Kumbukizi ya Nyerere vita ya Kagera yatia fora tamasha

Kama ulidhani Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere amesahaulika baada ya kifo chake mwaka 1999, basi umekosea.

Mawazo yake, vitendo vyake na dhamira zake bado zinaishi. Hayo yalijitokeza juzi kwenye tamasha la 36 la sanaa la kimatafa la Bagamoyo mjini hapa wakati kikundi cha maigizo cha Irene Sanga na produzya Mrisho Mpoto kilipofanya shoo.

Pamoja na usiku kuwa mwingi, saa tano, bado watazamaji wa igizo hilo maarufu kwa jina la Juliana lilionekana kusubiriwa kwa shauku na watazamaji wengi, wakubwa kwa watoto.

Hii ilitokana na kuwa igizo lililosheheni watu wenye vipaji vya uigizaji kama Oscar Nyerere anayesifika kwa kumwigiza Hayati Mwalimu Nyerere kwa sauti, vitendo, mavazi na hata mwonekano wa nywele zake zenye mvi nyeupe.

Zaidi linavutia kutokana na kuwa na msanii mwenye sauti na mbwembwe za kughani na kuimba kama Mrisho Mpoto halisi tofauti na zao zikiwa ni maumbile ya mwili na rangi. Lakini pia linavutia kutokana na kuwa na washiriki wenye haiba ya Rais wa zamani wa Uganda, Idd Amin Dada au Nduli nafasi ambayo imechezwa na mtu aliyeshiba vizuri na mrefu, mweusi kama Amin halisi huku kichekesho kikiwa cha Mkuu wa Majeshi wa zamani Tanzania, Jenerali David Musuguri kuwa dada mfupi, machachari na mkakamavu, Igizo hilo lilikuwa likirejerea historia ya vita ya Uganda ya mwaka 1978/79 ambapoTanzania ilimpiga Nduli hadi akakimbia uhamishoni huko Arabuni alikofia akiiacha nchi ikianza kipindi kigumu cha wananchi kufunga mikanda kwa miezi 18 iliyotangazwa na Rais Nyerere kukabili mtikisiko wa uchumi uliotokea.

Igizo linawaonyesha wananchi wa Kagera wakilalamikia kuvamiwa na wanajeshi wa Uganda kabla ya Mwalimu Nyerere kutangaza vita akisema sababu ya kumpiga Amin tulikuwa nayo, uwezo wa kumpiga tulikuwa nao na nia ya kumpiga tulikuwa nayo akiitaka Juuiya ya kimataifa ielewe Amin ndiye alituchokoza.

Igizo hilo liliwaacha watazamaji wakivunja mbavu kucheka pale Mkuu wa Majeshi, Jenerali Musuguri alipokuwa akiliweka sawa jeshi lake kumsikiliza Amii Jeshi Mkuu, Rais Nyerere ambapo mtangazaji alimtambulisha dada mfupi, mkamavu, mwenye kishindo ndiye Musuguri.

Kwa wanaomfahamu Musuguri halisi alivyo mtu wa miraba minne hawakuwa na namna zaidi ya kucheka na kufurahia ubunifu huo uliojaziwa na kishindo cha dada kuonesha ukakamavu uliostahili kuongoza kikosi kile.

Ni igizo lilolenga kuwakumbusha Watanzania kukabili matatizo ya kiuchumi kwa dhati pale yanapotokea matatizo badala ya kutafuta njia za mkato za kufanya biashara za magendo kama ambavyo baadhi waliamua kufanya magendo mpakani mwa Tanzania na Uganda, Mtukula.

Kabla ya igizo hilo, kundi la muziki wa asilia la Kunoga chini ya gwiji Saraganda lilitia fora kwa nyimbo sita likiacha watazamaji wakishangilia. Awali kulikuwa na kundi la Chivane band la Bagamoyo, JUNIOR sarakasi la Bagamoyo, mwera group, CD 4 na Revolution yaliyotamba huku Mrisho Mpoto na Malaika wakipanda pia na kusalimia kwa kughani na kuimba kidogo. Kwa hakika tamasha hili limesheheni uhondo.