Diamond Platnumz: Alivyomwibua upya msanii Saida Karoli

JINA la Saida Karoli sio geni kwa wapenzi wa muziki hasa wanaopenda midundo ya asili. Mwanamama huyu alitamba zaidi katikati ya miaka ya 90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 hasa akisifiwa kwa sauti yake yenye kuvutia.

Ni kati ya wanamuziki wachache waliowahi kutamba kwa nyimbo zenye vionjo vya asili. Aliwavutia watu wengi kwa kuimba nyimbo kwa vionjo vya kabila la Kihaya na kufanya wanamuziki wengine kutumia lugha zao za asili.

Wimbo wa Maria Salome ndio ulimtoa zaidi Saida na kumfanya ajulikane hadi nje ya nchi. Wimbo huo ulitokea kupendwa kiasi cha kumfanya hata mwanamuziki nguli wa muziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul a.k.a Diamond Platnumz aamue kuurejea akiuboresha zaidi.

Saida katokea wapi? Saida alizaliwa Aprili 4, 1976 kijiji cha Rwongwe, Wilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera na kutokana na changamoto za kimaisha, alilazimika kuishia darasa la tano. Katika mahojiano na gazeti hili, Saida anasema, baba yake hakuona thamani ya kumsomesha zaidi na alifariki miaka michache iliyofuata akabakia na mama yake tu na wadogo zake.

Mwaka 1991 akiwa na umri wa miaka 15, Saida anasema alijikita kwenye shughuli za uimbaji wa muziki kijijini hapo. Anasema alikuwa akiimba huku akipiga ngoma na alichukuliwa kama msanii wa kawaida tu.

Anasema alikuwa akiimba zaidi kwenye harusi na shughuli nyingine za maana hapo kijijini. Hata hivyo, anasema kutokana na kuimba kwa umahiri mkubwa, aliwashangaza wengi kwa kuimba na kupiga ngoma kwa wakati mmoja.

Mwanamuziki huyo anasema, kuimba na kupiga ngoma haikuwa rahisi na hakikuwa kitendo cha kawaida kwa wakati huo kumuona msichana akiweza kuimba na kupiga ngoma kwa wakati mmoja na hivyo wengi walivutiwa naye.

Alipotimiza miaka 20, mwaka 1996 alimpoteza mama yake mzazi na kulazimika kuutumia muziki kama chanzo kikubwa cha mapato yake. Anasema katika kipindi hicho ndio aliuona muziki kwake kama chanzo kikubwa cha mapato ili kuendeleza familia yake na yeye.

Ni wakati huo, alibahatika kuwasiliana na FM Production, kampuni iliyokuwa ikisaka vipaji. “Nilichukuliwa na Muta wa Fm Studio ndipo nikaanza kuona mwanga kwenye kazi yangu ya muziki. Hata hivyo, mwanga huo ulikuwa sio mwanga halisi niliostahili kupata”, anasema.

Saida anasema alianza kurekodi nyimbo zake chini ya Meneja wake, Muta. Kati ya nyimbo hizo, zilizokuja kutamba ni Maria Salome, Kaisiki, Ndombolo na Mimi Nakupenda. Saida alivyotamba kwenye muziki Saida alikuja kuibuka kama mmoja wa magwiji wa muziki ambapo nyimbo zake zilikubalika zaidi Kagera hadi Dar es Salaam na nje ya nchi.

Katika mahojiano anasema aliendelea kusikika na kualikwa kwenye matamasha mbalimbali akisifiwa zaidi kwa uimbaji, uchezaji na upigaji ngoma. Alialikwa harusini na hafla nyingine. Septemba 2, 2001 alizindua albamu yake ya kwanza iliyohanikizwa na shangwe za kila aina.

Aliuteka umati wa mashabiki kwenye uzinduzi wake nchini na nje, Kampala, Uganda alikojaza watu kwenye uwanja wao mkubwa wa soka. Alivyokuja kupotea Baada ya kutamba kwa muda mrefu, Saida alikuja kupotea katika anga ya muziki kiajabu.

Hata hivyo, baadaye ilikuja kubainika kuwa, alitoweka kutokana na kushindwa kuelewana na viongozi waliokuwa wakimsimamia kimuziki. Anasema alitofautiana na viongozi wake katika malipo akidai alikuwa hapati kile alichostahili.

Anasema, kutokana na kupata malipo kiduchu, alikata tamaa ya kuimba na kuamua kuendelea na shughuli za kawaida akiwa hana mahala pa kukaa jijini Dar es Salaam na kuamua kurejea tena kijijini kwao Rwongwe, Bukoba Vijijini.

