Ifahamu taaluma ya Ukalimani

UKALIMANI kama taaluma unashika kasi sana siku hizi tofauti na ulivyokuwa hapo zamani. Ukalimani na uhusiano vinakwenda sambamba na kasi ya utandawazi. Kasi ya ukalimani katika karne hii ya 21 inatokana na kupanuka kwa uhusiano baina ya mtu na mtu, jamii na jamii, taifa na taifa, hivyo kuhitajika kuwa na mawasiliano kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kibiashara.

Sababu hii ya kiutandawazi inaifanya dunia kuwa kama kijiji, hivyo ukalimani unaonekana kuwa ni chombo cha kurahisisha mawasiliano hasa kwa jamii ambazo zinazungumza lugha tofauti, na hivyo pia kuwa kama ajira kwa watu wanaozungumza lugha za kimataifa.

Ukalimani ni mchakato wa kiakili unaohusu shughuli changamani ya kuzungumza na kusikiliza kwa wakati mmoja. Ukalimani ni tafsiri ya mdomo ya kile kinachosemwa kwa lugha nyingine ili wazungumzaji wa lugha tofauti waweze kuwasiliana.

Zipo aina mbalimbali za ukalimani lakini zilizo kuu ni mbili ambazo ni Ukalimani wa Papo kwa Hapo (UP) na Ukalimani Fuatizi (UF). Aina nyingine ni Ukalimani wa Mikutano, Ukalimani wa Kiungo, Ukalimani wa Mahakama, Ukalimani wa Vyombo vya Habari, Ukalimani wa Simu, Ukalimani wa Video na Ukalimani kulingana na muktadha. Lakini hapa tutaelezea kwa muhtasari aina kuu mbili.

Ukalimani wa papo kwa hapo (Simultaneous Interpretation) Ulifanyika kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Nurenberg, ambapo lugha kuu rasmi za kazi zilikuwa nne. Tangu wakati huo mahitaji ya ukalimani yamekuwa yakiongezeka kwa kiasi kikubwa.

Lugha hizo zilikuwa Kijerumani, Kiingereza, Kifaransa na Kirusi. Katika ukalimani wa papo kwa hapo mkalimani anapeleka ujumbe kwenda lugha lengwa kwa haraka sana iwezekanavyo kama anavyouchukua kutoka lugha chanzi, huku mzungumzaji wa lugha chanzi akiendelea kuzungumza.

Mkalimani hukaa kwenye kibanda kisichopitisha sauti akizungumza kupitia kwenye maikrofoni akiwa anamwona na kumsikiliza kwa makini kabisa mzungumzaji wa lugha chanzi kupitia kwenye vifaa vya kusikilizia (hedifoni). Ukalimani huu hutumiwa sana na wakalimani wa lugha za ishara.

Unahitaji umakinifu wa hali ya juu sana kwa kuwa mkalimani hufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kama vile: Kusikiliza na kuzungumza Kuchanganua muundo wa kile kinachozungumzwa ili kuweza kuwasilisha hoja ya mzungumzaji kwa usahihi na Kusikiliza ukalimani wake mwenyewe ili kuchunguza usahihi wake katika kutamka maneno na kutoa ujumbe ulio sahihi.

Kwa hiyo, kila baada ya dakika 30 mkalimani hubadilishana na mwenzake ili kuepukana na uchovu mwingi wa akili na mwili kwa kuwa mkalimani mmoja hawezi kufanya kazi peke yake. Ukalimani Fuatizi (Consecutive Interpretation) Katika Ukalimani Fuatizi (UF) mkalimani huzungumza baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kumaliza.

Hotuba inagawanywa sehemusehemu, na mkalimani anakaa au kusimama karibu na mzungumzaji wa lugha chanzi huku akichukua madondoo kwa kuandika wakati mzungumzaji akiendelea kuzungumza. Mzungumzaji anapoacha kuzungumza ndipo mkalimani anaelezea sehemu ya ujumbe kwenda lugha lengwa.

Ukalimani huu unahitaji mkalimani kuwa makini sana na mahiri katika mawasiliano. Aina nyingine za Ukalimani ni: Ukalimani wa Mahakamani: Hii ni aina ya ukalimani ambao hufanyika mahakamani, kwenye mabaraza ya kutolea hukumu na ambapo masuala ya kisheria yanajadiliwa, kwa mfano, kwenye mikutano ya uapishaji, au wakati wa kuchukua maelezo ya mtuhumiwa katika kituo cha polisi.

