Athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyoongeza umasikini Chamwino

NI kipindi ambacho kaya zingekuwa zimevuna mazao mengi shambani na zingepata ziada ya chakula ambayo ingeuzwa na kuwa na kipato cha kukidhi mahitaji mengine muhimu. Hivi ndivyo ilivyokuwa imezoeleka katika kipindi cha mavuno kati ya Mei na Julai.

Lakini sasa hali ni tofauti. Njaa na ukata umeshika kasi. Ukame na mvua zisizotabirika zimesababisha upungufu wa uzalishaji mazao shambani. Hali hii imezikumba kaya katika vijiji vya Buigiri, Chinangali II, Mwegamile na Chamwino katika Tarafa ya Chilonwa, wilayani Chamwino, Dodoma. Hivi ni sehemu ya vijiji 107 vilivyoko katika wilaya ya Chamwino.

Wilaya hii ipo kilometa 40 kutoka katikati ya mji wa Dodoma ambao ni makao makuu ya nchi. Wakazi wa vijiji hivi vilivyo jirani na ikulu, wanalia njaa na kuwa tegemezi kwa chakula cha msaada. Mabadiliko ya tabianchi ambayo ni mtiririko wa mfumo wa hali ya hewa, yamechangia ukame na mvua zisizotabirika na kugeuka kichocheo cha umasikini kwa wakazi hawa.

“Tumeambulia mabua matupu,” anasema Emily Oriyo, mkazi wa Chinangali akielezea jinsi ambavyo uzalishaji umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka kutokana na ukame. Wakati msimu mmoja wa mvua ambazo huanza Novemba na kuishia Aprili, ulikuwa ukitumiwa na wakulima kuzalisha chakula na kutosheleza mahitaji, hivi sasa mvua hazina kanuni.

Katika msimu huo mmoja, wakulima waliutumia kupanda mazao mbalimbali na kuvuna, lakini Oriyo anaeleza namna ambavyo katika misimu mitatu iliyopita, mvua imekuwa ikinyesha bila utaratibu huku kipindi cha ukame kikiwa kirefu zaidi.

Oriyo anasema msimu wa mwaka 2016/17 umekuwa mbaya zaidi ya misimu iliyopita. Mkulima huyu ambaye sasa anafanya vibarua, hususani kuponda kokoto na kupata ujira wa Sh 1,000 kwa debe kutokana na kukosa chakula na fedha, anasema mvua ya kwanza iliponyesha, Desemba 2016, alipanda uwele katika ekari moja akitarajia kuvuna magunia 15. Lakini mkulima huyu ameambulia debe tatu za uwele na alizeti, amepata debe moja na nusu kutoka kwenye ekari moja.

Mkewe, Jane anakata kuni na kuuza mzigo kwa Sh 1,000. Familia hii ni sehemu ya wakulima na wafugaji wa viji hivyo vya Chamwino, Chinangali II, Buigiri na Mwegamile wanaolia na ukame na mvua zisizotabirika zilizochangia kutozalisha na kusababisha njaa na ukata; hivyo kuongeza umasikini. Mkazi wa Kijiji cha Buigiri, Olivia Chinyemba mwenye umri wa miaka 59 anaeleza jinsi ambavyo katika miaka ya 1990 alivuna kuanzia magunia matano ya mahindi na manane ya mtama kutoka kwenye ekari moja.

Lakini mwaka juzi (2015) alivuna magunia matatu ya mtama; Mwaka jana alipata magunia mawili na mwaka huu amepata gunia moja la mtama katika shamba lenye ekari moja huku mahindi akiwa amepata debe moja. Kwa upande wake, Peter Mkasanga wa kijiji cha Buigiri, ambaye ni mfugaji, anapolinganisha mwaka 1987 hadi 1990 na kipindi baada ya hapo, anasema tatizo si kwenye chakula tu, bali pia malisho ya mifugo.

Baadhi ya wafugaji, wameuza mifugo kutokana na uhaba wa malisho. Wakati huo huo ukosefu wa chakula na fedha, umewasukuma pia kuuza ng’ombe. Kwa mfano, Mika Tozili wa kijiji cha Chamwino alikuwa na ng’ombe 10 lakini mwaka huu amebakiwa na wanne. Wakilinganisha gharama za kilimo na mavuno, wakulima wanaotumia wanyama kazi wanasema wamejikuta katika hasara. “Ekari moja tunalima kwa Sh 30,000, palizi gharama yake ni Sh 15,000 hadi Sh 20,000.

