Tazara; alama isiyofutika mioyoni mwa Wachina

RAIS Xi Jinping wa China alipotembelea Tanzania mwaka 2013 alisema kuwa moyo uliooneshwa na nchi yake wakati wa ujenzi wa Reli ya TAZARA unapaswa kuendelezwa. Alichokuwa akimaanisha Rais huyo ni kuhusu kupanua ushirikiano wa kiuchumi baina ya China na Afrika kwa kuzingatia kila upande unufaike.

Wengi wanaweza kudhani kwamba labda ni kwa vile alikuwa Tanzania ndipo rais huyo akalazimika kuitaja Tazara na kwamba huko kwao ni kitu ambacho labda kilishasaulika, la hasha. Wachina wanaikumbuka Reli ya Tazara kama moja ya miradi yao mikubwa Afrika na ya kujivunia.

Wanaichukulia kama moja ya alama ya uhusiano wa kindugu baina ya nchi hiyo kubwa na bara hili. Hii ni reli iliyokuwa inahitajika sana wakati huo baina ya nchi za Tanzania na Zambia ili kupambana na kero za makaburu waliokuwa wakitawala Afrika Kusini, hususani katika kusafirisha mizigo ya Zambia ambayo haipakani na bahari.

Kilichotokea ni kwamba Wachina, chini ya mwasisi wa taifa lao, Mwenyekiti Mao Zedong, walikubali kuijenga katika kipindi ambacho uchumi wao ulikuwa bado mdogo sana kulinganisha na sasa na kuijenga kwa ufanisi mkubwa. Tazara inatajwa kama moja ya miradi yao mikubwa kwa wakati huo nje ya China.

Kwa sasa China ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani nyuma ya Marekani inayoongoza huku ikiwa imejizatiti sana katika viwanda na sekta ya ujenzi. Hivi karibuni wakati waandishi wa habari kutoka nchi 10 za Afrika walipokuwa nchini China kwa ajili ya semina maalumu iliyolenga kukuza uhusiano wa nchi hiyo na bara hili, jina Tazara lilikuwa linajirudia rudia pia.

Ingawa Wachina ndio pia walijenga Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kusaidia sana katika kubadilisha mandhari ya jiji hilo pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, lakini uwanja huo haukutajwa kama miradi mikubwa ambayo China imefanya Afrika kama reli ya Tazara.

Mwanadiplomasia na Balozi wa zamani wa China nchini Namibia, Ren Xiaoping ni miongoni mwa watoa mada walioitaja reli ya Tazara kama miradi muhimu ambayo China imefanya katika bara la Afrika.

Alitaja pia miradi ya karibuni ya nchi hiyo barani Afrika kuwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) iliyojengwa nchini Kenya na kuzinduliwa hivi karibuni. Miradi mingine ya China Afrika katika miaka ya karibuni ni pamoja na reli katika Pwani ya Nigeria yenye urefu wa kilometa 1,402 na pia ujenzi wa reli inayounganisha jiji la Lagos na Kano nchini humo yenye urefu wa kilometa 1124.

Mradi mwingine ni wa miundombinu na upanuzi wa miradi ya madini katika bonde la Mashamba na Dima nchini Congo (DRC), ujenzi wa mji wa kisasa (mini-city) nchini Afrika Kusini na kituo cha kuchakata mafuta ghafi Angola.

China pia imeshiriki mradi wa ujenzi wa reli yenye urefu wa kilometa 1,344 nchini Chad, ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mapenda Nkua nchini Msumbiji na ujenzi wa reli yenye urefu wa kilometa 726 nchini Sudan.

Balozi Ren, kama alivyomaanisha Rais Jinping, alisema kwamba China imedhamiria kushirikiana na Afrika katika ikijitahidi kuhakikisha kila upande unaneemeka na si kinyume chake. Kutokana na kauli ya Rais Jinping kuhusu Tazara alipokuwa Tanzania, aliyekuwa Makamu Mkuu wa Wahandisi wa Kichina wakati wa ujenzi wa Tazara, Komredi Lu Datong alikaririwa akisema: “Tulitiwa moyo sana na kuona tunathaminiwa kusikia maneno hayo kutoka kwa Rais wetu.”

Mhandisi huyo alisema hayo wakati akihojiwa Mei 27 na 28, 2013 na mahojiano hayo kuchapishwa na Idara ya Mipango ya Sera, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Watu wa China katika kitabu cha ‘Kumbukumbu ya Urafiki wa China na Afrika’ (A Monument to China-Africa Friendship).

Lu alifafanua kwamba maneno ya Jinping ya kuendelea na moyo uliooneshwa wakati wa ujenzi wa Tazara yana athari nyingi chanya. Mhandisi huyo akafafanua kwamba maana halisi ya maneno hayo ni ‘Kujitoa bila kutanguliza ubinafsi,’ jambo ambalo limekuwa ni sera ya China tangu zama za Mwenyekiti Mao hadi uongozi wa sasa.

China, sasa ikiwa imepiga hatua kubwa kiuchumi, iko tayari kuisaidia Afrika kujenga ‘Tazara nyingi’ tena kwa kiwango cha kisasa kama ilivyofanya kwa Kenya. Reli ya Tazara inajulikana pia kama reli ya Uhuru.

Waandishi 35 kutoka Afrika waliotembelea China, walishuhudia namna nchi hiyo ilivyopiga hatua kubwa katika eneo la miundombinu ambapo kuna barabara nyingi za kisasa na treni zinazomwezesha mtu kusafiri kama kutoka Dar es Salaam na Mwanza kwa saa zisizozidi sita.

Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, zinapaswa kuchangamkia utayari unaooneshwa na China katika kushirikiana kwenye nyanja ya maendeleo kama anavyosema Rais Jinping ikiwa ni pamoja na kuiboresha zaidi Tazara ambayo sasa ina miaka 41 tangu iasisiwe.

Utayari huo ulioneshwa na Rais Jinping pia wakati wa Jukwaa la Uchumi baina ya Afrika na China lililofanyika Afrika Kusini mwaka 2015 ambapo aliahidi kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya programu za maendeleo kwa Afrika kutegemea na uchaguzi wa nchi hizo.