Sasa unaweza kufuga samaki chumbani

INGAWA leo maonesho ya Sabasaba yanafikia mwisho katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara Kilwa, Dar es Salaam, bado unaweza kutumia siku ya leo kwenda ili kujifunza namna unavyoweza kufuga samaki kwa njia za kisasa.

Kama ukishindwa kufika, basi utalazimika kuwasiliana na Jeshi la Kujenga Taifa, hususani Shirika lake la kuzalisha mali (Suma- JKT), Makao Makuu Mlalakua ili kujua njia hii ya kisasa na hasa kama utakuwa una uwezo wa kununua tekonolojia hii mpya na hivyo kuwa sababu ya kujipatia kitoweo na kipato kwa kuuza ziada.

Katika maonesho hayo yanayomalizika leo, kama kuna eneo kwenye banda la JKT limekuwa linafurika watu wengi, basi ni hilo la ufugaji wa kisasa wa samaki kwa kutumia matenki.

Mbali na bidhaa za fenicha, JKT pia wanaonesha namna ya kufuga kuku na bata mzinga. Wingi wa watu umekuwa unawafanywa maofisa wa jeshi hilo walio katika kitengo hicho cha samaki kujibu maswali lukuki ya wananchi wanaotaka kujua namna ya kufuga samaki kwa njia hiyo ya kisasa inayotumia matenki.

Mmoja wa maofisa hao, Luteni Joseph Lyakurwa, anasema kwa hapa nchini, hiyo ni teknolojia mpya ya ufugaji samaki ni itakuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wanaotaka kufuga, kwani sasa hata wapangaji au wanoishi kwenye maghorofa wanaweza kufuga samaki bila kuhitaji maeneo makubwa kwa ajili ya mabwawa.

Anasema kwa muda mrefu, matenki ya maji makubwa ya lita 1,000 na kuendelea yamekuwa yakitumiwa kwa ajili ya kutunzia maji lakini sasa yanaweza kutumika kwa ajili ya kufugia samaki.

Anasema ufugaji huo wa kutumia madumu hauhitaji watu wengi kwani hata mtu mmoja anaweza kufuga samaki na kuwahudumia hadi kuvuna kwa ajili ya chakula au biashara. Anasema kupitia ufugaji huo kunakuwa na matangi ya lita 1,000 manne, na kila tenki linakuwa na samaki 100.

“Kwa hiyo utaona kwamba kwa wakati mmunaweza kufuga samaki 400 na inapofika miezi minne, wanakuwa tayari kwa chakula kwani wanakua na uzito wa kati ya gramu 350 na 500 (nusu kilo),” anasema.

Anafafanua kwamba endapo utataka samaki wako wawe wakubwa zaidi hadi kufikia kilo moja au zaidi, hapo utalazimika kupunguza samaki, wabaki wachache, na hapo watapata nafasi ya hewa zaidi.

“Unaweza kuacha kwenye tenki moja kati ya samaki 30 hadi 45 kama utataka wawe wakubwa zaidi,” anasema. Anasema ufugaji huo unafaa zaidi kwa samaki wasiopendelea kuishi kwenye matope kama sato (tilapia) kuliko samaki kama kambale ambao wanepanda kuishi kwenye tope.

Kuhusu chakula cha samaki hao, Luteni Lyakurwa anasema wanapendekeza kutumia chakula kinachozalishwa hapa nchini ambacho kiko katika mitindo wa punje ndogondogo.

Anafafanua kwamba unaweza kuwapa samaki chakula kilicho katika mfumo wa unga lakini maji yatachafuka na ndio maana ni muhumu samaki wale chakula cha punje. Anasema wakati wakijiandaa kuanzua kuzalisha chakula cha samaki wao wenyewe, kwa sasa wanawaelekeza wateja wao kwa wazalishaji waaminifu wa chakula cha samaki.

“Kama una mradi mdogo tu huna haja ya kujifunza kuzalisha chakula wewe mwenyewe na tunakushauri ununue, lakini kama una mradi mkubwa sana, tutakufundisha namna ya kuzalisha chakula cha samaki,” anasema.