Sasa ekari moja unavuna debe moja la mtama na mahindi debe moja. Unategemea umasikini utapungua?” anahoji Japhet Mdachi, mkazi wa Buigiri. Debe la mahindi ambalo miaka miwili iliyopita liliuzwa kati ya Sh 3,000 na 5,000 wakati wa kipindi cha mavuno, sasa linauzwa kati ya Sh 10,000 na Sh 13,000. Hii ni bei iliyowekwa kwa chakula cha msaada kilichopelekwa katika vijiji hivyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwegamile, Jeremiah Mpanduka anaelezea kuwa, Mei 2017, kaya zote 404 kijijini hapo, ziliidhinishwa kupata debe la mahindi hayo ya msaada lakini baadhi ya familia, zilishindwa kumudu kununua debe. “Si kaya zote zilimudu kununua mahindi hayo. Ilibidi serikali ya kijiji iruhusu wanaoweza kununua kidogokidogo. Ndipo watu wakawa wananunua kilo moja moja kadri wanavyopata fedha,” anasema.

Kila kaya ilipewa kibali cha kununua debe moja kwa Sh 15,000. Bei hiyo ilikwenda hadi Juni walipojitokeza wafanyabiashara wengi walioanza kupeleka mahindi kijijini hapo ndipo Agosti bei ilishuka hadi Sh 10,000. Kulingana na maelezo ya wanakijiji kutoka kaya zinazotegemea kilimo, wamekuwa wakipata mlo mmoja. Thomas Madimilo, mkazi wa Buigiri anaeleza: “Kila nyumba ina njaa...

Ukipata chakula sasa hivi (saa 6 mchana), utegemee tena kula kesho yake.” Kulingana na tathimini ya halmashauri, wilaya imetekeleza malengo ya kilimo ya mwaka 2016/17 kwa asilimia 65 kutokana na mvua kunyesha katika mtawanyiko usioridhisha hasa kipindi cha Januari hadi Machi, 2017. Jumla ya hekta 83,208 za mazao ya chakula zililimwa na kuzalisha tani 82,569 za chakula wakati mahitaji halisi ya wilaya kwa mwaka ni tani 87,518.

Hivyo wilaya inakabiliwa na upungufu wa uzalishaji wa tani 4,949 za mazao ya chakula katika msimu wa 2017/18. Wakielezea hali ya uzalishaji katika kilimo, wakulima 35 kati ya 40 niliozungumza nao, wanasema hawajawahi kutembelewa na maofisa kilimo zaidi ya kupokea ushauri kupitia mikutano ya hadhara ya kijiji. Hata hivyo, Newston Goi wa kijiji cha Buigiri anawatetea maofisa kilimo akisema, kuwa ukame na mvua zisizotabirika ziko nje ya uwezo wao.

Anatoa mfano kuwa yeye katika msimu wa 2016/17, alilima kwa kutumia wanyama kazi, akapanda mbegu za muda mfupi na mbolea ya samadi. Lakini bado hakuvuna kutokana na jua kali lililokausha mazao. “Hata maofisa kilimo wakitutembelea na kutushauri, kama hakuna maji, hatuwezi kupata mazao…

Sisi hatuwezi kutabiri kuwa mwezi huu tupande au tusipande,” anasema Goi. Ofisa Mifugo wa Kata ya Buigiri, Stephano Adeline anakiri kuwa si rahisi kumfikia kila mkulima na kumpa maelekezo ya kitaalamu. Kwa mujibu wa ofisa mifugo huyu, Kata ya Buigiri ina kaya 4,032 ambazo kati yao, wakulima ni 3,084 na wafugaji ni 948.

Anasema wamekuwa wakitumia mikutano ya hadhara kuwaelekeza wakulima mbinu mbalimbali ikiwamo, kupanda mbegu za muda mfupi, kutumia mbolea na kulima mtama na uwele badala ya mahindi. Kuhusu vitendea kazi hususani vyombo vya usafiri kwa maofisa ugani, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Chamwino, Athumani Masasi anasema mwaka wa fedha uliopita, wilaya ilinunua pikipiki 28 kwa ajili ya maofisa ugani wa kilimo na mifugo wa kata 28 kati ya kata 36 zilizopo.

“Hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa kata na vijiji wilaya inaendelea kutenga bajeti ili kila afisa ugani wa kata awe na pikipiki,” anasema mkurugenzi. Kwa mujibu wa sheria ndogo za kilimo za halmashauri, majukumu ya maofisa ugani ni pamoja na kutoa programu ya kilimo ya mwaka kulingana na hali ya hewa.

Programu itazingatia aina ya mazao kwa msimu, aina ya mbegu, namna na wakati wa kupanda, namna na wakati gani wa kuvuna na kuhifadhi mazao baada ya kuvunwa. Ataweza wakati wowote wa saa za kazi kuingia kwenye eneo la kilimo kwa madhumuni ya kusimamia utekelezaji. Atatakiwa kuwa na daftari linaloonesha idadi kamili ya wakazi na idadi ya ekari za mazao ya kilimo.

