Veta inavyofungua fursa za ajira kwa vijana

JINA VETA (Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi) ni maarufu miongoni mwa Watanzania wengi kutokana na kuakisi ufundi stadi. Katika makala haya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk Bwire Ndazi, anaeleza nafasi ya mamlaka katika kufungua fursa za ajira kwa vijana nchini.

Ndazi anaeleza kuwa Veta ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 1 ya mwaka 1994 na kupewa dhamana ya kutoa, kuratibu, kudhibiti, kugharimia na kuendeleza elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Majukumu hayo yanatekelezwa kupitia vyuo vinavyomilikiwa na VETA na vile vinavyomilikiwa na taasisi na asasi binafsi ambavyo huhitajika kupata usajili, ithibati na kufuata miongozo mbalimbali inayotolewa na VETA.

Katika kutekeleza dhamana ya kuendeleza elimu na mafunzo ya ufundi stadi, kwa sasa VETA inamiliki vyuo 28 vya ufundi stadi katika mikoa mbalimbali nchini. Inacho chuo kimoja cha kutoa mafunzo ya ualimu wa ufundi stadi kilichoko mkoani Morogoro.

Katika kudhibiti utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi, Veta imesajili vyuo vya ufundi stadi 761 vikiwemo vinavyomilikiwa na serikali, watu binafsi, mashirika ya dini na yasiyo ya kiserikali. Vyuo hivi vinatoa mafunzo katika fani zaidi ya 80 zilivyogawanywa katika sekta za ajira 13.

Nazo ni ufundi mitambo, ufundi umeme, ufundi ujenzi, ufundi magari, huduma za biashara, mavazi na nguo. Mafunzo mengine ni yanayohusu usafirishaji na uchukuzi, uziduaji (utafutaji, uchimbaji na uchakataji madini), uchapaji, urembo, ususi na umaridadi, kilimo na usindikaji chakula, hoteli na utalii pamoja na sanaa.

Katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria na mipango mbalimbali ya Kitaifa, VETA imekuwa ikiongozwa na mipango mkakati ya miaka mitano. Kwa sasa VETA inatekeleza Mpango Mkakati wa nne wenye malengo muhimu ikiwamo kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Malengo mengine ni kuongeza uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa kwa wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi. Dk Ndazi anasema mahitaji ya kupata ujuzi kwa Watanzania, hususani vijana ni makubwa na yanazidi kuongezeka kila mara.

Katika kukabiliana na mahitaji haya, mamlaka imekuwa ikibuni mbinu mbalimbali za kupanua wigo wa mafunzo na kuhakikisha mafunzo yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira na maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Juhudi na mbinu hizo zimeelekezwa katika mipango ya muda mrefu na muda mfupi. Mipango ya muda mrefu ni pamoja na kujenga vyuo katika maeneo mbalimbali nchini; kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika ujenzi na uendeshaji wa vyuo vya ufundi stadi.

Mikakati ya muda mfupi ni pamoja na kutoa mafunzo kwa njia mbalimbali za kisasa ikiwemo njia ya mitandao ya simu na kompyuta; kuanzisha mfumo wa mafunzo kwa kushirikiana na kampuni.

Mingine ni kutoa mafunzo ya muda mfupi katika sekta isiyo rasmi pamoja na kufanya utambuzi na urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo. Kwa mujibu wa Dk Ndazi, ingawa ujenzi wa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi ni wa gharama kubwa na unaochukua muda mrefu kukamilika ikilinganishwa na kasi ya ongezeko la mahitaji ya ujuzi kila mwaka, Veta imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake.

“Tumeongeza vyuo vinavyomilikiwa na Veta kutoka vyuo 14 vilivyokuwepo mwaka 1995 hadi kufikia vyuo 29 mwaka huu. Ongezeko hilo la vyuo limesaidia kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi katika vyuo vya ufundi stadi nchini,” anasema na kufafanua idadi imetoka wanafunzi 3,070 mwaka 1995 hadi 196,091 mwaka 2016.

Veta inaendelea na taratibu za ujenzi wa vyuo vipya vya mikoa ya Njombe, Simiyu, Rukwa na Geita na vya wilaya za Namtumbo, Karagwe, Kilindi, Chunya, Korogwe, Ukerewe, Nyasa na Chato. Aidha usajili wa vyuo binafsi umeongezeka kutoka vyuo 330 mwaka 1995 hadi zaidi ya vyuo 761 kufikia Juni 2017.

Idadi ya wahitimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nayo imefikia zaidi ya 180,000 kwa mwaka. Veta kwa kushirikiana na wadau wengine, imeanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo yanayolenga sekta zinazoibukia na kukua kwa kasi nchini kama vile sekta za madini na gesi.

Kupitia mpango huo, zaidi ya wanafunzi 800 wamehitimu mafunzo maalumu ya ujuzi wa kuendesha mitambo, pamoja na stadi za uchimbaji na uchakataji madini katika vyuo vya Moshi, Mwanza na Shinyanga. Asilimia 99 kati yao wamepata ajira katika migodi na kampuni mbalimbali zinazojihusisha na madini.

Mafunzo hayo yametolewa kwa ushirikiano na Chemba ya Madini na Nishati (TCME) na kampuni za madini. “Tumekuwa tukitoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza uwezo wa vijana kuajirika, hususani kwa vijana wa mikoa ya Lindi na Mtwara,” anasema.

Katika awamu ya kwanza ya mradi, mwaka 2012 hadi 2015, vijana wapatao 477 walinufaika na mafunzo hayo yaliyotolewa katika fani za uchomeleaji na uungaji vyuma, useremala, ufundi bomba, umeme, utayarishaji wa chakula na ufundi magari.

