Viazi lishe; zao lenye faida maradufu

UTAPIAMLO unaelezwa kuwa ni upungufu wa viini lishe mwilini, na unaelezwa kuwa tatizo la kiafya linaloathiri watoto chini ya miaka mitano, wajawazito, wanaonyonyesha na hata wazee, kutokana na mahitaji ya lishe kuwa makubwa kulinganisha na makundi mengine.

Licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, mamilioni ya watoto na kina mama wanaendelea kupata matatizo yatokanayo na lishe duni ikiwemo uzito mdogo, udumavu, ukondefu, upungufu wa Vitamini A, upungufu wa madini joto na upungufu wa madini chuma, hali inayosababisha tatizo la upungufu wa damu (anemia).

Tatizo la udumavu linalotokana na lishe duni husababisha ukuaji duni kimwili na kiakili wa mtoto na pia hutajwa kuwa chanzo cha vifo vingi miongoni mwa watoto wadogo nchini. Udumavu huchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa umaskini katika jamii, kwani hupunguza nguvu kazi kutokana na mtoto mwenye udumavu kuugua mara kwa mara.

Katika kupambana na tatizo la lishe duni, Taasisi ya Bill and Melinda Gates chini ya mradi wa Usambazaji wa Haraka wa Mbegu Bora za Mazao ya Mizizi kwa wakulima wadogo, wamefadhili na kuandaa mwongozo wa namna ya kusambaza mazao hayo, yaani viazi vitamu na muhogo. Mwongozo huo unawawezesha walimu wa shule za msingi na watumishi katika ngazi ya jamii kutumia elimu ya lishe kupitia vyakula katika kutatua tatizo la utapiamlo.

Katika mwongozo huo chakula kilichopewa kipaumbele ni viazi vitamu na bidhaa zake. Halikadhalika hatua nzima imepata ushirikiano kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi ya Elimu. Taarifa zinaonesha kwamba viazi vitamu ni zao muhimu kwa chakula na biashara hapa nchini, likifuatiwa na muhogo.

Ni kwa mantiki hiyo, wakulima wa Tanzania wana fursa nzuri ya kuondokana na matatizo mbalimbali ya kiuchumi na kilishe kwa kujielekeza katika kilimo cha viazi lishe. Katika kipindi cha miaka 10, viazi lishe vimeanza kupata umaarufu nchini kwa kuwa vina vitamin A ambayo ni muhimu kwa afya humsaidia mtu kuona vizuri hasa kwa watoto na wajawazito.

Jitihada za kuingiza viazi lishe kutoka nchi mbalimbali nchini zilianza mwaka 2000 ambapo mbegu ilitolewa Marekani kisha kufanyiwa majaribio kabla ya kusambazwa kwa wakulima.

Mtafiti Mkuu wa Kituo cha Utafiti Mikocheni jijini Dar es Salaam (MARI), Dk Joseph Ndunguru anasema mwaka huo 2000 walianza mradi huo wa viazi lishe katika nchi za Uganda na Kenya, kwa kutumia vikundi vya wakulima na shule za msingi.

Anasema wakulima ambao walipokea mbegu hizo baada ya mafunzo walipata mafanikio makubwa. “Baada ya kuonekana mafanikio kwenye nchi za Uganda na Kenya ndipo jitihada hizo zilielekezwa hapa Tanzania,” anasema.

Dk Ndunguru anasema mwaka 2008 walikuwa na mradi wa viazi lishe hasa Kanda ya Ziwa na katika mradi huo wakulima walifundishwa umuhimu wa viazi lishe na jinsi ya kuvizalisha na kuvitunza.

Halikadhalika, anasema wakulima hao walifundishwa kuhifadhi mbegu (marando) hasa wakati wa kiangazi kwa kuyaweka kwenye mashimo ama maeneo oevu au chini ya migomba, katika maeneo yenye kivuli.

Anasema kilichofanywa na watafiti baada ya kuletwa kwa marando hayo ni kuangalia changamoto za magonjwa zilizoko Marekani kuja huku kwa kuwa hali ya hewa ni tofauti.

Lingine, waliloangalia anasema ni kuona kama yanastahimili magonjwa na ukame. “Tafiti hizi tulifanya kwa kushirikiana na vikundi vya wakulima. Ziko aina za mbegu za viazi ambazo zinafaa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa na zile zinazofanya vizuri, Pwani na Nyanda za Juu, Iringa na Ruvuma,” anasema.

Kwa maelezo ya Dk Ndunguru, vikundi ambavyo vimepata mbegu hizo na kuona mafanikio yake ni Kanda ya Ziwa ambako watu wengi wamepata mafanikio kwa kuzalisha tani tano hadi sita kwa ekari.

“Gunia moja la viazi vitamu la kilo 50 bei ya mwaka jana ilikuwa Sh 30,000. Hapo mkulima anaweza kupata magunia 198 kwa ekari akiwa ametunza shamba lake vizuri,” anasema Ndunguru.

Anasisitiza kuwa viazi lishe kwa kuwa vina vitamin A kwa wingi vina faida nyingi sana mwilini na katika kuinua uchumi wa mkulima. Kuhusu changamoto za kilimo katika zao hilo, Dk Ndunguru anasema kubwa ni magonjwa.

Anasema viazi vinaugua pia ugonjwa wa batobato kama ilivyo kwa mihogo na migomba na kwamba kuna wadudu waharibifu kama inzi weupe na vidukari wanasoumbua ukuaji wa viazi.

Hivyo anasema wanafanya utafiti kudhibiti hali hiyo. Changamoto nyingine anasema ni upatikanaji wa mbegu kwani ni viazi ambavyo vinalimwa kwa muda mfupi na kufuatiwa na kipindi kirefu cha jua na hivyo kuwapo tatizo la kutunza marando ili yasikauke na hasa kwa kuzingatia kwamba kilimo cha wakulima wengi wadogo ni cha kutegemea mvua.

Ufinyu wa bajeti za kuzalishia marando kwa ajili ya wakulima anasema ni changamoto nyingine kwani ni wengi wenye uhitaji wa mbegu kulinganisha na kiasi kinachopatikana. Mtaalamu huyo anashauri serikali ishirikiane na wadau mbalimbali, asasi zisizokuwa za serikali na mashirika ya dini kutatua