Katiba iliyosuswa ni zaidi ya yaliyotokea Kenya

BAADA ya Mahakama ya Juu ya Kenya kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Agosti 8 nchini humo, upinzani Tanzania umeonekana kuumia kwa sababu Rais Uhuru Kenyatta waliyempigia debe atalazimika kuthibitisha tena ukweli wa ushindi wake ndani ya siku 60.

Hata hivyo, wamepongeza katiba ya nchi hiyo kuruhusu uchaguzi wa urais kuweza kupingwa mahakamani. Hawakuishia hapo, bali pia wamepongeza hatua ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kutengua matokeo yaliyompa ushindi Uhuru, wakisema ni hatua inayoonesha mahakama hiyo kuwa huru.

Kwa mfano, David Kafulila, mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini kupitia chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi aliandika kwenye akaunti yake ya Facebook maneno haya: “Nilipenda Uhuru ashinde lakini nimependa zaidi ujasiri wa Mahakama ya Kenya. Tunataka mahakama zijisimamie kiasi hiki Afrika.

Ni fundisho kwa mahakama za Afrika na sehemu kubwa ya Afrika.” Watanzania wengi pia hususani wapinzani kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakikariri Ibara ya 74 (12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema kwamba baada ya mshindi wa urais kutangazwa hakuna ruhusa ya kupinga matokeo hayo mahakamani.

Lengo la kukariri kifungu hicho ni kutaka kuonesha kwamba ni wakati mwafaka sasa kwa Tanzania pia kuruhusu matokeo ya urais kuweza kupingwa mahakamani kama inavyofanyika kwa uchaguzi wa wabunge.

Wanaopongeza hatua ya mahakama kama alivyosema Kafulila wanasema kilichofanyika Kenya ni mfano wa kuigwa Afrika na dunia kwa ujumla na wengine wamefikia ‘kukufuru’ kwamba Wakenya hawafai hata kuwa sehemu ya Afrika! Hapa kuna mambo mawili; la Katiba ya Kenya kuruhusu uchaguzi kupingwa mahakamani na hatua ya mahakama kutengua matokeo.

Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa uchaguzi wa urais nchini Kenya kupingwa mahakamani lakini mara ya kwanza matokeo ya urais hayakutenguliwa na hakukuwa na maneno mengi kama sasa.

Ni muhimu pia kukumbusha kwamba suala la uchaguzi kupingwa mahakamani siyo Kenya pekee bali hata Uganda mara kadhaa uchaguzi wa urais umepingwa mahakamani kwani sheria za nchi hiyo pia zinaruhusu.

Hata katika uchaguzi wa nchi hiyo wa Februari mwaka jana, Waziri Mkuu wa zamani wa Uganda Amama Mbabazi alifungua shauri mahakamani akipinga ushindi wa Rais Yoweri Museveni.

Mbambazi aliyekuwa Waziri Mkuu chini ya Museveni kati ya mwaka 2011 na 2014, alikuwa mshindi wa tatu katika uchaguzi wa Rais huku akiwa na chini ya asilimia 2 ya kura zote.

Mshindi wa pili alikuwa Dk Kizza Besigye ambaye huko nyuma pia alishapinga ushindi wa Museveni mahakamani huku mahakama wakati fulani ikikubaliana na hoja zake lakini ikisema hata kiwango cha kura alizokuwa akilalamikia angepata zote bado isingeathiri matokeo.

Lakini swali la kujiuliza ni hili: Je, kama mahakama ikiona sababu zilizotolewa na wapingaji hazina nguvu kubatilisha uchaguzi hapo mahakama inakuwa haijafanya kazi yake na hivyo haiwezi kuwa mfano kwa Afrika na dunia? Kwani, ili kutengua matokeo si ni lazima kuwe na sababu au hoja za mahakama kujiridhisha kufanya hivyo?

Mahakama isiporidhika na hoja zinazotolewa ili kutengua uchaguzi maana yake ni kwamba hiyo mahakama si jasiri na wala haijisimamii? Hilo la uamuzi unaofikiwa na mahakama kuhusu kufuta au kutofuta matokeo si hoja inayoangaliwa na makala haya bali suala zima la katiba kuruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani.

