Hoteli ya kifahari yageuzwa gereza

DUNIA haiishi vituko na mara zote kumekuwa kunaibuka kwa vituko mbalimbali ambavyo kwa ujumla wake vinasaidia katika kuifanya Dunia kuwa eneo la watu kuishi na kufurahi.

Makala haya ya kimataifa wiki hii yameangazia hoteli ya kifahari wanamozuiliwa wana wa wafalme Saudi Arabia Ritz – Carlton ni jina la moja ya hoteli za kifahari zilizo maarufu kote duniani.

Marais, Mawaziri Wakuu na wafalme wamekaribishwa katika hoteli hizo ya Ritz-Carlton mara kadhaa. Lakini kwa mujibu wa ripoti kadhaa, hoteli hizo zilizo katika mji mkuu wa Saudi Arabia wa Riyadh yamekuwa gereza.

Watu kadhaa mashuhuri nchini Saudi Arabia sasa wanaripotiwa kuwekwa kizuizini katika hoteli hiyo inayotumika pia kufikia wageni mashuhuri wa serikali huku hoteli hiyo ikitajwa kuwa gereza la kifahari zaidi duniani.

Wana wa wafalme 11, mawaziri wanne na watu wengine kadhaa wamekamatwa katika kile mamlaka za Saudi Arabia zinasema kuwa ni kampeni ya kupambana na ufisadi nchini humo. Bilionea maarufu duniani humo, Prince Alwaleed bin Talal anaripotiwa kuwa miongoni mwa wale waliokamatwa na kushikiliwa katika gereza hilo la aina yake.

Mtandao wa gazeti la The New York Times ulichapisha kanda ya video iliyoonesha matumizi hayo mengine mapya ya Hoteli ya Ritz-Carlton Riyadh. Katika video hizo walinzi wanaonekana wamelala kwenye mikeka katika chumba kimoja cha hoteli, watu wenye sare pia nao wanaonekana huku bunduki zikionekana zikiegeshwa kwenye ukuta.

Gazeti la Guardian liliripoti kuwa wageni waliombwa siku ya Jumatano jioni wakusanyike sehemu moja na mizigo yao, kabla ya kusafirishwa kwenda kwa hoteli zingine mjini Riyadh ili kuifanya hoteli hiyo kubakia na jukumu moja la kuwahifadhi wafungwa.

The Guardian imemnukuu ofisa mmoja wa Saudi Arabia akisema kuwa mamlaka hazingeweza kuwaweka watu hao gerezani na hilo lilikuwa suluhu bora. Jitihada za kulipia vyumba katika hoteli hiyo siku ya Jumanne hazikuzaa matunda.

Hatua hiyo imekuja katika wakati ambao nchi hiyo imekuwa inachukua hatua mbalimbali za kubadili mifumo ya kimaisha. Hivi karibuni Saudi Arabia ilitangaza kuanza kuwaruhusu wanawake kuhudhuria michezo katika viwanja vya michezo kwa mara ya kwanza kuanzia mwaka ujao.

Sasa familia zitaweza kuingia kwenye viwanja vitatu vya michezo vya - Riyadh, Jeddah na Dammam. Ni hatua nyingine ya kuwapa wanawake wa Saudi Arabia uhuru zaidi, ambao kawaida hukumbwa na ubaguzi wa kijinsia na baada ya kuondolewa marufuku ya kuendesha magari.

Mfalme Mohammed bin Salman yuko katika harakati kubwa kuifanya Saudi Arabia kuwa nchi ya kisasa na kuboresha uchumi. Mabadiliko hayo yanaambatana na mipango mikubwa ya mabadiliko yaliyotangazwa na mfalme huyo wa umri wa miaka 32 kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa taifa hilo linalotegemea mafuta, yanayojulikana kama maoni ya mwaka 2030.

Mwaka jana amri ya kifalme ilisema kuwa wanawake wanaweza kuendesha magari kwa mara ya kwanza kuanzia mwezi Juni mwaka huu. Warsha zinafanywa na sinema zinatarajiwa kurejeshwa tena.

Siku ya Jumatano Prince Mohammed alisema kurejeshwa kwa Uislamu wa wastani ni kiungo muhimu cha kuifanya nchi kuwa ya kisasa. Alisema kuwa asilimia 70 ya watu nchini Saudi Arabia wana umri wa chini ya miaka 30 na alisema kuwa wanahitaji maisha ambayo yanastahili dini.

Lakini wadadisi wanasema mipango haitakosa pingamizi. Wanawake nchini Saudi Arabia bado ni lazima wafuate mitindo ya mavazi na wasiwe na mahusiano na wanaume wasiostahili.