Ruvuma katika mikakati ya kufanana Zanzibar kiutalii

UTALII wa kiutamaduni haujapewa kipaumbele ikilinganishwa na nchi nyingine kama Afrika Kusini ambayo utalii huo umepiga hatua kubwa. Mkoa wa Ruvuma una utajiri mkubwa wa utalii wa utamaduni ikilinganishwa na utalii wa ikolojia.

Miongoni mwa vivutio vya utalii wa utamaduni ni Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yaliyopo katika eneo la Mahenge Manispaa ya Songea. Ofisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Challe anasema wadau wa utalii wamekusudia kuanzisha utalii wa kiutamaduni sanjari na kuboresha maeneo yote ya kihistoria ili kuendeleza utamaduni hatimaye maeneo hayo yaweze kuingiza mapato baada ya watalii kutembelea kama ilivyo katika visiwa vya Zanzibar.

Challe anasema, wadau kutoka wilaya zote za mkoa wa Ruvuma tayari wameshatembelea maeneo muhimu ya kihistoria. Maeneo hayo ni pamoja na makumbusho hayo ya taifa ya maji maji, Maposeni, Luhira na Chandamali katika wilaya ya Songea ili kutambua maeneo ya kihistoria na umuhimu wake kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Huu ni mwanzo wa jukumu la kuziboresha kumbukumbu za kihistoria katika mkoa wa Ruvuma na kuimarisha utalii wa ndani na nje, lengo likiwa ni kuutangaza mkoa wa Ruvuma kupitia sekta ya utalii wa kiutamaduni,’’ anasema Bartazar Nyamusya ambaye ni Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.

Nyamusya anasisitiza kuwa serikali imedhamiria kuyafanya makumbusho ya taifa ya mashujaa wa vita ya Majimaji kuwa ya kitaifa kutokana na makumbusho hayo kuhifadhi vifaa na silaha ambazo walizitumia mashujaa hao kupambana na wakoloni wa Kijerumani.

“Hii ni makumbusho pekee nchini ambayo imebahatika kuwa na vifaa vyote asilia na muhimu katika historia ya mtanzania hali ambayo inaitofautisha makumbusho hii na nyingine zilizopo hapa nchini, ” anasisitiza mhifadhi huyu.

Kwa upande wake, Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu anasema kuwa mji wa Songea ni miongoni mwa miji michache nchini ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita vya majimaji na kwamba katika makumbusho hayo kuna ushahidi unaoonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki kikamilifu katika vita hiyo. Anabainisha zaidi kuwa katika eneo la mashujaa wa majimaji yamejengwa majengo mbalimbali ambayo yamehifadhiwa vifaa vilivyotumiwa na mashujaa hao.

Ndani ya makumbusho ya taifa ya Majimaji kuna mnara wa kumbukumbu ya wanajeshi ambao walitoka Songea kwenda kupigana vita ya Idd Amini kati ya mwaka 1978 hadi 1979. Simulizi zinasema, wakati wanarudi baada ya kushinda vita hivyo walipata ajali mbaya na kufa askari wote 56 katika milima ya Lukumbulu wilayani Songea.

Ili kuwakumbuka mashujaa hao, serikali ilijenga mnara katika eneo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji ambako walizikwa mashujaa wa vita vya Majimaji kama sehemu ya kuwakumbuka.

Kulingana na Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997, pamoja na sheria ambayo inayatambua maeneo haya, serikali imeamua mji wa Songea uingizwe katika vivutio vya utalii wa kiutamaduni kwa ajili ya kuendeleza historia ya Mji wa Songea ili uwe wa kihistoria, kishujaa na kiutamaduni.

Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Dar es Salaam, Philipo Maligisu anasema, utafiti uliofanywa na umebaini kuwa mji wa Songea una vigezo vyote vya kuingizwa katika rasilimali za kiutamaduni za taifa kuhakikisha kuwa watalii wengi wa ndani na nje ya nchi wanafika katika makumbusho hayo kujifunza mambo mbalimbali ya historia ambayo ni urithi wa taifa letu.

Mwenyekiti wa Baraza la Makumbusho ya Majimaji, Said Mteso anasema kila mwaka baraza hilo hufanya kumbukizi la kuwaenzi na kuwakumbuka mashujaa hao wakiwemo mashujaa 68 ambao walinyongwa na kuzikwa katika kaburi moja. “Katika tukio la mashujaa hao kunyongwa walitimiza wajibu wao kwa ajili ya maslahi ya taifa letu la sasa na kizazi kijacho ambapo ushujaa ndiyo njia pekee ya kujikomboa na kulinda uhuru wa taifa letu’’, anasisitiza Mteso.

Mwenyekiti huyo kwa niaba ya Baraza la Makumbusho ya Majimaji, anaishukuru serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa uamuzi wa kumiliki makumbusho ya taifa ya Majimaji ili kurithisha mila, desturi na utamaduni kwa vijana wa sasa na vizazi vijavyo.

“Hali ya mila, utamaduni na desturi iliyopo kwa vijana wa sasa katika nchi yetu ni mbaya kwa kuwa vijana wengi wamesahau utamaduni mila na desturi za mtanzania na kuendekeza mila za kigeni ambazo zimeharibu kabisa maadili mema ya mtanzania,’’ anasema.

Mjumbe wa Bodi ya Utalii katika Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mbunge wa Nyasa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya anasema uhamasishaji wa kufufua utalii Kusini unaendelea kuhakikisha watu wa rika zote wanatembelea vivutio mbalimbali vya utalii ikiwamo makumbusho hayo ya majimaji.

Manyanya anaipongeza Idara ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji kwa kuandika barua kwa wakuu wa shule mbalimbali katika mkoa wa Ruvuma ili kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi ya kutembelea vivutio vya utalii.