Ni ligi ya matukio

LIGI Kuu Bara imesimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati inayotarajiwa kutimua vumbi Nairobi kuanzia kesho. Michuano hiyo inashirikisha timu kutoka nchi wanachama wa Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) ambapo ndugu Tanzania Bara na Zanzibar zimepangwa kundi moja.

Mbali na hilo pia wachezaji wengi wa kigeni ambao wanatoka nchi za ukanda huo ambao wanacheza Ligi Kuu Bara watalazimika kujiunga na timu zao za taifa kushiriki michuano hiyo. Ligi imesimama huku kila timu ikiwa imeshacheza mechi 11 na kila mmoja ameona alichokivuna hasa ikizingatiwa zimebaki mechi nne kumalizika kwa mzunguko wa kwanza.

Ni wakati wa kujitathimini kuona wapi wamekosea na pindi ligi itakapoendelea warekebishe makosa na kufanya vizuri kwenye mechi zao. Kiuhalisia ligi ya msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa zaidi na ndiyo maana kinara wa ligi hiyo Simba inaongoza kwa tofauti ya mabao tu baada ya kulingana pointi 23 na Azam inayoshika nafasi ya pili.

Yanga ambayo ni ya tatu ina pointi 21 ikifuatiwa na Singida United yenye pointi 20 na nafasi ya nne inashikwa na Mtibwa Sugar yenye pointi 19. Kwenye msimamo kuanzia kinara mpaka timu inayoshika mkia, nyingi zimepishana kwa tofauti ya pointi chache, na hapo ndipo inapodhihirika ugumu wa ligi hiyo.

Msimu huu mechi nyingi zinamalizika kwa sare na endapo timu itaibuka na ushindi basi huwa mwembamba aidha 1-0, 2-1. Ni Simba na Yanga tu ndizo zilizopata ushindi mkubwa. Simba ilimfunga Ruvu Shooting mabao 7-0, ikamfunga Njombe Mji 4-0.

Yanga walimfunga Mbeya City 5-0 na kisha wakaifunga Stand United mabao 4-0. Mbali ya ugumu uliokuwepo msimu huu ligi hiyo kuna matukio kadhaa yametokea na kwenye makala haya tunakuletea baadhi ya matukio hayo ambayo yalionekana kuwa si ya kawaida.

SIMBA KUDAI KUONEWA

Ikiwa ligi inazidi kuchanganya wapenda soka wengi walishtushwa na kushangazwa na kitendo kilichofanywa na Simba SC kudai kuwa wamekuwa wakionewa kwenye baadhi ya mechi zao hali inayowafanya kuwa na wakati mgumu kwenye kusaka pointi tatu kwenye mechi zao.

Simba kupitia kwa mkuu wake wa kitengo cha habari, Haji Manara, alitoka mbele ya waandishi wa habari akiwa na ushahidi wa video za mechi mbalimbali ambazo wanadai kuwa waamuzi hawakuwatendea haki.

Jambo hilo lilitoa mjadala mkubwa kwa kushangaa kuwa kwa nini hawakupeleka malalamiko hayo sehemu inayostahili ambapo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kupata haki yao na badala yake kulalamika kwa waandishi wa habari ambao hawawezi kutoa maamuzi yoyote.

ASANTE KWASI

Huyu ni beki wa kati wa timu ya Lipuli FC ya Iringa ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu. Raia huyu wa Ghana alijiunga na timu hiyo akitokea Mbao FC ambayo msimu uliopita ilikuwa ikitikisa kwenye ligi.

Licha ya kuwa beki wa kati lakini ameshangaza wengi baada ya kuoneka kuwa na uwezo wa kupachika mabao tena muhimu kama vile anacheza nafasi ya ushambuliaji. Mpaka sasa ana mabao matano sawa na mshambuliaji wa Yanga aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Simba, Ibrahim Ajib, na kuwa nyuma kwa mabao matatu na kinara wa mabao Emmanuel Okwi wa Simba.

USAJILI WA SIMBA WASHTUKIWA

Mwanzoni mwa msimu Simba ndiyo ilitikisa kutokana na kufanya usajili wa nguvu ambao unakadiriwa kuwa wa takribani shilingi bilioni moja. Kati ya wachezaji hao waliowasajili ni Okwi, Haruna Niyonzima, Bocco na Aishi Manula.

Macho ya wapenda soka wengi nchini yalitamani kuona usajili huo utatoa matunda gani ligi itakapoanza. Lakini mpaka raundi ya 11, imekuwa kinyume na matarajio ya wengi kwani haikuwa na makali ya kutisha hali iliyowafanya wawe kileleni wakiwa sawa kwa pointi na Azam. Kutokana na mwenendo huo wengi wanahoji thamani ya fedha zote hizo hazijaonekana kwenye kikosi hicho.

MFUNGAJI BORA ANA BAO MOJA

Msimu uliopita kulikuwa na wafungaji bora wawili, Simon Msuva aliyekuwa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting. Wachezaji hao wote waliibuka kuwa wafungaji bora baada ya kupachika mabao 14 kila mmoja. Msuva kwa sasa ameihama Yanga na amejiunga na timu ya Difaa al Jadid ya Morocco lakini Abdulrahman bado yupo na timu yake ya Shooting.

Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita alionekana kuwa moto tangu mwanzo wa ligi, msimu huu mpaka sasa ana bao moja tu.

NGOMA HAJULIKANI ALIPO

Mashabiki wa Yanga kwa nyakati tofauti walipatwa na wasiwasi baada ya kusikia mchezaji wao kipenzi, Mzimbabwe Donald Ngoma hajulikani alipo baada ya kuondoka kwenye timu hiyo bila ruhusa kutoka kwa uongozi.

Tangu msimu uliopita iliripotiwa kuwa Ngoma alikuwa na mikwaruzano na uongozi wa timu hiyo na zilipokuja taarifa hizo mashabiki wa Yanga wakajua kuwa mshambuliaji wao huyo tayari ameshaondoka moja kwa moja.

Zikaja taarifa zingine zilizowachanganya watu pia mchezaji huyo amejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe kinachokwenda kushiriki michuano ya Cecafa huku ikiwa mchezaji huyo hajaitumikia timu yake ya Yanga kutokana na kuwa majeruhi