Anasema maisha kwake yalikuwa ni zaidi ya magumu kwa kuwa alikuwa akisutwa na nafsi yake kuwa alikuwa mtu maarufu ambae ameishia maisha ya chini kuliko hadhi yake. Anasema alisumbuliwa na ugumu wa maisha na kulazimika kuimba tena kwenye mazingira ya kijijini kwao akitumia usafiri wa kudandia malori, Fuso kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Saida hafichi ukweli kuwa, kutokana na maisha kuwa magumu, alinusurika kujiua mara mbili kwa msongo wa mawazo na maisha magumu yaliyokuwa yakimkabili kijijini kwao huko. Msanii huyo anasema kuna wakati alilazimika kurejea tena mjini lakini alikosa fedha za kuendelea kuishi kutokana na ukata mkubwa.

“Ilifikia wakati wa kujuta kwa kuwa maarufu kwa kuwa niliishia kudharauliwa na hata ile thamani tena ya umaarufu iliisha na nikawa kama mtu wa kawaida kabisa”, anasema. Anasema kushindwa kujua na kusoma kwa wakati ule kulinifanya nishindwe hata kuelewa nini kinachotakiwa kwenye mikataba na kuingia mkataba ambao umekuwa mwiba kwake.

Anasema hakupewa hata nusu ya fedha alizoshiriki kuzichangisha kwenye nyimbo zake na shoo zake kadhaa alizofanya miaka yote hii. Saida anasema, alipotoweka aliamua kwanza kujipanga ili kuhakikisha anarejea tena sokoni akiwa anajua kusoma na kuandika ili kujua namna ya kwenda sanjari na soko la muziki.

“Kwa sasa ninajua kusoma na kuandika na tena sio Kiswahili tu bali hata Kiingereza cha kusoma na kuandika yaani masuala ya Yes and No kwangu si ishu tena,” anasema akicheka.

Anauona mwanga upya tena Anasema tayari akiwa ameshajua kusoma na kuandika anakutana na mwanga tena kwenye muziki wake ambapo anachukuliwa na Meneja wake wa sasa, Jonas Albert ambaye anamtoa kijijini Rwongwe na kumleta tena mjini.

Anasema meneja huyo akiwa kwenye shughuli zake kijijini alimwona akiwa mwenye shida na kumleta mjini akampangishia nyumba ya kuishi na kumpeleka ofisi za Taasisi ya kukuza vipaji Tanzania, THT alikomwanzishia safari mpya.

Saida anasema, kwa sasa anauona mwanga kwa kuwa kwanza amepokewa vema kwenye fani ya muziki na msanii mahiri wa Bongo Fleva, Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambaye anaurudia wimbo wake wa Chambua kama Karanga uliomrejesha kwenye chati kwa nguvu.

Anasema kitendo cha Diamond kuuimba wimbo huo kimempatia uhai tena kwani amelipwa na kisha amerejeshewa heshima iliyokwishazikwa. “Hapo tu ndio nimeona thamani ya kazi yangu na uhai kurejea kwani licha ya kulipwa vizuri, hadhi na mwanya wa kutokea tena kisanii ndio uliamka na ndio nimerejea, “anasema Saida.

Anavyorejea kwenye fani Juni 9 mwaka huu Saida aliwaalika futari katika ofisi za THT, wasanii wa muziki mbalimbali, watangazaji wa radio na luninga na wadau wa muziki kuomba wampokee tena kwenye fani.

Anarejea akianza na uzinduzi wa video ya wimbo mpya ya O’Rugambo ambayo ni ya wimbo huo wenye vionjo vya muziki wa asili uliochanganywa na muziki wa Bongo Fleva. Anasema ameamua kutotumia zaidi muziki wa asili peke yake bali ameunganisha na vionjo vya Bongo Fleva ili kuleta thamani halisi ya muziki.

Anawaambia wadau hao: “Nimerejea ninaomba waandishi wa habari, wanamuziki wenzangu na wote wenye nia kuendeleza muziki kunipokea na tushikane mikono ili kazi iende juu zaidi”. Meneja wake, Albert anasema wimbo wa O’ Rugambo ndio wa kwanza kwa Saida kurejea kwenye chati na anatarajiwa kuachia nyingine.

Anasema katika wimbo huo, ameshirikisha vionjo vya msanii Darasa na Diamond ili kuwavuta karibu zaidi mashabiki wake. Anasema anamsimamia ikiwa ni mkakati wa kumuinua kw amer m k nilish kupan Nina walionire Sitowaang tufa tusa h