Sasa ni zamu yetu katika riadha

TIMU ya taifa ya riadha imerejea nchini na kupokewa kwa vifijo kwenye Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere baada ya kupata medali ya shaba katika marathoni katika mashindano ya dunia London, Uingereza.

Furaha iliyoje ilijaa kuanzia kwa viongozi wa Riadha Tanzania (RT), Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), wale wa Multichoice- Tanzania, maofisa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wanamichezo na wadau wengine wa mchezo huo waliofika kiwanjani hapo.

Baadhi ya watu wanaweza kujiuliza kwanini Watanzania walifurahia medali moja tu tena ya shaba kutoka kwa Alphonce Simbu licha ya kupeleka wanariadha wanane katika mashindano hayo?

SABABU YA FURAHA:

Kwa mara ya mwisho Tanzania ilitwaa medali katika mashindano ya dunia ya riadha mwaka 2005 yalipofanyikia Helsinki, Finland pale Christopher Isegwe alipotwaa medali ya fedha.

Hiyo ilikuwa medali ya kwanza na mwisho kwa Tanzania kuipata katika mashindano hayo makubwa kabisa ya mchezo huo duniani. Na siyo tu mashindano hayo, pia Tanzania katika miaka ya hivi karibuni imeshindwa kabisa hata kutwaa medali katika mashindano mbalimbali ikiwemo hata Michezo ya Jumuiya ya Madola, ambayo wanariadha wetu walikuwa wakitamba.

Pia furaha nyingine ilisababishwa na wanariadha wetu akiwemo Simbu kuonesha uzalendo mkubwa kwa kujitoa kwa moyo kushiriki mashindano hayo bila kuweka mbele maslahi binafsi. Wanariadha hao kila mmoja hakupewa zaidi ya pauni 60 kwa siku zote za mashindano hayo yaliyofanyika kuanzia Agosti 4 hadi 13 jijini London lakini hawakuwa na kinyongo na kulitetea taifa kwa moyo wote.

NCHI ZINGINE SHIRIKI

Ukilinganisha na nchi kibao, Tanzania ndiyo ilipeleka idadi ndogo ya wanariadha lakini ilirudi na medali wakati kuna nchi ambazo zilipeleka lundo la wachezaji, lakini ziliambulia patupu.

Mfano kama wenyeji Uingereza wenyewe walikuwa na wanariadha kibao lakini walijikuta hawana zaidi ya medali tatu licha ya uwingi wao na kutumia fedha nyingi katika maandalizi.

UTITIRI WA MARATHONI

Kuwepo kwa utitiri wa mbio za marathoni nchini huenda nao ukawa umechangia kuinua hamasa kwa wanariadha chipukizi kushiriki mbio hizo. Hata Simbu naye aliibuliwa kutoka katika mbio za `mchangani’ na hadi sasa amekuwa mkimbiaji mkubwa.

Hata hivyo, utitiri wa mbio hizo pamoja wakati fulani kuibua vipaji, lakini bado unaweza kuchangia kuua vipaji endapo atasimamiwa vizuri na ndiyo maana RT Septemba 2 imeitisha kikao kukutana na waandaaji wote ili kuweka mambo sawa.

Katibu wa Kamati ya Ufundi ya RT, Rehema Killo anasema kuwa wameamua kuitisha kikao hicho ili kuwekana sawa na kuwapa taratibu waandaaji hao ambao baadhi yao ni wababaishaji wakubwa.

Anasema kuwa baadhi yao wamekuwa wakibabaisha katika utoaji zawadi huku wengine wakiendesha mbio hizo bila kusajiliwa, bila kulipa ada RT, kutokuwa na usimamizi mzuri wakati wa mbio na mambo mengine kibao.

USHINDI WA SIMBU

Siri kubwa ya ushindi wa Simbu ni maandalizi ya muda mrefu, ari ya kushindana, udhamini kutoka Multichoice- Tanzania pamoja na kulamba ajira kutoka JKT. Mwanariadha huyo alikuwa na uhakika wa kupata mlo wake pamoja na familia yake baada ya DStv kumdhamini, ambapo kila mwezi walikuwa wakimuigizia katika akaunti kiasi cha Sh milioni 1.

Mashindano ya Dunia ndiyo makubwa zaidi katika riadha na yamekuwa yakishirikisha wanariadha nyota duniani kutoka mataifa yenye majina makubwa katika mchezo huo. Kikubwa ni ufinyu wa maandalizi na kutokuwa na uzalendo kwa nchi kwani baadhi ya wanariadha wamekuwa wakifanya vizuri katika mashindano ya mialiko na kuchemka katika mashindano mengine.

KUFANYA VIZURI NYUMA

Huko nyuma Tanzania ilikuwa ikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa kama akina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Zakaria Barie, Gidamis Shahanga, Peter Mwita, Mwinga Mwanjala, Nzael Kyomo na wengineo. Wanariadha kadhaa wa Tanzania wamewahi kushikilia ubingwa au rekodi za dunia katika mbio tofauti tofauti lakini kutokana na maandalizi kuwa mazuri miaka ya nyuma.

SASA NI ZAMU YETU

Kama wasemavyo DStv: Sasa ni Zamu Yetu. Hilo halina ubishi kwani wanariadha wote walioshiriki mashindano hayo ya dunia wamesisitiza kuwa sasa wana ari kubwa ya kufanya vizuri katika mashindano yoyote makubwa yajayo.

Inaelekea sasa ni zamu yetu kwani ushindi mbali na maandalizi ya uwanjani pia mwanariadha kama mwanariadha anatakiwa yeye mwenye awe na ari ya ushindi moyoni mwake na siyo kulazimishwa na fedha au kocha wake.