BONGO MOVIE: Walicheza na kima sasa wanavuna mabua

NAWEZA kusema hatimaye wasanii wamekubali kwamba vita hii ya kupambana juu ya filamu za kigeni imewashinda, kilichobaki wanasubiri kudra ya Mwenyezi mungu kama sio ya Serikali itakayoweza kuwasaidia kwakuwa nguvu zao ndipo zilipoishia.

Nikiwa kama mdau wa Tanzania mpya ya Viwanda, Tanzania ya watu kujiajiri wenyewe sina furaha yoyote, kwa kuwa duka kubwa linalosambazasa filamu Kariakoo la kampuni ya Steps Entertaiment limefungwa rasmi na watu kupoteza ajira zao kuanzia kiwandani na hata madukani.

Najua watafutaji na wahangaikaji kama mimi waliokuwa wakifanya kazi ya kupakia filamu, kubeba na kusafirisha filamu, kuigiza, kutengeneza filamu, kusambaza filamu Kariakoo, “kuprint Cd”, kubandika na kusambaza vipeperushi watakosa kazi. Pia wale ambao wapo katika Bodi ya Ukaguzi wa Filamu najua walikuwa wakitoza kwa dakika, zile stika za TRA, Baraza la Sanaa Tanzania ëBasataí na wengine ambao Wizara iliwaandaa kushughulikia masuala yote ya filamu watakuwa wamepumzika kusumbuliwa na Bongo Movie.

Nilishawahi kuandika makala kadhaa nikielezea kwanini tasnia inakufa jinsi wasanii wanavyosababisha tasnia kufa, na jinsi wasambazaji wanavyosababisha tasnia kufa. Kweli haikuwa suluhisho lakini wangeanza na ule udodoso niliowapa na wangefanya na uchunguzi kabla ya kupambana vita ingewapa majibu ya wapi waanze kupambana na vita hii.

Ukiwa kama msanii na mdau wa filamu wacha nikuambie kuna vita nne ndani ya vita moja, ambao wasanii wenyewe walikuwa wakipigana bila kujua. Wasanii walikuwa hawajui kwamba kulikuwa na vita kuu nne, ya kwanza ikiwa vita ya Wasanii kwa wasanii, ya pili ikiwa vita ya wasanii na wanasiasa, ya tatu ikiwa vita ya wasanii na wananchi, lakini vita ya nne na ndio vita ya mwisho ilikuwa wasanii na wasambazaji wa filamu za kigeni.

Hii vita ya nne ambayo ya wasanii na wasambazaji wa filamu za Kizungu ilibidi iwe ya mwisho katika vita yao, lakini kwao ilikuwa ya kwanza huku wakisahau kwamba kuna vita zingine ambazo wao iliwapaswa wapigane wao kabla ya kwenda huko.

Labda nianze kufafanua hizi vita na kwanini zilisababisha wasanii kuua tasnia wenyewe, nikianza vita yao wenyewe kwa wenyewe ambayo ndiyo vita iliyoanza muda mrefu kabla ya vita zote.

Kipindi nikiwa mwandishi wa muswada “Skripti” wa mwigizaji Issa Mussa “Cloud 112”, nilikuwa karibu na wasanii wote, nikaweza kuona utofauti wao. Ila ninachokumbuka wasanii wachanga waliokuwa wakipata nafasi ambapo kama nilivyowahi kueleza katika makala za nyuma, walikuwa wakionesha wao wana nguvu kuliko wasanii wakongwe. Leo nakumbuka kauli ya Jacob Steven, JB, alishawahi kuwaambia, kwamba “tuheshimiane japo kwa ukongwe wa tasnia, lakini kama haitoshi japo ukongwe wa umri”.

Niliona chuki zilizokuwa zikijificha ndani yao hasa ya kuwania kuuza katika kampuni kubwa ya usambazaji wa filamu Tanzania ya Steps Entertainment, huku kila mmoja akimfanyia mwenzake fitina asifike pale. Chuki ile ilisababisha wenye filamu nzuri na wenye filamu mbaya kutofahamu nani ni nani, isipokuwa kulionekana ukubwa wa tabaka wa wanaosikilizwa na wanaopuuzwa.

Hapa tayari filamu zilikuwa zikiuzwa kwa jina la kampuni na sio kwa jina la mtu, hivyo wasanii walijua wakiuza katika kampuni hiyo wanapata manufaa zaidi kuliko kampuni zingine. Ile chuki ilijaa moyoni mwa baadhi ya wasanii wakajikuta wanaanza kujiengua mapema, ndipo baadhi ya wasanii tukawa hatuwasikii. Lakini sio kwamba walijiengua walikuwa hawajapata nafasi ya kuuza katika kampuni kubwa, ila walikuwa wakidai maslahi yao ambayo walipohisi hawawezi kuyapata walionekana kuamua kufanya ishu nyingine.

Sasa kundi hilo likaanza kuwa kubwa kwa kuwa wasanii walianza kujitokeza wale walionyimwa mkataba kwa kudai haki zao, wale waliokuwa wakifanya kazi kwa nguvu zao na walipozifikisha pale zilikaa kwa zaidi ya miaka, wale waliokuwa wakidai fedha walikuwa wakisumbuliwa.

Pia wapo wale ambao walikuwa wakipanga foleni kuonana na bosi msanii mkubwa akija anapita bila ya kusubiri wakati hata wao wametoka mbali na tasnia, wapo ambao walikuwa wakiambiwa hawauzi lakini sokoni wanasifiwa.

