Wakulima Chamwino wanavyoweza kuepushwa na changamoto ya ukame

UMASIKINI unaochochewa na ukosefu wa mavuno kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, umeendelea kuwatikisa wakulima katika vijiji vya Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Hivi karibuni, mwandishi wa makala haya alifika katika vijiji vya Chamwino, Buigiri, Chinagali II na Mwegamile katika Tarafa ya Chilonwa na kuzungumza na wakulima, wafugaji pamoja na wadau wengine wa kilimo.

Katika makala haya, anaeleza namna ambavyo utekelezaji madhubuti wa mipango na mikakati ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, unavyoweza kupunguza kama si kukomesha umasikini unaochochewa na uzalishaji mdogo katika kilimo.

Uzalishaji mdogo umejidhihirisha zaidi katika msimu wa mwaka 2016/17 ambao Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino, Athumani Masasi anasema upo upungufu wa tani 4,949 za chakula.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, takribani hekta 83,208 za mazao ya chakula zililimwa na zikazalishwa tani 82,569 za chakula. Mahitaji halisi ya wilaya hiyo yalikuwa tani 87,518. Kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, wilaya ina wastani wa watu 330,543 na wastani wa watu 4.5 kwa kaya.

Akielezea namna uzalishaji ulivyoshuka, mkulima katika kijiji cha Buigiri, Olivia Chinyemba anasema mwaka 2015 alilima ekari moja ya mtama na kuvuna gunia tatu; mwaka jana akapata gunia mbili. Mwaka huu amepata gunia moja la uwele na kwa upande wa mahindi, katika ekari moja amepata debe moja.

Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Chinangali, Michael Mbena, mwaka juzi alilima ekari moja ya mahindi akaambulia gunia nne na ekari moja ya uwele alikopata gunia tano. Mwaka 2016/2017 alilima shamba la ukubwa huo huo akapata gunia mbili na nusu na uwele akapata gunia tano.

Mwaka huu anasema hakupata chochote. Ofisa Mifugo wa Kata ya Buigiri, Stephano Adeline, ingawa hana takwimu rasmi za uzalishaji katika kilimo, anakiri mavuno yamekuwa yakishuka mwaka hadi mwaka kuanzia 2014. “Takwimu kamili sina ila naongea kulingana na ninachokiona.

Mwaka 2014 mavuno yalikuwa mazuri, hata mwaka 2015 mazao yalianza vizuri lakini ilipofika mwishoni , mvua ikakatika,” anasema Adeline akisisitiza kuwa msimu wa 2016/17 hali imekuwa mbaya zaidi.

Asilimia tano ya wakulima 40 waliozungumza na mwandishi wa makala haya kwa nyakati tofauti kutoka vijiji hivyo vya Chamwino, Buigiri, Chinangali II na Mwegamile, wanaamini hakuna namna ya kukabili njaa na umasikini endapo mvua zitaendelea kutotabirika.

“Sisi hatuna majibu, bali tunamwachia Mungu... Ofisa Kilimo utambanaje? Kwani yeye ana chakula? Mungu ndiye anayejua hili tatizo la ukame. Tunamwachia Mungu mipango yake,” anasema mkulima wa Chinangali II, Michael Mbena.

Lakini pia wakulima 14 sawa na asilimia 35 ya waliohojiwa wanasema wataalamu, hususani maofisa ugani ndiyo wanapaswa kuja na suluhisho la uzalishaji mdogo unaochangia umasikini.

Mathalani, Japhet Mdachi, ambaye ni mkulima katika Kijiji cha Buigiri, anasema, maofisa kilimo na mifugo wa vijiji na kata wasisubiri mikutano ya hadhara ndipo wawape ushauri wa kuhimili ukame. Kadhalika, wakulima 24 sawa na asilimia 60 wanasema serikali ndiyo yenye suluhisho wakimaanisha halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Wizara ya Kilimo na Rais.

Hata hivyo, wakulima wote walipohojiwa kama wanaelewa mipango, miongozo au mikakati ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo, walisema hawafahamu. Pia baadhi ya maofisa ugani, wanasema hawafahamu vizuri mipango hiyo, Ofisa Mifugo wa Kata ya Chamwino, David Msimbe anasema: “Mimi ninachokiona, mabadiliko ya tabianchi, nayaelewa kwa sababu nimesoma.

Lakini mpango mkakati wa kitaifa au wa kiwilaya, kwetu sisi tunakuwa hatufahamu vizuri. Hatujui wilaya imejipangaje. Tunatumia uzoefu tu wa kule chuoni ni namna gani ya kuwasaidia wakulima.”

Mpango wa Kilimo wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2014-2019 (ACRP) ni miongoni mwa mipango ambayo wakulima, maofisa ugani, halmashauri na wadau wengine wanapaswa waielewe na kuitekeleza.

ACRP umeainisha maeneo, mikakati na mbinu za kilimo kinachohimili mabadiliko chenye tija kama vile udhibiti wa maji katika ardhi ikiwamo kilimo cha umwagiliaji, uvunaji wa maji na kuyahifadhi na kilimo cha matuta.

Mbinu nyingine zinazoainishwa katika mpango huu ni kuhusu mbegu bora huku mpango ukisisitiza matumizi ya mbegu fupi zinazohimili ukame; uboreshaji wa taarifa za hali ya hewa na kuhakikisha zinawafikia wakulima.

