Nyerere anavyokumbukwa kwa kuenzi Kiswahili

HAYATI Mwalimu Julius Nyerere ni miongoni mwa viongozi wanaokumbukwa kwa kuwa watetezi wa lugha na falsafa za Kiafrika, ambapo alifanya juhudi kubwa za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili katika kuwaunganisha Watanzania.

Mchango wake ulianza wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Hii inajidhihirisha kwa kuangalia jinsi alivyoamua kutumia lugha ya Kiswahili kama chombo muhimu cha mawasiliano ambacho kiliwaunganisha Watanganyika kudai uhuru.

Nyerere alitumia Kiswahili katika kampeni za kisiasa ambapo siasa na sera za chama cha Tanganyika African Unioni (Tanu) zilienezwa sehemu mbalimbali nchini kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Matumizi ya lugha hii ni sababu mojawapo ya Tanganyika kupata uhuru wake mapema na bila kumwaga damu ambapo wale waliokuwa hawaifahamu na waliokuwa hawajui kusoma walipata nafasi nzuri ya kujifunza na kuelewa hatua za kudai uhuru zinavyokwenda.

Baada ya uhuru, Mwalimu Nyerere akiwa Waziri Mkuu wa kwanza alitangaza Kiswahili kuwa lugha ya Taifa na kuagiza kitumike katika shughuli zote rasmi za umma. Kwa kuonesha msisitizo wa matumizi ya lugha hii, Nyerere alitoa hotuba ya kusherehekea Sikukuu ya Jamhuri tarehe 10, Desemba 1962, kwa lugha ya Kiswahili.

Hatua hiyo ilidhihirisha na kuonesha kwamba lugha hii kama lugha asili ambayo ilitumika ili kuondoa uwezekano wowote wa mafarakano yanayohusu mitafaruku ya kimatamshi. Aidha, Mwalimu Nyerere alihutubia hafla zote kwa lugha ya Kiswahili, hatua ambayo ilifanya kila mwananchi kuelewa mipango na mikakati ya serikali katika kuwaletea maendeleo yao.

Kuanzia wakati huo, Kiswahili kilianza kutumika katika shughuli na katika nyanja mbalimbali nchini kwa kuimarisha mahusiano ya makabila na kuifanya nchi kuwa kama kabila moja badala ya makabila zaidi ya 120 yaliyopo nchini.

Hatua ya pili iliyochukuliwa na Mwalimu Nyerere ilikuwa ni kupitisha Azimio la Arusha mwaka 1967, aliposema kuwa ni mfumo wa Ujamaa pekee ambao ungefikia lengo la uunganishaji wa Watanzania wote kwa maana ya kuwaondoa katika matabaka ya kiuchumi.

Matumizi ya Kiswahili yaliendelea kupanuka ambapo mnamo 1962, lugha hii ilianza kutumika rasmi bungeni na kwa upande wa elimu, Kiswahili kilianza kutumika kufundishia masomo yote katika shule za msingi nchini huku Kiingereza kikibaki kufundishwa kama somo.

Mwalimu Nyerere pia alianzisha mpango wa Elimu ya Watu Wazima ambapo watu wazima walifundishwa kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili, pia alianzisha maktaba za vijiji ambazo zilitumia vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili.

Aidha kampeni mbalimbali za kitaifa zilizotangazwa na viongozi na kutekelezwa na wananchi zilitumia kaulimbiu za Kiswahili. Mfano wa kampeni hizi ni ‘siasa ni kilimo’, ‘mtu ni afya’, ‘kilimo cha kufa kupona’ na ‘madaraka mikoani’.

Mwalimu Nyerere pia aliandika vitabu kwa lugha ya Kiswahili, baadhi ya vitabu hivyo ni ‘TANU na Raia’, ‘Elimu haina mwisho’ na ‘Tujisahihishe’. Pia alitafsiri kitabu cha ‘The Merchant of Venice’ cha William Shakespear kama ‘Mabepari wa Venis’ kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili.

Juhudi za Mwalimu Nyerere katika kukiendeleza Kiswahili zilikwenda mbali kwa kutoa idhini ya kuanzishwa kwa asasi mbalimbali za kushughulikia maendeleo ya Kiswahili nchini. Baadhi ya asasi hizo ni pamoja na TUKI, BAKITA na UKUTA.

Kwa sasa lugha ya Kiswahili imezidi kuenea sehemu mbalimbali duniani na kuongeza idadi ya watumiaji. Juhudi za kuendeleza lugha hii nchini ziliwekewa msukumo na marais waliofuata baada ya Mwalimu kwa kusisitiza kwa vitendo matumizi yake.

Tumeshuhudia awamu zilizopita na iliyopo madarakani jinsi ambavyo wanatumia lugha ya Kiswahili katika kuhutubia ndani na nje ya nchi na shughuli zote za kiserikali. Lugha ya Kiswahili kwa sasa inatumika katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na pembe ya Afrika.

Baadhi ya nchi zinazotumia lugha hiyo ni pamoja na Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Malawi. Nyingine ni Msumbiji, Zambia, Visiwa vya Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kinatumiwa na watu wanaokadiriwa kuwa zaidi milioni 150.

Mafanikio ya Kiswahili nchini yametokana na juhudi kubwa za Mwalimu Nyerere ambaye mpaka leo anakumbukwa kwa kuienzi. Katika kuunga mkono jitihada zake, watanzania tunapaswa kujivunia juhudi hizi na kuwa mstari wa mbele katika kukiendeleza na kukitumia Kiswahili kama utambulisho wetu ili kueneza utamaduni wan chi yetu.

Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazozungumzwa sana katika nchi nyingi sio tu barani Afrika bali hata katika nchi za mashariki ya mbali na Ulaya, na kwa mujibu wa tafiti zinazojishughulisha na maendeleo ya lugha ya Kiswahili barani Afrika ni lugha ya pili inayotumiwa na watu wengi ikitanguliwa na Kiarabu