Hili limeshaelezwa na wengi kwamba kile ambacho wapinzani wanakinyooshea kidole kwamba ni wakati mwafaka sasa kwa Tanzania pia kuwa na ruhusa ya kuweza kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani walikikataa wenyewe pale waliposusa mjadala wa Katiba Pendekezwa.

Kwamba kwa vile katiba hiyo ilikuwa na mengi mazuri, kuisusa kwa sababu ya mambo machache ambayo hawakukubaliana na hatua ya kuyaondoa kulisababisha hata yale mazuri yote kutotumika kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Katiba Pendekezwa katika Ibara 87 (1) inasema: Kwa kuzingatia masharti ya Ibara ndogo ya (2), endapo mtu yeyote aliyeshiriki kama mgombea katika nafasi ya madaraka ya Rais katika uchaguzi wa Rais hakuridhika na matokeo ya uchaguzi huo, anaweza kuwasilisha malalamiko katika mahakama ya juu kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyotangazwa na Tume Huru ya uchaguzi.

Katiba hiyo katika ibara zingine ilikuwa inaweka muda wa kuwasilisha malalamkiko na muda wa kusikiliza hadi kutolewa hukumu. Hilo limegusiwa na wasemaji wengi kuwajibu wapinzani lakini ukweli ni kwamba katiba iliyosuswa na Ukawa ilikuwa pia inajibu malalamiko mengi ya Watanzania ingawa mengine yasiyohitaji ‘msuli mkubwa wa sheria’ yamekuwa yakifanywa na Rais John Magufuli. Baadhi ya haya yangekuwa yanafanywa na marais wa nchi jirani, bila shaka wapinzani wangesema: “Hakika hili linapaswa kuwa fundisho kwa Afrika na dunia nzima!”

KUPAMBANA NA UFISADI

Kwa mfano, Katika mpya ilionesha dhamira ya kudhibiti ufisadi na ubadhirifu, jambo ambalo wananchi kila kona ya nchi walikuwa wanalilalamikia wakiwemo wapoinzani. Kumbukumbu zinaonesha kwamba wananchi walikuwa hawaridhishwi na jitihada za serikali katika kusimamia maadili katika utumishi wa umma kwani matendo ambayo yalikuwa yanaashiria mmomonyoko mkubwa wa maadili katika karibia ngazi zote za utumishi wa umma yalikuwa yamekita mizizi kila mkona.

Suala hilo Rais Magufuli amepambana nalo kwa mkono wake bila kusaidiwa na Katiba. Katiba mpya ilikuwa inaondoa sekretarieti ya utumishi wa umma na kuunda Tume ya Utumishi wa Umma iliyokuwa ina meno makali zaidi.

Katiba ilikuwa inasema kwamba wajumbe wa tume hiyo watateuliwa na rais baada ya kupendekezwa na kamati maalumu ya uteuzi. Kamati hiyo maalumu ya uteuzi ilikuwa na jukumu pia la kuteua wajumbe wa Tume huru ya uchaguzi. Kwamba wajumbe wa Tume huru ya Uchaguzi kutoteuliwa na Rais lilikuwa jambo lingine kwenye katiba iliyosuswa na ambalo wapinzani wamekuwa wakililalamikia.

Katiba Pendekezwa ikazidi kusema kwamba “majukumu ya kikatiba ya tume itakuwa ni kusimamia mienendo na maadili ya watumishi wa umma. Pia kuchunguza tabia na mienendo ya viongozi wa umma na kuchukua hatua pale panapostahili.”

Kwa mujibu wa katiba hiyo iliyosuswa, Mwenyekiti na makamu mwenyekiti wangeteuliwa na rais kutoka wajumbe ambao tayari wameteuliwa na kamati maalumu ya uteuzi. Ikasema kwamba Tume ya maadili ya viongozi wa umma kitakuwa chombo huru na hakitaingiliwa na mtu yeyote, ofisi yoyote, bunge, mahakama, wala serikali.