“Baadhi yao walifanya na kufuzu mitihani ya kimataifa,” anasema Dk Ndazi. Anaeleza zaidi kwamba, baada ya mafanikio ya awamu ya kwanza, kampuni hizo zimefadhili tena awamu ya pili ya mafunzo kwa sh bilioni nne.

Vijana wapatao 550 wanatarajiwa kunufaika na kutambulika kimataifa huku kukiwa na ongezeko la fani za ujenzi wa majukwaa, upakaji rangi viwandani na uendeshaji wa mitambo mizito.

Veta imeona umuhimu pia wa kuhakikisha makundi maalumu katika jamii hayaachwi nyuma kwa kuendelea kudahili vijana wenye ulemavu, yatima na wengine waliokosa fursa ili kuwapa ujuzi wa kujikwamua kiuchumi na kujitegemea.

“Tunatambua kuwa, ufundi stadi unaweza kusaidia makundi maalumu katika jamii kama vile wenye ulemavu na walio katika kaya masikini kuweza kujikwamua kiuchumi. Kwa hivyo, tumekuwa tukitoa mafunzo maalum kwa makundi hayo katika vyuo vyetu na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,” anafafanua.

Miradi inayolenga makundi hayo ni pamoja na Mradi wa Kuwezesha Vijana Kiuchumi (YEE) kwa kushirikiana na mashirika, hususani Plan International katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Lindi na Mtwara. Vijana wapatao 2,830 wamehitimu mafunzo ya muda mfupi katika fani tisa.

Upo pia mradi wa Kuwafadhili Vijana kupata Mafunzo ya Ufundi Stadi, Ujasiriamali na Stadi za Maisha kwa kushirikiana na International Youth Foundation (IYF). Vijana 1,526 walipatiwa mafunzo katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Kigoma, Ruvuma, Mbeya na Mtwara kati ya mwaka 2012 na 2015.

Wakati huo huo, Veta imebaini pia umuhimu wa kuwainua mafundi wenye ujuzi katika mfumo usio rasmi. Hivyo, imeanzisha utaratibu wa kutambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo.

Mpango huu unalenga kuwainua mafundi (wanagenzi) ambao tupo nao katika maeneo yetu, wanafanya kazi nzuri za kiufundi lakini hawakupata ujuzi wao kupitia vyuo na taasisi zinginze za elimu.

Baada ya kuwafanyia tathmini ya ujuzi wao, mafundi hao huandaliwa mafunzo maalumu ya kuziba upungufu walio nao, hutahiniwa katika ujuzi husika na hatimaye hutunukiwa vyeti na kurasimishwa.

Mpango wa awali ambao ulifanywa kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) umefanikiwa kurasimisha wanagenzi 1,103 katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya, Mwanza, Arusha, Morogoro, Lindi na Arusha.

Veta inashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kupanua kazi ya kutathimini na urasimishaji ujuzi kwa mikoa yote nchini; hatua itakayowafikia vijana wasiopungua 5,000.

Namna nyingine ambayo VETA imeona kuwa ina fursa ya kusaidia kuwapatia ujuzi bora vijana na kuwasaidia kupata ajira kwa urahisi, ni kuendesha mafunzo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali vikiwemo viwanda.

Inaendesha mafunzo kwa kushirikiana na kampuni na viwanda 33 kupitia mafunzo yanayofanyika kwenye vyuo na maeneo ya kazi . Mpango huo unalenga kuhakikisha mwanafunzi anahitimu akiwa mahiri zaidi katika stadi husika huku akiwa na uelewa pamoja na uzoefu wa mazingira halisi ya sehemu ya kazi.

Vijana 48 wamehitimu katika mpango huu katika fani za ufundi magari, ufundi umeme na huduma za hoteli. Mamlaka inatambua kikwazo cha baadhi ya watu kushindwa kuhudhuria mafunzo ya ufundi stadi kutokana na ama mazingira yao ya kazi au kuwa mbali na vyuo vya ufundi stadi.

Kwa hivyo, imeamua kuanzisha mafunzo kwa njia ya mtandao wa simu ili kuwawezesha watu mbalimbali waweze kujifunza katika mazingira na muda unaofaa kwao. Kundi hili huhitajika kwenda chuoni kwa ajili ya mafunzo ya vitendo pekee baada ya kuwa wamefaulu mitihani ya nadharia.

Wanashirikiana na Airtel kutoa mafunzo ya ufundi stadi kupitia simu za mkononi. Vijana wanaweza kujisajili kwa njia ya mtandao na kuchagua fani wanazohitaji na kujisomea kwa nadharia. Baada ya kufaulu nadharia, hutakiwa kuhudhuria mafunzo kwa vitendo katika vyuo vilivyo karibu na maeneo walipo.

Mradi huu ambao bado upo kwenye majaribio tangu ulipozinduliwa mwaka jana, vijana wasipoungua 8,000 wamejisajili katika mfumo huo na 50 kati yao wamehitimu mafunzo na kutunikiwa vyeti.

Dk Ndazi anasisitiza kuwa serikali kupitia Veta, inaendelea na mpango wake wa kuongeza fursa za upatikanaji wa mafunzo ya ufundi stadi nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya utoaji wa mafunzo hayo kuhakikisha azma ya kuandaa nguvu kazi yenye weledi na ujuzi stahiki kuelekea uchumi unaotegemea viwanda, inatimia.

Anasema wakati Tanzania ikielekea kwenye uchumi wa viwanda, jamii inapaswa kutambua kuwa viwanda vinahitaji ujuzi na ujuzi unapatikana VETA