Mauaji ya Soweto na tafakuri ya kumlinda mtoto wa Afrika

LEO ni Siku ya Mtoto wa Afrika. Hii ni siku ambayo Tanzania inaungana na mataifa mengine barani kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto, Afrika Kusini waliouawa siku kama ya leo, mwaka 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.

Maadhimisho haya yanatokana na azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kuwakumbuka watoto hao mashujaa. Iliazimia Juni 16 kila mwaka, iwe Siku ya Mtoto wa Afrika. Watoto hao waliokuwa wakipinga mifumo ya elimu ya kibaguzi.

Walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu sawa na bora. Mauaji hayo kwa wanafunzi 170 yaliyofanywa na askari wa utawala wa makaburu, yaligeuka kuwa kichocheo cha harakati za uhuru kwa Afrika Kusini.

Wanafunzi hao waliandamana kupinga uamuzi wa serikali ya makaburu kutaka lugha ya Kiafrikana ifundishwe shuleni. Simulizi zinasema, watu walishangazwa kuona wanafunzi waliokuwa na sare za shule walibeba mabango yaliyolaani ubaguzi wa rangi.

‘Kiafrikana kinanuka…Kiafrikana kinatakiwa kuondolewa’, baadhi ya mabango yalisomeka hivyo. Katika maandamano hayo yaliyoanzia katika shule ya sekondari ya Orlando, ambayo wanafunzi waliimba na kucheza, polisi walifika.

WaliWApa watoto dakika kadhaa za kuondoka na walipokataa, waliwafyatulia risasi zilizosababisha vifo hivyo vya wanafunzi wapatao 170. Tukio hili lililoandika historia ya machozi siyo tu kwa wazazi, walezi, bali pia kwa kila binadamu mwenye utu, linaendelea kuleta tafakuri juu ya ulinzi wa watoto na kukabili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kutishia ustawi wao.

Watoto hawa wanaenziwaje? Ndiyo maana, katika maadhimisho ya mwaka huu, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya anaikumbusha serikali na wadau wengine kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Afrika na kuzitafutia ufumbuzi.

Maadhimisho haya ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa sera za taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki, ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na taifa kwa ujumla. Dk Ulisubisya anasema mwaka huu maadhimisho haya yatafanyika kimkoa hivyo kila mkoa utaadhimisha siku hii kwa kuzingatia mazingira yake.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto.’ Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Wizara inatoa mwito kwa wanahabari, asasi za kiraia na wadau wengine kushirikiana na serikali katika kuadhimisha siku hii na kuelimisha jamii kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu. Utekelezaji wa kaulimbiu hii utasaidia kuimarisha ulinzi, usalama wa mtoto na kutoa haki sawa kwa watoto wote kwa lengo la kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030.

Aidha Dk Ulisusibya anawakumbusha Watanzania wote kutambua kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao za msingi kuanzia katika ngazi ya familia ambayo ni kitovu cha maendeleo ya mtoto, jamii na taifa kwa ujumla.

Mtoto ni nani? Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na Mkataba wa Kitaifa wa haki za Mtoto wa mwaka 1989, mtoto ni kila binadamu aliye chini ya umMimba za utotoni Miongoni mwa mambo ambayo yanapaswa kupewa tafakuri na kuyapiga vita, ni pamoja na mimba za utotoni.

Mkoa wa Rukwa unaadhimisha siku hii ya mtoto huku ukikabiliwa na changamoto ya utatuzi wa ndoa za utotoni. Kwa hiyo katika kuadhimisha siku hii, wadau wa haki na maendeleo ya mtoto, wanapaswa kutafakari juu ya namna ya kukabili mambo yanayochochea ndoa hizo za utotoni. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na tamaa ya mali, umaskini, elimu duni, mila kandamizi na mfumo dume ndani ya jamii .

Shirika la Plan International Tanzania limepata ufadhili wa kuendesha mradi wa kampeni dhidi ya ndoa za utotoni. Mradi huu ambao unafadhiliwa na na Shirika la Maendeleo la NORAD, kauli mbinu yake ni ‘Tuwajengee Uwezo Wasichana, Tushirikiane, Kuzuia Ndoa za Utotoni.

Mauaji ya Soweto na tafakuri ya kumlinda mtoto wa Afrika Inatoka Uk. 13 Mradi ulioanza kutekelezwa mwaka 2019 katika kata za Mtenga, Mkwamba na Nkandasi zilizopo katika wilaya ya Nkasi, utahitimishwa mwaka 2019.

