Giniki: Jina linaloinukia katika riadha

RIADHA ni moja ya michezo ambayo sasa imejipatia umaarufu baada ya wanariadha wa Tanzania kufanya vyema katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Miongoni mwa wanariadha wanaonekana kuja juu kwa kasi nchini sasa ni Emmanuel Gisamoda Giniki wa Klabu ya JKT Arusha.

Mwanariadha huyo anakimbia mbio fupi kuanzia mita 5,000 na ndefu, kilometa 21. Alianza riadha alipokuwa akisoma darasa la sita shule ya msingi Dumbeta kata ya Kateshi wilaya ya Hanang, Manyara.

Safari yake katika riadha Giniki akiwa chini ya Kocha Gidamis Shahanga alifuzu majaribio ya km 12 ya mbio za riadha yaliyofanyika Dumbate. Baada ya kushinda mbio hizo, ilimlazimu kuhama shule ili kuwa karibu na kocha kuendelea kujijenga zaidi katika riadha. Alimaliza elimu ya msingi shule ya msingi Jorodom ambako ndiko aliweza kujifunza kwa juhudi na kufikia kiwango alichonacho.

Baada ya shule ya msingi alisimama kukimbia riadha hadi alipomaliza elimu ya sekondari aliyokuwa akisoma katika shule ya Ganana, huko Kateshi mwaka 2011. Alianza tena kushiriki mbio na kuumia jambo lililofanya ashindwe kufanya vizuri katika mbio na kuacha hadi mwaka 2014 aliporejea rasmi katika tasnia ya riadha.

Mwaka 2014 alifanya vizuri katika mbio za nyika kuchagua timu ya taifa yaliyofanyika katika viwanja vya Magereza jijini Arusha. Baada ya hapo alikwenda kushiriki mashindano ya kitaifa ya kilometa 21 mkoani Kilimanjaro ambapo alishika nafasi ya pili na aliendelea kufanya vizuri mbio za ndani hadi alipofanikiwa kutoka nje.

Mashindano kimataifa aliyoshiriki Mwanariadha huyo aliendelea kufanya vizuri katika mashindano ya ndani ya riadha na kwa mara kwanza Mei 2015 alishiriki mbio ya nje ya nchi za km 21 za China ‘jinjiang inter half marathon’. Alishinda nafasi ya kwanza kwa kutumia dakika 62:36.

Mbio hizo zilishirikisha wachezaji kutoka mataifa tofauti ikiwemo Kenya, Ethiopia, Uganda na nyinginezo. Mwanariadha huyo anasema, baada ya kutoka huko, alirudi na kujiunga na timu ya taifa iliyoshiriki michezo ya Afrika inchini Congo Brazzaville Septemba 2015.

Katika michezo hiyo, Giniki alishika nafasi ya 11 na kurudi katika kambi yake iliyokuwa Kateshi mkoani Manyara. Novemba mwaka 2015 alipata mwaliko wa kurudi China ambapo alikimbia mashindano manne tofauti ya kilomita 21 na kushinda matatu na moja akashika nafasi ya tatu.

Anasema, baada ya mashindano hayo, alirejea nchini Desemba na kushiriki mashindano ya ndani na kushinda katika mashindano ya ‘Hapa kazi tu’ yaliyofanyika Dododma Januari 2016 .

Februari 2016 alirudi nchini China tena kushiriki mashindano matatu Februari na kushinda mashindano mawili akishika nafasi ya kwanza na ya pili akawa wa pili. Alirejea Machi akaitwa China kushiriki mbio za kimataifa za kilomita 21 na kushika nafasi ya tano.

Alishiriki mbio hizo tena na kushika nafasi ya pili tena kabla ya kuumia goti na kushindwa kukimbia tena. “Julai 2016 nilirudi China kwa matibabu ambako nilikaa mwezi mmoja hadi Agosti.

Septemba nilianza mazoezi baada ya kupona nikashiriki mbio, ” alisema Giniki. Alivyong’ara mbio za kimataifa Giniki alifanikiwa kuonesha uwezo mkubwa Aprili mwaka huu aliporejea na ushindi baada ya kushinda mbio tatu mfululizo katika mashindano ya China.

Mbio ya kwanza alikimbia Aprili 27 Shanghai half Marathoni’ akamaliza kwa muda wa dakika 1:01:36, Naijing Xianlin half marathon iliyofanyika Mei 7 akashinda baada ya kutumia muda wa saa 1:02:00. Mbio nyingine zilikuwa za Mei 16 za ‘Jurong half marathon’ alikofanikiwa kumaliza akitumia muda wa saa 1:04:00.

“Shukrani zangu kwa uongozi wa JKT bila kusahau vyama vya riadha kwa kuhakikisha tunafanya vizuri. Tunaomba waendelee kutusaidia ili tung’are zaidi,” alisema Giniki. Alitaka wanariadha watambue kila kitu kinawezekana kwa malengo na juhudi za pamoja kwani katika mbio za nje unakutana na wanariadha kutoka maeneo tofauti.

“Safari yangu ya riadha imenibadilishia maisha kwa kiasi kikubwa kwani imekuwa ni ajira kwangu,” alieleza Giniki. Alisema kikubwa katika riadha ni kujiamini , kujituma, nidhamu na kuzingatia mazoezi. Changamoto zake katika riadha Moja ya changamoto alizokutana nazo alipoanza riadha ambazo nusra zimfanye akate tamaa kuendelea ni majeraha.

“Nilivyoanza riadha nilikutana na vikwazo. Nilipata majeraha yaliyofanya nione siwezi kuendelea na mbio lakini nashukuru baada ya kumaliza elimu ya sekondari nikarejea tena katika riadha nikiwa na matumaini ya kufika mbali. Namshukuru Mungu,” alisema.

Kuelekea mbio za dunia Giniki alieleza Tanzania ina matumaini ya kufanya vyema kwani wanariadha wapo kambini wakiendelea na mazoezi kushiriki mbio za mita 5000 zitakazofanyika nchini Ubelgiji Julai 22 kutafuta nafasi ya kufuzu kushiriki mbio za dunia Agosti mwaka huu.

Mwanariadha huyu bado ana ndoto ya kuweka rekodi kwa muda wa historia na kujenga kituo cha kukuza mchezo huu kwa watoto wenye vipaji wafikie ndoto zao. Mafanikio katika riadha “Nashukuru JKT imechukua wachezaji na kuwafadhili, kuwalea na kuwanoa zaidi.

Hii ni sehemu ya mafanikio, ni taswira mpya kwa chipukizi kuongeza juhudi,” alisema. Alishukuru uongozi wa Riadha Tanzania , w a d a u na Serik a - li kwa j u h u d i za pamoja zinazofanywa k u i n u a mchezo wa riadha.