Wapo wanaohimiza Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuandaa kalenda mpya ya kilimo, kwani inasemekana yapo matukio ya wakulima kupishana na kipindi cha mvua kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Programu ya Kitaifa ya Kilimo Kinachohimili Mabadiliko ya Tabianchi ya mwaka 2015 ni mkakati mwingine wa serikali. Programu hii ni dira kwa sekta ya kilimo, ikilenga kuhimili mabadiliko ya tabia nchi na kuwa na usalama wa chakula kwa maendeleo ya uchumi yanayoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Upo pia Mwongozo wa Kilimo Kinachohimili Mabadiliko ya Tabianchi uliozinduliwa Mei mwaka huu ambao maofisa mipango na maofisa ugani wamepewa nguvu ya kupanga na kuandaa bajeti kwa ajili ya maendeleo ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii wanazozitumikia.

Maofisa ugani wanatakiwa kuhamasisha na kufundisha wakulima kutumia mbinu za kilimo zinazohimili mabadiliko ya tabianchi kama vile uvunaji na utunzaji wa maji ya mvua; umwagiliaji kwa njia ya matone; hifadhi ya udongo na maji pamoja na kilimo cha matuta.

Mwongozo unataja Bima ya Mazao kuwa ni mbinu nyingine ya kuwaepusha wakulima kuingia hasara na hatimaye umasikini kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuhusu bima ya mazao, Mratibu wa Bima ya Mazao katika Shirika la Bima la Taifa, Prosper Peter anasema lengo ni kumfidia mkulima ikiwa mazao yameharibiwa na mvua au ukame yakiwa shambani.

Hata hivyo, Prosper anasema shirika lake halijaingiza rasmi bima hii sokoni. Lakini anasema itakapoingia hivi karibuni, imejielekeza kwenye mazao ya biashara. Aidha anasema hakujawa na utaratibu maalumu wa kumsaidia mkulima mdogo asiye na uwezo wa kuchangia katika mfuko wa bima.

“Baadhi ya nchi za wenzetu kumekuwa na utaratibu wa serikali kuchangia gharama ya bima ya mazao lakini Tanzania hakujawa na utaratibu kama huo,” anasema Prosper. Ofisa Tathimini na Ufuatiliaji wa Taasisi ya Dodoma Network Environment (DONET), Emmanuel James katika kuelezea suluhisho la tatizo, anasisitiza halmashaui kuweka kipaumbele kwenye utekelezaji wa mbinu za uhifadhi wa ardhi na maji ikiwamo kuendesha kilimo cha umwagiliaji.

James anashauri mbinu hizo ziende sambamba na kuwapa wananchi njia nyingine za kujipatia kipato wasitegemee kilimo pekee. Anatoa mfano wa ufugaji wa nyuki kuwa ni shughuli isiyohitaji mvua nyingi inayoweza kufanyika wilayani Chamwino na wakulima wakajipatia kipato.

Shirika limekwishatoa mizinga 60 kwa vijiji vya Idifu (wilaya ya Chamwino) na Kikombo (Manispaa ya Dodoma) kila kimoja. Pia kijiji cha Mayamaya na Asanje vimepewa mizinga 38 kila kimoja lengo likiwa ni kuwezesha jamii kujipatia kipato.

Katika kuelezea suluhisho la tatizo, Mkurugenzi wa Shirika la Climate Action Network (CAN) linaloshughulika na masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Sixbert Mwanga, anahimiza wakulima kupatiwa utabiri wa hali ya hewa ulio sahihi, unaojielekeza kwenye eneo mahususi.

Mwanga ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, anasema: “Siyo mkulima apewe utabiri wa jumla. Mfano utabiri unaotaja kuwa mvua itanyesha katika Kanda ya Kati, au utabiri unaosema mvua itanyesha mkoa wa Dodoma, hautoshi.

Mkulima asaidiwe kutumia taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi,” anasema Mwanga. Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga anataja suluhisho lingine la tatizo ni wakulima kuzingatia mwongozo wa uzalishaji mazao kulingana na kanda za kilimo za kiikolojia badala ya kung’ang’ania mazao yasiyostawi katika maeneo yao.

Afisa Tarafa ya Chilonwa, Mohammed Mfaki anasema katika msimu ujao, wamepanga atakayelima mahindi zaidi ya inavyoshauriwa, hawatasita kuyafyeka kwa lengo la kuwafanya wakulima watii ushauri wa kitaalamu. Anatoa mfano kuwa baadhi ya wakulima wameendelea kupanda mahindi ambayo hayastawi katika maeneo yao.

Kulingana na mwongozo huo, mazao ya kipaumbele ya chakula katika Wilaya ya Chamwino ni mtama na njugu mawe na ya biashara ni zabibu na ufuta. Mazao mengine yanayoweza kulimwa ni alizeti, karanga mpunga na viazi vitamu.

Mwongozo huo umezingatia ikolojia ya wilaya hii yenye mwinuko wa meta 500 -1,400, mvua milimita 400 – 800 na udongo mwekundu na kichanga. Mkuu wa Idara ya Mazingira katika Wizara ya Kilimo, Shakwaanande Natai anasisitiza kuwa suluhisho ni mipango, miongozo na mikakati ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi kuwafikia wakulima.