Meneja wa Plan International Tanzania Wilaya ya Nkasi, William Mtukanaje anasema kuwa tatizo la mimba za utotoni wilayani humo ni kubwa. Anasema utafiti ambao shierika limefanya, umebaini wapo watoto wenye umri wa miaka 14 walioolewa. “Madhara yake kiafya kwa watoto hao ni kubwa,” anasema akitaja kuwa miongoni mwa hatari zinazowakabili, ni matatizo katika uzazi yanayoweza kusababisha vifo.

Anaelezea kuwa, mjamzito mwenye umri chini ya miaka 18, kawaida via vyake vya uzazi havijakomaa kiasi cha kuhimili heka heka za uzazi . “Tatizo hili la ndoa za utotoni zinasababishwa na utamaduni ndani ya jamii ambapo unaruhusu mtoto wa kike akivunja ungo lazima aolewe,” anasema.

Anaongeza, “Pia umasikini, unakuta wazazi wa mtoto wa kike ambao hawajawahi hata kumiliki kuku hata mbuzi akipewa ng’ombe watano tu kama mahari wanaridhia mtoto wao mwenye umri wa chini ya miaka 18 aolewe,” anaeleza.

Anasema iwapo mtoto wa kike akimaliza elimu ya msingi akishindwa kujiunga na kidato cha kwanza wazazi wake hawamsaidii kuhakikisha anaendelea na masomo yake, matokeo yake anaolewa akiwa katika umri mdogo hivyo kukatiza ndoto zao za maisha.

“Jamii ijue kuwa watoto kuolewa mapema wakiwa na umri mdogo unaowasababishia umaskini wa kudumu kwa kuwa ndoto zao zinaishia hapo hawawezi tena kuendelea na masomo isitoshe mdhara yake kiafya ni makubwa ikiwemo vifo vinavyosababishwa na uzazi , fistula kwa kuwa via vyao vya uzazi bado ni vichanga,” anasema Mtukanaje.

Anasema kutokana na tatizo hilo la ndoa za utotoni katika wilaya ya Nkasi, Plan International Tanzania kupitia mradi wake, linaendesha kampeni kuhakikisha vitendo vya kuozesha watoto chini ya umri wa miaka 18, vinakoma.

Kwa mujibu wa Mtukanaje, kupitia mradi huo, watoto 116 kutoka katika kata tatu za Mtenga, Mkwamba na Nkandasi zilizoko wilayani Nkasia, waliobainika kuwa katika mazingira ya kuathirika na ndoa za utotoni wanapatiwa mafunzo mbalimbali ikiwemo ufundi umeme, ushonaji na mapishi waweze kujiajiri.

Wakati lengo la shirika ni kufikia watoto wengi zaidi, anasema kuwa kupitia mradi huo, pia wanazungumza na viongozi wa kimila, viongozi wa kidini na serikali waweze kuchukua hatua ambazo zitawawezesha wasichana kiuchumi na kuzuia ndoa za utotoni.

Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii, Manispaa ya Sumbawanga, Hassan Kimaro anaelezea nafasi yao katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika na kusema, watakutanisha mabaraza ya watoto kutoka kata 19 zilizopo kwenye manispaa hiyo.

Wataelimishwa kuhusu haki zao za msingi na wajibu wao ikizingatiwa madhira ambayo wamekuwa wakiyapata shuleni, mitaani na hata nyumbani huku wakiwa hawana mahala pa kusemea. Lengo ni kuwawezesha watoto wafahamu vitendo mbalimbali wanavyofanyiwa kama ni sahihi au la. Wanajengewa uwezo wa kuwa mawakala, wanaharakati na mabalozi wa wenzao katika kufichua ukatili wowote watakaotendewa.

Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Kiuchumi, Manispaa ya Sumbawanga, Mtatiro Linti anasema manispaa hiyo iko katika kuuanda majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika kata 19 zilizopo kwa kuwa watetezi wakubwa wa watoto ni akina mama.

Anasema lengo ni kuwasaidia wanawake kujua fursa za kiuchumi. Wakati serikali ikiwa na nafasi yake ya kuhakikisha inaweka mazingira yatakayomfanya mtoto apate haki zao mbalimbali, pia ni wajibu kwa jamii kufanikisha hilo sanjari na kuhakikisha mtoto anapata ulinzi wa kutosha.

Mathalani, mzazi na mlezi anawajibika moja kwa moja kumlea, kumtunza na kumlinda mtoto bila kujali mazingira yake kiuchumi na kijamii. Elimu bora ni miongoni mwa mahitaji muhimu ambayo mzazi anawajibika kumpa. Huu ndiyo urithi bora unaoamua hatma ya baadaye ya mtoto.