Magufuli kama Kagame kusimamia rasilimali

MWAKA jana, Rais Paul Kagame wa Rwanda alielezea kufurahishwa na uongozi wa Rais mwenzake wa Tanzania, John Magufuli, hususani katika kipengele cha kubana matumizi.

Kagame ambaye yeye na Magufuli mwezi uliopita walisherehekea miaka yao ya kuzaliwa, alizungumza kwa Kinyarwanda na waliotafsiri hotuba hiyo wanasema alikuwa anakemea ziara za mara kwa mara zilizokuwa zinafanywa na maofisa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) nchini mwake, akisema hazina umuhimu.

Kagame alisema maofisa hao walikuwa wanatumia chombo hicho kama njia ya kujinufaisha kwa kufanya ziara na kuhudhuria mikutano ya Jumuiya hiyo hata isiyo muhimu na hivyo akaahidi kuiga mfano wa Rais wa Tanzania, Magufuli, kutokomeza ufisadi huo kwa kusitisha ziara za mawaziri zenye mwelekeo wa kufuja mali ya taifa.

Akizungumza katika mkutano wa faragha wa viongozi wa taasisi zote za serikali nchini mwake, Kagame alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imeanza kuwa ghali na mzigo kwa taifa lake.

“Ni kama mawaziri wa nchi hizi walikubaliana kushinikiza serikali zao kuwa lazima wahudhurie kila aina ya vikao vya Jumuiya hii kwa kisingizio kuwa waziri anayeshindwa kuhudhuria nchi yake inachukuliwa hatua ama inaonekana kupinga juhudi na mikakati ya jumuiya,” alisema Rais Kagame.

Kagame alikaririwa akipongeza juhudi za Rais Magufuli za kukomesha ufisadi uliokuwa umekithiri katika taasisi za serikali ya Tanzania, na kwamba lazima na yeye afuate nyayo hizo katika suala zima la kukomesha ufisadi.

Kabla ya hapo, Rwanda ilikuwa pia imesifia hatua zilizochukuliwa na serikali ya Rais Magufuli katika ‘kusafisha’ ufisadi katika bandari ya Dar es Salaam. Rais Magufuli, baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), mwaka jana, aliitaka sekretarieti ya chombo hicho kukumbuka kwamba wanahudumia nchi za watu masikini na hivyo kujitahidi kadri inavyowezekana kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko, alisema hatua za mwanzo za kubana matumizi kufuatia agizo la Magufili, hasa kuzuia safari zisizo za lazima Jumuiya ilikuwa imeshaokoa dola za Marekani 588,768 (zaidi ya Sh bilioni 1.2) ndani ya kipindi cha miezi minne kuanzia Mei hadi Agosti, mwaka jana.

Kabla ya kupiga hodi EAC, Rais Magufuli pia alikuwa keshazuia ziara za maofisa wa serikali ya Tanzania nje ya nchi akiagiza kwamba mpaka zifanywe kwa kibali chake baada ya kujiridhisha kwamba zina tija kwa taifa. Wakati Rwanda ikiisifia Tanzania, Rais Magufuli naye aliwahi kuitolea Rwanda ya Kagame mfano kwamba hakuna majambazi kiasi cha mabasi ya abiria kulazimika kusindikizwa na askari kama ilivyo kwa Tanzania.

Lakini wakati Kagame akimsifia Magufuli na Magufuli akiisifu Rwanda kwa kukomesha ujambazi, wawili hao wana mengi ya kupendeza, kufanana na pengine ni muhimu kuigana pia.

KAGAME KAFANYA NINI?

Kagame ambaye Jumatatu ya wiki iliyopita alisherehekea miaka 60 ya kuzaliwa kwake, ameifanyia mengi Rwanda toka aingie madarakani. La kwanza kabisa linalotajwa ni chama chake cha Rwandan Patriotic Front (RPF) kuweza kusimamisha mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 huku jumuiya ya kimataifa ikiwa inaangalia tu bila kutoa mchango wa maana.

Katika mauaji hayo, inakadiriwa kwamba takriban watu 800,000, wengi wao wakiwa Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa. Viongozi wengi wa mataifa makubwa wamekuwa wakiona aibu kwa jinsi walivyoshindwa kusaidia kukomesha mauaji nchini humo hadi RPF iliyokuwa ikipigana kutoka msituni ilipofanikisha hilo.

Lakini Kagame anasifiwa zaidi kwa kuitoa nchi katika ‘majivu’ ama kukaribia kufutika kabisa na kuinyanyua kwa kasi hadi ilipo sasa baada ya kuingia madarakani huku wengi wakidhani kwamba RPF ambayo kimsingi ilikuwa chama cha Watutsi wachache isingefika popote.