Atapanga ratiba ya kutembelea mashamba ya wakazi ili kujionea kama wanatekeleza wajibu wa kulima na kutunza mashamba. Hali kadhalika, kulingana na mwongozo wa kitaifa wa Kilimo Kinachohimili Mabadiliko ya Tabianchi uliozinduliwa Mei mwaka huu, maofisa kilimo wa vijiji na kata wanaelekezwa kuhamasisha na kufundisha wakulima kutumia mbinu za kilimo zinazohimili mabadiliko ya tabianchi.

Maofisa mipango na maofisa ugani wanaelekezwa kupanga na kuandaa bajeti kwa ajili ya maendeleo ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii wanazozitumikia. Ofisa Mtendaji wa Kata ya Buigiri, Boniphace Chikoti anasema katika ngazi ya kata, wamekuwa wakiibua mambo wanayotaka yatekelezwe na halmashauri ikiwemo maombi ya kuchimbiwa visima na malambo na kuyapeleka kwenye halmashauri ya wilaya.

Hata hivyo, Ofisa Mipango, Paschal Masatu anasema wao pia huangalia vipaumbele kwa kuzingatia bajeti iliyopo. Lakini Ofisa Kilimo wa Wilaya, Godfrey Mnyamale anafafanua kwamba, uwepo wa mipango si tatizo bali tatizo ni utekelezaji ambao hutegemea upatikanaji fedha.

Anatoa mfano wa mwaka 2015/16-2016/17 kuwa fedha za maendeleo hazikupatikana kama walivyohitaji jambo ambalo liliathiri utekelezaji wa mipango iliyopitishwa na halmashauri katika vikao halali.

Mnyamale hakueleza kiasi cha fedha walichopokea na shughuli ambazo ziliathirika kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha. Mkurugenzi wa Halmashauri, Masasi anasema halmashauri ingetamani miradi ya umwagiliaji iwe hata katika kila kijiji lakini ukosefu wa fedha za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji hasa mabwawa, visima na nishati ya kusukuma maji ndiyo sababu kubwa ya kutosambaza au /kujenga skimu kila kijiji.

Kwa mfano, skimu ya Buigiri ina eneo linalofaa kwa umwagiliaji lenye hekta 9,191, lakini zinazotumika kwa umwagiliaji ni hekta 1,656. Akielezea hatua zinazofanyika kuhakikisha fedha zinapatikana na kunakuwapo na skimu za umwagiliaji vijijini, mkurugenzi anasema wilaya inashirikisha sekta binafsi na serikali (PPP) katika ujenzi wa skimu kama ya Chinangali II ambayo imekamilika kwa ushirikiano wa serikali, wakulima na benki ya CRDB Wilaya imeshirikisha mashirika ya kimataifa kwa kuandika andiko lililowezesha kupatikana fedha za ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika vijiji vya Fufu (ekari 100), Suli (ekari 100), Chiboli (ekari 100) na Mvumi Makulu (ekari 140).

Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia nchi na mazingira, Sixbert Mwanga kutoka shirika la Climate Action Network (CAN - Tanzania) anafafanua namna ambavyo inaweza kuwa vigumu kwa mkulima kuhimili mvua zisizotabirika bila mbinu za upatikanaji maji.

Mwanga ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa CAN-Tanzania anasema, hata wakulima wakipanda mbegu za muda mfupi kama vile mtama na uwele, endapo zitakosa maji katika kipindi sahihi, hawawezi kupata mavuno.

Mwanga ambaye anasisitiza wakulima kupewa mbinu mbalimbali ikiwamo za uhifadhi wa maji na udongo, anasema kuna hali ijulikanayo ‘dry spell’ (kipindi kirefu cha ukame) inaweza kufanya mkulima asivune.

Anasema mvua ya kwanza ikinyesha na mkulima akaanza kupanda, inatakiwa ndani ya siku 30 tangu mbegu ipandewe, isitokee ukame kwa siku 10 mfululizo. “Ikitokea, basi ujue kuwa mkulima hawezi kuvuna,” anasema Mwanga huku akisisitiza wataalamu wa kilimo kuwa karibu na wakulima kwa lengo la kuwaelekeza mbinu mbalimbali za kuhifadhi maji ardhini.

Wakulima wa Chamwino ni sehemu ya asilimia 78 ya Watanzania walioajiriwa katika sekta ya kilimo inayochangia zaidi ya asilimia 95 ya mahitaji nchini. Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 inasema ifikapo mwaka 2025, maisha ya wananchi yawe bora na kuwepo utoshelevu na usalama wa chakula.