Kwa mujibu katiba hiyo, Tume ingekuwa na mwenyekiti mmoja, makamu mwenyekiti mmoja na wajumbe wasiopungua saba na kwamba mwenyekiti na makamu wake wangekaa katika uteuzi kwa kipindi cha miaka isiyozidi mitatu au chini yake kutegemea na barua zao za uteuzi.

HESHIMA KWA WANANCHI

Katiba pendekezwa pia ilikuwa imeweka vipengele vya kumfanya mtumishi wa Umma kumheshimu mwananchi jambo ambalo pia Rais Magufuli amelipigania kivyake vyake. Sura ya 4 ibara ya 28(1) (a) inasema kuwa mtumishi wa umma anao wajibu wa kutunza na kulinda heshima ya ofisi lakini pia anawajibika kuwaheshimu wananchi.

Hii ilikuwa ni hatua kubwa kuwa na ibara kama hii katika katiba kwani misingi ya kanuni za utawala bora huamini kuwa madaraka na utawala wote wa nchi hutoka kwa wananchi. Hii maana yake ni kuwa hata utumishi wa umma hutolewa na wananchi na huanzia kwa wananchi. Wananchi ndiyo hutoa ajira ya utumishi wa umma kwa mtumishi.

Hii huanzia pale wananchi wanapomteua mtumishi wa umma namba moja ambaye ni rais ambapo naye huwateua wengine wote kupitia utaratibu maalumu. Kwa msingi huu kumbe mtumishi wa umma kutomheshimu mwananchi yafaa liwe kosa kubwa kwa kuwa ni sawa na kutomheshimu bosi wake au mwajiri wake.

Hiki ndicho kilichokuwa kinamaanishwa na ibara hii. Lengo kubwa la ibara hii ni kuhuisha, kuyarudisha, kuyapa nguvu kikatiba maazimio ya Azimio la Arusha ambayo yalilenga kutoa maadili ya uongozi na utumishi wa umma kwa ujumla na kujenga heshima kwa wananchi wote bila kujali tofauti zao na nafasi zao katika jamii.

MAMBO YA WANANCHI

Katiba pendekezwa ilikuwa inanyanyua hadhi ya mwanamke ikiwa ni pamoja na kumwezesha mwanamke kuruhusiwa kuuza, kumiliki ardhi hata ya ukoo wa mwanamume. Sura ya 3 Ibara ya 23 (2)(d) ya rasimu ambayo isingesuswa na kupita ingekuwa katiba tunayotumia sasa ilikuwa inasema kuwa kila mwanamke atakuwa na haki ya kupata, kumiliki, kutumia, kuendeleza na kusimamia ardhi kwa masharti yaleyale kama ilivyo kwa mwanaume.

Ikumbukwe kwamba jambo lolote linapoingia katika katiba basi hutoa haki ya kushitaki au kushitakiwa kwa yule atakayekaidi kutekeleza. Hii ilikuwa na maana kwamba haki ya mwanamke kufungua mashtaka dhidi ya mtu binafsi, kundi la watu, taasisi, kampuni, idara, au kitengo chochote iko palepale iwapo hatapewa haki ya kumiliki ardhi sawasawa na ilivyo kwa mwanaume.

Katiba pia ilikuwa inamlinda mwajiriwa anayenyanyaswa na mwajiri. Kwa mfano, katika eneo hilo, Katiba hiyo iliyosuswa ilikuwa inamwezesha mwajiriwa kumfungulia mashtaka mwajiri kwa manyanyaso na siyo kuishia kwenye kampuni kwani kisheria kampuni ni mtu (legal person).

Kwa lugha nyngine Katiba Pendekezwa ilikuwa inaweka mazingira ya kuwashtaki wamiliki wa kampuni hata kama kosa limetendwa na kampuni kwa ajili ya usalama na kuepuka utapeli wa baadhi ya watu kuunda makampuni na kuyatumia kufanya uhalifu ili kukwepa kushtakiwa wao kama wao.

Hayo ni baadhi ya machache tu ambayo yalikuwa kwenye Katiba iliyokuwa inapendekezwa lakini ilisusiwa na upinzani na hata mchakato wake kuwa mgumu na pengine imechangia kutufanya mpaka sasa kuendelea kutumia katiba ya mwaka 1977.