Ukalimani wa Mikutano: Aina hii ya ukalimani hufanyika katika mikutano. Mikutano ya aina hii huweza kujumuisha lugha nyingi. Mara nyingi ukalimani unaofanyika kwenye mikutano ni ukalimani wa papo kwa hapo, ambapo mkalimani hufanya ukalimani kutoka lugha ya kigeni kwenda lugha yake ya asili. Ukalimani wa Simu: Ukalimani wa aina hii humsaidia mkalimani kufanya ukalimani kwa simu.

Mara nyingi hufanyika katika mazingira ambayo watu wanaohitaji kuwasiliana tayari wamekwishakuzungumza kwa simu. Hii ni huduma ambayo inawaunganisha wakalimani kwa simu na watu wengine ambao wanataka kuwasiliana lakini hawazungumzi lugha moja. Ukalimani kwa simu huhawilisha lugha moja kwenda nyingine na kuwawezesha wasikilizaji na wazungumzaji kuelewana.

Mara nyingi aina hii ya ukalimani hutumia utaratibu wa Ukalimani Fuatizi; kwa maana kwamba mkalimani anasubiri hadi mzungumzaji amalize kuongea ndipo na yeye afanye ukalimani. Ukalimani wa Video: Ukalimani huu hufanyika katika mazingira ambayo mmojawapo wa watu wanaowasiliana ni ama hasikii au hawezi kuongea ( bubu). Katika mazingira haya ukalimani wa lugha huhitajika zaidi.

Hii ni huduma ya mawasiliano ya simu video ambayo hutumia vifaa kama vile kamera za mtandao kuonyesha lugha ya ishara au lugha zinazozungumzwa katika huduma ya ukalimani. Ukalimani wa Vyombo vya Habari: Ukalimani wa vyombo vya habari hufanyika kwa njia ya ukalimani wa papo kwa hapo. Hufanyika zaidi katika matangazo ya moja kwa moja ya televisheni au redio.

Ukalimani wa Kiungo: Ukalimani huu ni pale ambapo mkalimani humsaidia mtu au kikundi cha watu katika utalii, matembezi au katika mkutano. Ukalimani wa Lugha ya Alama: Huu ni ukalimani ambao hufanyika kati ya lugha ya alama na lugha ya mazungumzo. Aina hii humwezesha mzungumzaji kuongea na mkalimani akahawilisha mawazo hayo kwa njia ya alama.

Aidha, mtu asiyesikia huweza kufanya mawasiliano kwa njia ya alama na mkalimani akahawilisha maana kwa njia ya mazungumzo. Hapa ni muhimu pia tueleze tofauti baina ya Ukalimani na Tafsiri kwamba Ingawa zinatumika katika maana zisizo za kitaaluma kama mbadala, Ukalimani na Tafsiri si kitu kilekile.

Kukalimani ni kuchukua ujumbe kutoka lugha chanzi na kuuhawilisha kwenda lugha lengwa kwa mdomo (mf. Kiingereza kwenda Kiswahili) wakati Tafsiri ni kuhawilisha maana kutoka matini moja kwenda matini nyingine (iliyoandikwa au kurekodiwa), huku mfasiri akiwa na muda wa kutumia kamusi, faharasa n.k. ili kuweza kutoa matini sahihi, yaani kuchukua namna moja ya lugha na kuhawilisha maneno yaleyale kwenda namna nyingine.

Kunapokuwa na tatizo la mawasiliano baina ya watu wawili, ndipo mkalimani anapohitajika. Mkalimani hurahisisha kazi ya makundi mawili yenye mjadala baina yao ili kuweza kuwasiliana katika muda mwafaka. Tofauti nyingine ni kwamba mfasiri anaweza kutafsiri maneno 2000-3000 kwa siku, wakati mkalimani anakalimani maneno 150 kwa dakika.