Anasifiwa pia kwa kuanzisha harakati za maridhiano na kupunguza uhasama wa asili baina ya makabila mawili makubwa nchini humo, Wahutu na Watutsi. Kabila lingine nchini humo lenye asilimia ndogo ya watu ni Watwa. Kagame anasifiwa pia kwa kuwapa nafasi zaidi za kiutawala wanawake kulinganisha na watawala wa zamani nchini humo na hata nchi nyingine za Afrika.

KUPAMBANA NA UFISADI

Kwa kipindi kifupi, Kagame ameweza kufanya mengi ambayo yamewashinda viongozi wengi wa Afrika kama ilivyo kwa Magufuli. Mbali na kukuza uchumi wa nchi, amejidhihirisha kuwa mmoja wa watawala wachache wa Kiafrika aliyedhamiria kukomesha ufisadi akitaka rasilimali za nchi ziwanufaishe wananchi wote, hususan masikini. Wakati fulani akihojiwa na kipindi cha Monday Agenda kilichorushwa na Capital Television ya Dar es Salaam, Kagame alisema ameamua kwa dhati kupambana na ufisadi, licha ya kwamba inamgharimu yeye mwenyewe dhidi ya marafiki zake, yaani ‘wakombozi’ wenzake katika RPF ambao waliamini kwamba wakipata madaraka ya kutawala basi itakuwa ni nafasi yao ya kuanza ‘kula nchi’.

Anasema hawezi kulinda maslahi ya genge la watu wachache wanaotaka kutumia madaraka yao serikalini kujinufaisha dhidi ya maslahi ya umma mpana wa Wanyarwanda. Anaweka wazi kwamba, maadui wake wa kisiasa, mbali na wale wanaoendekeza tabia zilizozaa mauaji ya kimbari nchini humo na ukabila, ni wale wenye nia ya kutumia rasilimali za nchi kwa manufaa yao.

Kutokana na kusimamia vyema uchumi na kupinga rushwa, Rwanda imepiga hatua kubwa katika huduma za jamii kama afya na elimu kuliko wakati wowote toka nchi hiyo ipate uhuru.

Mwaka 2005, mwandishi wa gazeti moja la Botswana aliyetembelea Rwanda, aliwahi kunukuliwa akiandika haya yafuatayo (kwa tafsiri isiyo rasmi). Angalia katika: http://www. gazette.bw/tbg_buhead2.htm:

Anasema alipotembelea jiji la Kigali, alikuta serikali ya Kagame ikiwa imeamua ‘kutaifisha’ magari ya kifahari yaliyonunuliwa na serikali hiyo na kuendeshwa na mawaziri, maofisa usalama na viongozi wa kijeshi. Serikali hiyo ilikwenda mbali zaidi hadi ikawa inakamata magari ya wataalamu kutoka nje.

Mwandishi huyo anasema, asubuhi moja, maofisa waandamizi wa serikali walipoamka walikuta askari polisi wakiwa wametanda kila mtaa wakisimamisha na kisha kuchukua magari ya serikali bila kuangalia sura ya mtu na kuwaacha wakitembea kwa miguu kwenda maofisini.

Baadhi ya wafadhili wa kimataifa wanaoonekana kila sehemu Afrika wakidai wapo kwa ajili ya kusaidia bara hili kuondokana na umasikini nao walikumbwa na hatua hiyo hadi kujikuta wakitembea vichwa chini.

Wafadhili waliokunwa na hilo ni wale waliokuwa wanatembelea magari ya kifahari, wakitumia ofisi ghali na za kisasa, wakilipana mishahara minono na pia kuishi katika majumba ya kifahari licha ya kudai kwamba wako Rwanda ‘kukomboa masikini’! Katika hali ya kujiamini, Rwanda iliyashikilia hata magari yanayomilikiwa na miradi ya wahisani. Hatua hiyo ilikuja baada ya Kagame kusafisha ufisadi katika serikali yake.

Mwandishi huyo wa Botswana anasema hatua yake hiyo, licha ya kumjengea maadui wengi wakiwemo marafiki zake wa zamani, iliwatisha pia wahisani na wafadhili. Akiongea na mwandishi huyo, Kagame alisema kwamba aliangalia katika baadhi ya miradi ya kupunguza umasikini na kugundua kwamba ina harufu ya ufisadi na haina tija.

