Hatimaye Afrika imechukua hatua kuelekea Soko la Pamoja

WAKUU 44 wa bara la Afrika waliokutana jijini Kigali (Rwanda) tarehe 21 Machi mwaka huu wamesaini makubaliano ya kuanzisha soko huria barani Afrika. Matokeo yake ni kuundwa kwa jumuiya moja ya kiuchumi katika bara letu badala ya mfumo wa hivi sasa wa kuwa na jumuiya za kikanda kama COMESA (nchi 26), EAC (nchi 6) na SADC (nchi 15).

Marais walisaini makubaliano haya (Continental Free Trade Area – CFTA) huku kwaya ikiimba wimbo mashuhuri wa hayati Bob Marley unaosema “Tuungane” (Let’s get together). Lengo la CFTA ni kuunda soko moja la Afrika ili kukuza biashara miongoni mwa nchi za Kiafrika. Hivi sasa biashara hii ni asilimia 12 tu ya biashara yote. Maana yake asilimia 82 ya biashara ya Afrika ni kati yake na nchi za nje.

Hii asilimia 12 ni ndogo sana ikifananishwa na Amerika Kusini (asilimia 22), Amerika Kaskazini (40), Asia (50) na Ulaya Magharibi (70). Wakuu wa nchi zote 55 za Umoja wa Afrika (AU) walijadili muswada wa CFTA kwa muda wa miaka miwili, lakini si wote waliosaini. Kuna nchi kama Nigeria na Afrika Kusini ambazo ziliomba muda zaidi wa kutafakari.

Na hata nchi zilizosaini itabidi mabunge yao yaridhie. CFTA itaanza kutumika pale tu nchi zisizopungua 22 zitakaporidhia. Baada ya hapo nchi hizo zitafungua mipaka yao ili bidhaa kutoka Afrika ziingie bila ushuru au vikwazo. Bidhaa chache ambazo wanafikiri ni nyeti zitaendelea kutozwa ushuru. Nchi zitakazoridhia zitapaswa ziorodheshe bidhaa hizo. Licha ya CFTA kuna makubaliano mengine ya kuruhusu Waafrika kusafiri bila ya viza (Single African Air Transport Market). Waraka huu ulisainiwa na wakuu 27, wakikubali kuruhusu raia wa Afrika kuingia nchini mwao na kukaa kwa muda usiozidi siku 90 bila ya kutakiwa kuomba kibali (viza). Hii pia ni hatua muhimu na ya kihistoria katika bara la Afrika.

Ilitokana na mkutano wa wakuu wa AU uliofanyika mjini Addis Ababa mnamo Januari mwaka huu. Matokeo yake ni kuwa na soko moja la safari. Inategemewa kuwa usafiri miongoni mwa nchi za Afrika utaongezeka na hii itasaidia kuendeleza uchumi wetu. Wakati CFTA inasainiwa huko Kigali, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria hakuwepo. Alifuta safari yake kutokana na mjadala unaoendelea nchini mwake kuhusu makubaliano hayo.

Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini humo (Nigeria Labour Congress – NLC) pamoja na wafanyabiashara wana wasiwasi kuwa CFTA huenda ikaathiri viwanda vya Nigeria ambavyo vinahitaji kulindwa. Walitoa mfano wa kampuni yao kubwa ya Dangote, wakisema kiwanda chake cha simenti hakingefanikiwa bila ya kuzuia simenti kutoka nje. Labda ni kweli kuwa viwanda vya Nigeria vinahitaji kulindwa lakini kwa upande wa pili chini ya CFTA simenti ya Dangote itapata soko barani kote bila ya kutozwa ushuru. Licha ya Nigeria, nchi zingine ambazo bado kusaini CFTA ni Afrika Kusini, Burundi, Lesotho, Namibia, Eritrea, Benin, Sierra Leone na Guinea Bissau. Hata hivyo nchi hizo zimepewa siku 90.

Inategemewa kuwa wakuu wao watasaini watakapokutana tena nchini Mauritania mnamo Julai mwaka huu. Faida moja kubwa ya CFTA ni kuifanya Afrika kuwa soko moja kubwa. Viwanda vya Afrika vitakuwa na fursa ya kuuza kokote katika bara hili. Hii itatoa msukumo mkubwa kwa ukuaji wa viwanda katika bara letu. Wawekezaji wa ndani na wa nje watapata motisha wa kuwekeza kwa wingi kwa sababu watakuwa na uhakika wa soko kubwa. Hatutakuwa tena tunazalisha kwa ajili ya soko la ndani tu bali kwa soko la Afrika lenye watu bilioni 1.2 Kwa njia hii inakisiwa kuwa uchumi wa bara utakuwa unapanuka kwa asilimia 6 hadi 7 kila mwaka. Ifikapo mwaka 2050 uzalishaji wa bara zima (GDP) utafikia dola trilioni 29.