MATATIZO NA CHANGAMOTO KATIKA UKALIMANI

Matatizo katika kazi ya Ukalimani ni mengi. Baadhi ni: Kukosa maandalizi ya kutosha: Wakati mwingine wakalimani hawapewi nakala za mkutano mapema ambazo humwezesha mkalimani kufahamu mada itakayozungumziwa ili kufanya kazi yake vizuri. Mzungumzaji kuongea kwa kasi Mzungumzaji huweza kuongea kwa kasi kubwa mpaka kufikia kuchanganya mambo muhimu, kusahau mada anayozungumzia na kusahau kuwa kuna mkalimani.

Kwa hiyo, mkalimani anashindwa kufuatana naye na anachoka haraka kiasi cha ubora wa kazi yake kushuka. Mkalimani kushindwa kumudu lugha Mkalimani anaweza kushindwa kumudu lugha, hususan lugha mojawapo miongoni mwa zile anazofanyia kazi, yaani lugha chanzi au lengwa.

Muda wa kazi kuwa mrefu: Muda wa kazi unapokuwa mrefu tofauti na kiwango kilichopangwa huweza kumsababishia mkalimani uchovu na hata wakati mwingine kuanza kuzungumza maneno tofauti na yale yanayozungumzwa. Upotoshaji wa maana: Mkalimani huweza kutoa ujumbe tofauti na ule wa lugha chanzi, yaani hupotosha maana ya ujumbe.

Wakati mwingine ni kutokana na matamshi na lafudhi mbaya kutoka kwa wakalimani wengine wanaochukua rilei (kusikiliza kutoka kwa wakalimani wa lugha nyingine na kukalimani).

Mazingira ya kazi: Hali ya hewa katika kibanda cha Ukalimani (joto, baridi, unyevu) huweza kusababisha mkalimani akashindwa kufanya kazi yake vizuri. Kushindwa kwa uongozi: Uongozi unaweza kushindwa kusimamia kazi zake ipasavyo, hivyo kumfanya mkalimani naye kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Baadhi ya mambo ambayo mara nyingi uongozi hushindwa kuyafanya ni: kutokuwapa wakalimani nyaraka za mikutano mapema ili wajiandae; malipo duni kwa wakalimani; kutokuwathamini wakalimani; kutokuandaa vifaa au kuandaa vifaa vya kazi visivyo na ubora; kupanga idadi ndogo ya wakalimani kwa kuhofia gharama kuwa kubwa nk. Vifaa vya kazi: Vifaa vya kazi vinaweza kuwa duni kama vile maikrofoni na hedifoni na kumfanya mkalimani kutokusikika au kutosikia vizuri.

Idadi ndogo ya wakalimani: Idadi ya wakalimani kwa baadhi ya lugha hasa Kiswahili, Kiarabu, Kireno n.k. ni ndogo. Wakati mwingine mkutano ambao unahitaji wakalimani 10, unahudumiwa na wakalimani wanne.

Katika hali hii ubora wa kazi hushuka kwa kuwa wale wachache huchoka sana na kushindwa kuwa makini katika kazi. Tatizo hili linasababishwa Na kutokuwa na vyuo vinavyofundisha taaluma hii ya Ukalimani, pamoja na kufundisha lugha kubwa mbalimbali zinazotumika kwenye mikutano mikubwa ya kimataifa, kama vile Kifaransa, Kireno, Kiarabu, Kispanyola, Kiingereza nk.

Kwa muhtasari makala haya yamezungumzia Maana ya Ukalimani, Aina za Ukalimani, Tofauti baina ya Ukalimani na Tafsiri, pamoja na Matatizo na Changamoto zinazojitokeza wakati wa kufanya kazi hii. Aidha baada ya kujadili haya yote, tuseme tu kwamba taaluma hii ni muhimu sana na kwamba katika nyakati hizi za Utandawazi jitihada zaidi zinahitajika ili kuweza kuinusuru isididimie kabisa.

Miongoni mwa Jitihada hizo ni: Kuingiza kozi za ukalimani kwenye mitaala ya shule za sekondari; kuwa na mafunzo ya wakalimani ya mara kwa mara ya kupigwa msasa; Wizara ya Elimu kuwa na mpango wa kufundisha lugha mbalimbali za kimataifa zinazotumika kwenye mikutano mikubwa ya kimataifa; na pia kuunda vyama vya wakalimani kwa ajili ya kushughulikia na kutetea haki na maslahi yao.