“Kuna mradi hapa, kwa mfano, una thamani ndogo tu ya dola za Marekani milioni tano, lakini nilipoangalia matumizi, nikagundua kwamba dola milioni moja katika mradi huo zinakwenda kwenye kununua magari ya kifahari, kila moja likiwa na thamani ya dola 70,000.

“Kiasi kingine, dola milioni moja zinatumika kununua samani za ofisi, zaidi ya dola milioni moja nyingine zikitumika kwa ajili ya mikutano na pia dola nyingine milioni moja zikitumika kwa kuwalipa wataalamu na hivyo kubakia dola milioni moja tu zinazokwenda kwenye matumizi halisi ya kupunguza umasikini. Hapo kweli tunapambana na umasikini ama kiini macho?” Alihoji Kagame.

Magari yaliyokamatwa yalipigwa mnada kisha serikali yake ikapiga marufuku ununuzi wa magari ambayo ukubwa wa injini zake unazidi cc 2,500. Serikali ya Kagame pia iliweka ukomo wa matumizi ya simu za mikononi kwa mawaziri wake, viongozi wa kijeshi na maofisa usalama kutozidi Faranga 50,000 za Rwanda kwa mwezi (takriban Sh 135,000 za Tanzania).

Serikali ya Rwanda pia ilipiga marufuku semina, warsha na mikutano inayohusu kupunguza umasikini kufanyikia kwenye mahoteli ya kifahari na hivyo tangu mwaka 2005 semina kama hizo zimekuwa zikifanyikia kwenye majengo ya serikali kwa gharama ndogo au bila gharama kabisa.

Serikali ya Kagame pia iliagiza wizara na idara zote za serikali kuondoka kwenye majengo binafsi yanakolipiwa pesa nyingi za serikali na kwenda kwenye majengo ya serikali. Kagame, pia alishaweka wazi kwamba anapokuwa anatetea maslahi ya watu wake haangalii mtazamo wa nchi wafadhili.

Nchini Rwanda, mawaziri ama maofisa wengine waandamizi wa serikali wanatakiwa kujiuzulu nyadhifa zao na wakati mwingine kufukuzwa kazi pale wanapotuhumiwa tu kwa ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

“Sisi hapa Rwanda, kama hakuna ushahidi wa kukutia hatiani kwamba umeiba pesa za umma kwa kutumia nafasi yako, tunakuomba uache kazi ya umma ama tunakufukuza kazi,” alisema Kagame kumwambia mwandishi huyo wa Botswana.

Kutokana na juhudi zake za kukuza uchumi na kupambana na ufisadi kwa dhati, kwa muda mrefu Serikali ya Kagame imekuwa ikichukuliwa na wahisani wengi kama inayojitahidi katika suala zima la utawala bora.

Wakati fulani, Kagame alifanya mkutano na waandishi wa habari na kusema kwamba mapambano ya serikali yake dhidi ufisadi yataendelea kuimarika na wale wanaodhani kwamba ni nguvu ya soda basi hawajui walifikirialo.

Kagame pia amepigana kuhakikisha kwamba kile mtumishi wa serikali alichoiba lazima kinarudishwa serikalini na hasa pale mahakama inapomtia hatiani mtu huyo. Kwa Watanzania wanaosoma hapo juu, bila shaka wataona kwamba mengi aliyofanya Kagame ndiyo anayofanya Rais Magufuli kama vile kupiga marufuku mikutano ya kiserikali au taasisi za umma kwenye mahoteli ya kifahari, kupambana na watumishi wa umma wezi na kadhalika.

Kagame kama Magufuli Pamoja na mafanikio hayo makubwa, Kagame analalamikiwa kwa kuminya demekrasia dhidi ya wapinzani wake. Katika kujibu hilo, amekuwa akisema kwamba wanaodai anaminya demokrasia ni mafisadi au mawakala wao sambamba na wanaopenda kuendekeza ukabila baina ya Wahutu na Watutsi.

Hayo pia ndiyo yanamkuta sasa Rais Magufuli ambaye Jumapili ya juzi alisherekea miaka 58 ya kuzaliwa, katika kudhibiti ufisadi na matumizi ya ovyo ya rasilimali za umma ambapo wameibuka mawakala wa mafisadi, wanyonyaji na ‘wapiga dili’ waliokalia kumchafua Magufuli sambamba na kumwita dikteta.

Wakati fitina za mawakala wa ufisadi zikimwandama Magufuli kama zinavyomwandama Kagame, Tanzania inaanza kupaa kimaendeleo kama Rwanda ambayo imejipanga kufikia Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2020. Tanzania imejipangia kufikia hatua waka 2025.