Wapo ambao walikuwa wana chuki binafsi kwa kuwa kazi zao hazina ubora na walipoambiwa walinuna kwa kuwa wana nguvu katika baadhi ya sekta Serikalini kulingana na urafiki au ndugu katika sekta hizo.

Wote hawa na wengine wenye chuki za namna hiyo walijikuta wakiichukia kampuni ya Steps Entertainment na kampuni zingine ndio hawa leo walioamua kutumia nguvu zao kuhakikisha kwamba vita hii haifanikiwi.

Kwa kuwa waliamini kufanikiwa kwa vita hii ndio kufanikiwa kwa kampuni ya Steps Entertainment ambayo tayari kwao wanaiona kama adui wao, huku wakisahau kwamba kila kampuni ina utendeji wake katika kujiendeleza yenyewe.

Hiyo ndiyo vita ya wasanii kwa wasanii robo tatu ya wasanii ninaowauliza juu ya vita ya filamu za kigeni au maandamano wanasema wameyaona kwenye runinga na mitandao ya kijamii.

Wanadai eti kama kweli vita hii ni haki yao inapaswa kupiganiwa na wasanii wote, kwanini wasiitane kwa pamoja na kutoa tofauti zao bila ya kumuhusisha mfanyabiashara. Wanadai kwanini wasingekutana viwanja vya Leaders wasanii wa itikadi zote, dini zote, vyama vyote, kampuni za usambazaji tofauti bila ya kuhusishwa wafanyabiashara?

Wao ndio wataamua kwa moja, nguvu na kauli zao wamfuate nani wamsaidie, wachangaje fedha na wapambanae kwa njia ipi? Kuliko kumshirikisha mfanyabiashara kwa kuwa atazidi kuwa juu yao kwa kuwa atasema anatumia fedha zake.

Mimi sijui ukweli upo wapi kwa kuwa wasanii wengi wanadai kwamba maandamano yaliyofanyika wengi waliyashitukia yakifanyika, hawakuwa na taraifa miongoni mwao ni Haji Adam, mwenyekiti wa wasanii wanawake Ndumbangwe Misayo, Amri Athumani “King Majuto”, Aisha Bui, Shamsa Ford, Steve Nyerere na wengine.

Kutokana na hayo wanasema tatizo la soko la filamu halipo katika filamu za kigeni ila wasanii wenzao wanatumiwa na baadhi ya wafanyabiashara ya filamu katika kupigania maslahi yao katika soko. Maneno hayo sio kwamba wananiambia mimi na wewe la hasha, wanazungumza kwa viongozi, mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari.

Kiongozi akisikia hayo anajiuliza namsaidia msanii au nasaidia kampuni, ndio maana leo msanii akienda kuomba asaidiwe kuinua tasnia mwingine anaenda anasema kingine kwamba huyo anatumika.

Tena wasanii hao wana nguvu ya kauli kutokana na ukaribu wao na viongozi na wengine ukongwe wao katika tasnia pia hata sababu wanazozitetea kwa nguvu zinaleta ushawishi ukizingatia na historia ya nyuma ya soko la filamu.

Kikwazo cha pili nilisema ni wasanii na wanasiasa hili sitaki kuingia sana ndani, kwa kuwa nisije kuleta mambo mengine lakini wakubali wakatae wanajaribu kuruhusu siasa iingie katika hii vita. Nikipitia juu juu kwamba Katika kampeni ya mwaka 2015 wasanii walijiingiza katika siasa kulingana na itikadi zao za kichama jambo ambalo lipo katika nchi zote duniani.

Hiyo haikatazwi kwa kuwa siasa ni maisha ya mtu ukiachilia mbali sanaa yake, ndio maana tutaendelea kusikia waigizaji wakubwa duniani wanawania viti tofauti vya uongozi wa juu katika nchi zao akiwemo Kanye West aliyetangaza mara kadhaa kuwa na mpango wa kuwania urais wa Marekani. Lakini kibaya ni msanii kuruhusu kutumiwa kisiasa wakati wewe hujaamua kuwa mwanasiasa au kujitokeza katika mechi zinazochezwa na wanasiasa.

Leo kuna wasanii wa filamu wanajaribu kujibu mashambulizi ya kisiasa, tena wengine wakijibu vitu ambavyo wanasiasa ilibidi wajibu wanasahau hii ni siasa ya Afrika. Wengine wanapewa mialiko na wanasiasa wakiwa kama wasanii lakini wanashindwa kuhudhuria kwa kuwa wao wanamuunga mkono mwanasiasa fulani.

Sasa baadhi ya wanasiasa wanaendeleza msemo “Wamecheza na kima, watavuna mabua” ndio maana wanaacha soko life na unapoingilia kati kuzuia wanakuwa wakali kama moto wa kifuu.

Kwenye siasa sitaki kuendelea zaidi kwa kuwa wapo wasanii wenyewe wanaojijua kwamba walikubali kutumika kisiasa japo sekunde kwa mwanasiasa ndani ya mgogoro wa kifilamu na kusahau kwamba tasnia ni kazi yake. Wacha niishie hapa nikipata wasanii nitaendelea wiki ijayo, kwa kuwa bado nina mengi kwanini vita ya wasanii juu ya kuinua tasnia ya filamu inashindikana.