Maendeleo ya lugha ya Kiswahili baada ya Uhuru

LUGHA ya Kiswahili huzungumzwa katika sehemu nyingi duniani. Katika eneo la Afrika Mashariki, lugha hii ina utajiri mkubwa wa msamiati, semi, methali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo nyingi zikiwemo za utamaduni wa Mswahili.

Kiswahili ni lugha inayotumika shuleni katika mawasiliano na kufundishia kwenye baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania. Vitabu vingi vya kiada na ziada vimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili, hivyo huwasaidia wakazi wa Afrika Mashariki kuendelea kujifunza na kujiongezea maarifa na msamiati wa Kiswahili katika maisha yao ya kila siku.

Maendeleo ya Kiswahili nchini Tanzania yanaweza kuangaliwa katika nyakati tofautitofauti na kwa kuangalia zaidi shughuli za kiuchumi, kisiasa na kijamii zilizokuwa zikifanyika kwa wakati huo. Katika makala haya tutaangalia maendeleo ya Kiswahili baada ya uhuru kwa kuzingatia mambo yaliyokuwa yakifanyika wakati huo. Baada ya uhuru, kuna hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza na kukuza Lugha ya Kiswahili.

Harakati hizo ni pamoja na kupendekezwa kuwa lugha rasmi. Kiswahili pia kilipendekezwa kuwa lugha ya taifa na kwa maana hiyo kilitumika katika shughuli zote za kiserikali na kitaifa, mfano katika elimu, hususani elimu ya msingi. Serikali kwa dhamira ya dhati ilianzisha Taasisi mbalimbali zitakazoshughulikia lugha ya Kiswahili. Baadhi ya Taasisi hizo ni Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), taasisi ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na 27, mwaka 1967, ili kusimamia maendeleo ya lugha ya Kiswahili.

Zaidi baraza likipewa majukumu yafuatayo: • Kuratibu na kusimamia Kiswahili nchini kote • Kushirikiana na vyombo vingine nchini ambavyo vinajihusisha na maendeleo ya Kiswahili na kuratibu shughuli zao • Kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika shughuli rasmi na za kawaida • Kushirikiana na mamlaka zinazohusika kuthibitisha tafsiri sanifu za istilahi • Kuchapisha jarida au toleo linalohusu lugha na fasihi ya Kiswahili

• Kushirikiana na mashirika ya kitaifa, asasi na watu binafsi, kufuatilia, kushauri na kusimamia shughuli zinazolenga kukuza Kiswahili • Kushirikiana na mashirika mengine ya kitaifa na kusimamia utafiti unaohusu Kiswahili • Kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, kuthibitisha (lugha) vitabu vya Kiswahili. Katika kutekeleza majukumu haya mazito Taasisi nyingine kama vile Tuki sasa (Tataki), Ukuta, Uwavita n.k. zilianzishwa kwa nyakati tofautitofauti kwa lengo la kutimiza majukumu ya kukiendeleza Kiswahili zikisaidiana na Bakita.

Baada ya kuundwa kwa vyombo hivi nchini Tanzania, Kiswahili kilienea kwa kasi kubwa kwa kuwa Serikali ilishaweka kichocheo. Pamoja na taasisi hizi pia kuna vyombo vingine mbalimbali ambavyo vimechangia maendeleo ya lugha ya Kiswahili.

Miongoni mwake ni hivi vifuatavyo: VYOMBO VYA HABARI Baada ya uhuru kupatikana vyombo vingi vya habari vilianzishwa. Vyombo hivi vilitumika kueneza Kiswahili kwa kasi kubwa, licha ya kuwepo kwa changamoto za kiuchumi viliweza kutumia lugha ya Kiswahili. Vyombo hivyo ni pamoja na redio ya Taifa wakati huo ikijulikana kama Redio Tanzania, Dar es Salaam (RTD), gazeti la chama (Uhuru), na majarida mbalimbali ambayo yaliandikwa kwa lugha ya Kiswahili.

Vyombo hivyo kwa pamoja vilikifanya Kiswahili kuenea kote ndani na nje ya nchi.

WAANDISHI WA VITABU

Waandishi wa vitabu ambao wamekuwa wakiandika kwa kuzingatia matukio yaliyojiri kwa wakati huo wamekuwa wahamasishaji wakuu wa matumizi ya lugha ya Kiswahili. Waandishi wa riwaya kama vile, Faraji Katalambula aliyeandika vitabu vya (Simu ya Kifo, Buriani), Ibrahimu Hussein (Mashetani), Edwin Semzaba (Ngoswe, Penzi Kitovu Cha Uzembe), Shaffi Adam Shaffi (Kuli) na G. Mhina (Mtu ni Utu), Shaaban Robert (Diwani ya Shaaban Robert, Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika), Mathias Mnyampala (Diwani ya Mnyampala) ni baadhi ya waandishi wa vitabu vya riwaya, tamthilia na ushairi waliochangia maendeleo ya Kiswahili nchini Tanzania kwa miaka ya sabini.

Miaka ya themanini uandishi wa riwaya pendwa, zikiandikwa na waandishi wakongwe kama vile Elvis Musiba (Kufa na Kupona, Hofu, Njama, Kikosi cha Kisasi) na Amiri Bawji-(Hadithi Za Kusisimua) ni miongoni mwa maandiko yaliyosaidia kutia hamasa katika usomaji hivyo kuendeleza na kuchochea matumizi ya Lugha ya Kiswahili fasaha na sanifu.

Kuibuka kwa waandishi wa vitabu mbalimbali vya Ukimw, ugonjwa ambao ulishamiri miaka hiyo ya themanini kuliibua pia waandishi wengi wakiandika maudhui yaliyohusiana na chanzo cha ugonjwa huo, dalili zake na madhara yake, baadhi ya vitabu hivyo ni Kilio Chetu kilichoandikwa na Taasisi ya Medical Aid Foundation.

Kitabu hiki ni moja ya maandiko yaliyokuwa yakitumika katika Shule za Sekondari kama kitabu cha marejeo ya fasihi. Tamthiliya nyingine ni Orodha iliyoandikwa na Steve Reynold mwaka 2006 ikiwa na maudhui yanayohusu ugonjwa wa UKIMWI na madhila yake.

KUANZISHWA KWA VYUO VIKUU VYA SHAHADA ZA KISWAHILI

Kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Shule ya Sanaa na Lugha pamoja na kuongezeka kwa vyuo vinavyofundisha Shahada ya Lugha ya Kiswahili nchini kama vile vyuo vikuu vya SAUT, Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, Chuo Kikuu cha Serikali Zanzibar (Suza), Tumaini na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni hatua madhubuti na ya makusudi ili kuongeza wasomi wenye taaluma ya Kiswahili, licha ya changamoto ya wanafunzi hao wa Kiswahili kukosa maandalizi ya sehemu sahihi za kufanyia kazi wanapomaliza shahada za lugha ya Kiswahili.

Kuongezeka kwa istilahi za lugha ya Kiswahili ni jambo linaloashiria kupanuka kwa matumizi ya Kiswahili. Kuwepo kwa istilahi hizi kumechochea uandishi wa machapisho ya istilahi mbalimbali za Kiswahili yaliyotolewa na Bakita kama vile Tafsiri Sanifu Na. 1-6. Hali kadhalika Bakita limetunga Kamusi Kuu ya Kiswahili ambayo imesheheni msamiati mbalimbali wa lugha ya Kiswahili ili kukidhi mahitaji na matumizi ya msamiati ambao unaibuka kila siku kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Itaendelea wiki ijayo