 12 mpaka sasa. Timu yake inatarajia kucheza leo dhidi ya Azam FC kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Iwapo atashinda magoli mengi basi pengine yeye akaibuka mfungaji bora. Bado kazi itakuwa ngumu kwa Obrey Chirwa mwenye magoli 12. Lakini ana nafasi ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho kama atasaidia timu yake kushinda leo katika mchezo mgumu dhidi ya Mbao FC utakaochezwa jijini Mwanza. Wote wawili Chirwa na Yusuf wana kazi kuwafikia Msuva na Mussa kwani wanatofautiana magoli mawili kwa moja.

Anahitaji kufunga magoli mengi. Pia,Tambwe mwenye magoli 11 inawezekana kukaa nje muda mrefu kwa majeruhi kumepoteza nafasi yake ya kuendelea kuongoza kwa upachikaji wa mabao. Msimu uliopita alikuwa na magoli 21. Pengine katika mechi hii ya mwisho akafunga zaidi. Lakini tayari ametolewa katika kinyang’anyiro hicho baada ya kuachwa nyuma kwa tofauti ya mabao matatu dhidi ya kinara, Msuva.

Mchezaji mwingine ni Shiza Kichuya wa Simba. Ana magoli 11 hivyo anahitaji kufunga magoli matatu zaidi katika mchezo wa mwisho dhidi ya Mwadui ili kuongoza. Mchezaji huyo hajafunga muda mrefu huenda katika mchezo wa leo miujiza ikatokea. Lolote linawezekana. Pia, Rafael Daud wa Mbeya City ana mabao tisa, akifuatiwa na John Bocco wa Azam na Kelvin Sabato wanaolingana.

Donald Ngoma wa Yanga na Mzamiru Yasin wa Simba wana magoli manane kila mmoja na tayari wameachwa mbali. Hawana nafasi labda kujipanga zaidi kwa msimu ujao kama wataendeleza viwango vyao. Wengine waliopo kwenye orodha wakifunga mabao saba kila mmoja ni Rashid Mandawa wa Mtibwa Sugar, Riffat Khamis wa Ndanda, na Ibrahim Ajibu wa Simba.

Waliofunga mabao sita kuna Haruna Chanongo wa Mtibwa, Omar Mponda wa Ndanda, Peter Mapunda wa Majimaji, Shaban Idd wa Azam na Victor Hangaya wa Tanzania Prisons. Kwa kutazama orodha hiyo inaonyesha kuwa washambuliaji wa Tanzania wanajitahidi kwa kiasi fulani na kuna uwezekano mkubwa wa mchezaji atakayechukua kiatu akatokea nyumbani.

Na kwa kutazama orodha hiyo wapo ambao wataingia sokoni muda sio mrefu baada ya ligi kumalizika kutokana na kucheza kwa viwango vya juu katika timu wanazotumikia. Mfano Msuva, Mussa, Mbaraka Yusuf, Rafael Daud ni miongoni wanaotajwa kuondoka katika klabu zao baada ya msimu kuisha. Wakitarajiwa kusajiliwa na klabu za ndani na nje ya nchi.