Anasema katika matenki yote manne, bila kujali ukubwa wao, samaki hula wastani wa robo kilo ya chakula kwa siku. Kuhusu vifaranga wa samaki anasema wanapatikana kwao kwa bei ya wastani wa Sh 100, kwa kifaranga.

Akizungumzia ufugaji huo, Lyakurwa anasema walifanya kwanza utafiti kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu wakiboresha utafiti uliokuwa umegunduliwa na watu wengine awali ili kuwezesha kuendana na mazingira ya Tanzania.

Anasema mbali na matangi makubwa manne, kunakuwa na mapipa mawili, moja kwa ajili ya kusafisha uchafu kwa maana ya taka ngumu zinazotokana na kinyesi cha samaki na lingine lenye vizibo maalumu kwa ajili ya kunasa hewa yenye sumu.

“Ukiona uchafu unazaidi kuna sehemu hapa ya kufungulia maji machafu kisha unarejesha maji mengine masafi kwa kiwango kile kile kinachotakiwa,” anasema.

Anafafanua kwamba maji yanayofaa zaidi ni ya kisima au ya mvua na kama ni ya bomba, yanaweza kuwa na dawa nyingi (chlorine) na hivyo unashauri kuyaacha kwa siku tatu yakiwa wazi na kisha kuyatumia kama kawaida.

Kingine kilicho katika mfumo huo wa ufugaji samaki kisasa maarufu kama recycling aquaculture ni mashine (mota) inayotumika kusambaza hewa kwenye maji na kuyafanya yawe yakizunguka kwenye matangi hayo hadi kwenye mapipa ya kunasia uchafu.

Mfumo huo pia una kifaa kiitwacho inventor na betri kwa ajili ya kutunzia umeme pale umeme wa Tanesco unapokatika. “Kama hakuna umeme kwa saa 12 samaki wanaweza kufa. Kwa hiyo hii inakuhakikishia kuwa umeme wa Tanesco unapokatika.

Lakini pia kama unatumia umemejua (sola) ni rahisi kuunga hapa na kuendelea na ufugaji. “Unajua samaki wanapokuwa ziwani, kwenye mabawa au baharini, kunakuwa na hewa ya kutosha.

Lakini kwenye matenki inabidi uaongezee hewa kupitia hii mashine,” anasema. Luteni Lyakurwa anafafanua kwamba ufugaji huo unatumia umeme kidogo na ni rafiki wa mazingira. “Kama una mashamba, uchafu wa samaki ni mbolea nzuri, tena isiyo na kemikali kwa ajili ya mimea,” anasema.

Akizungumzia faida nyingine ya kufuga samaki katika madumu anasema kuwa samaki wanakuwa salama zaidi kuliko kwenye mabwawa ambako wanaweza kuliwa na kenge au ndege wanaozamia samaki. Anasema gharama za kununua mfumo huo wa ufugaji wa samaki kwa sasa ni shilingi milioni tatu.

“Ukishanunua, tunakuja kwenye kwako tunakufungia kila kitu kwa gharama hizo. Wewe unaingia tu gharama nyingine ya kununua vifaranga,” anasema. Anasema endapo matangi hayo utaweka nje, wanashauri uyafunike kwa paa juu.

Shirika la uzalishaji mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) lilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya mashirika ya umma ya mwaka 1974 kupitia amri ya Rais ya mwaka 1982. Lengo la kuanzishwa kwake ni kuendesha miradi mikubwa ya uzalishaji mali kibiashara na hivyo kusaidia kupunguza matumizi ya serikali katika kuendesha shu ghuli za JKT.

Shirika limekuwa likianzisha bidhaa mbalimbali na kutoa huduma bora kwa jamii kama vile kilimo, ujenzi, ufugaji, uvuvi na uhandisi. Suma JKT pia inatoa huduma ya ulinzi na uuzaji na usamb