Hii ni sawa na GDP ya Umoja wa Ulaya na Marekani kwa pamoja. Soko huria pia litapunguza urasimu. Vibali vya kusafirisha au kuagiza bidhaa vitapungua. Urasimu pia utapungua kwa wasafiri kwa vile Waafrika hawatahitaji viza za kusafiri ndani ya Afrika. Chini ya ukoloni tulikuwa na mfumo wa biashara iliyotawaliwa na Ulaya. Ilikuwa rahisi kwa nchi za Kiafrika kufanya biashara na Ulaya kuliko baina yao wenyewe. Na biashara tuliyofanya ni sisi kuwauzia pamba yetu halafu kununua nguo kutoka kwao. Huu ndiyo mfumo tuliourithi mpaka leo.

Ndiyo maana tunaona biashara kati ya Waafrika leo ni asilimia 12 tu ya jumla ya biashara yetu yote. Ndiyo maana tunaona zaidi ya nusu ya mafuta yanayozalishwa Afrika yanakwenda nje ya bara letu. Halikadhalika na bidhaa ghafi kama pamba na kahawa. Matokeo yake ni kuwa katika bidhaa zote zinazosafirishwa nje ya Afrika ni asilimia 18 tu zinatoka viwandani. Wakati huohuo, bidhaa zetu zinazouzwa Afrika zinalipiwa ushuru zaidi kuliko unaolipwa Ulaya. Kwa maneno mengine chini ya mfumo wa sasa ni nafuu kuuza bidhaa zetu Ulaya kuliko kuuza kwa Waafrika wenzetu. Lengo la CFTA ni kuleta mageuzi makubwa ili ifikapo 2022 biashara kati yetu itaongezeka kwa kiwango cha asilimia 60.

Ingawa tutakuwa tumepoteza ushuru tunaotoza hivi sasa lakini tutakuwa tumeongeza soko kwa bidhaa zetu. Kwa mfano, itakuwa rahisi kuuza viatu vyetu katika nchi za Kiafrika. Ni ndoto kutegemea soko la Ulaya kwa sababu wanachotaka wao ni sisi kuendelea kununua mitumba kutoka kwao. CFTA ni sehemu ya mpango wa maendeleo wa AU wenye lengo la kurahisisha biashara na safari barani Afrika ifikapo mwaka 2063. Biashara ikiongezeka na safari zitaongezeka. Mfanyabiashara wa DRC hataenda China kutafuta simu za mkononi. Badala yake atakuja Tanzania. Wawekezaji wetu hapa nchini watafungua kiwanda cha kutengeneza simu au redio au kompyuta hapa kwetu na kuziuza katika bara zima la Afrika.

Na wao watatengeneza bidhaa zao ambazo zitahitajika hapa kwetu. Ufanisi wa makubaliano haya utategemea zaidi utekelezaji wa mikataba ya umoja wa kanda ambayo tayari imekuwepo kwenye bara hili kwa miaka mingi sasa. Kuna jumuia saba za kikanda katika Afrika. Jumuia zenyewe ni soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika (COMESA), jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), jumuiya ya kiuchumi ya Afrika ya kati (ECCAS), mamlaka ya maendeleo mashariki mwa Afrika (IGAD) na jumuiya ya nchi za Sahel na Sahara (CENSAD). Kwa kiasi fulani jumuia hizi zimesaidia kuunda soko la pamoja katika kanda zao.

Hata hivyo, tukiangalia kila moja tunaona kuwa zimepishana. Kwa mfano, katika SADC biashara ya ndani ni asilimia 21, EAC ni asilimia 13 na COMESA ni asilimia 8, wakati ECCAS ni asilimia 2 tu. Ni dhahiri kuwa tuna safari ndefu mpaka kuwa na soko la pamoja lenye nguvu barani Afrika. Ikiwa Umoja wa Ulaya (EU) wamefanikiwa kuuziana wenyewe kwa asilima 65 ya bidhaa zao na jumuiya ya Asia Kusini Mashariki (ASEAN) kuuziana kwa asilimia 23, ni dhahiri Afrika tuna safari ndefu. Hata hivyo, CFTA ni hatua muhimu na ya kihistoria kufikia lengo letu.

Ni hatua ya kihistoria kwa sababu tumeanza kutekeleza ndoto ya waasisi wa umoja wa bara letu. Wao walikuwa wanataka kuliona bara la Afrika siku moja likiwa limeungana na wakazi wake wakitembea bila vipingamizi. Hiki si kitendo cha kusaini tu makubaliano, bali ni hatua muhimu ya kuthubutu kutekeleza mkakati mpana wa kuifikia “Afrika tuitakayo”. Ni hatua ya kutekeleza ndoto ya waasisi wetu kina Kwame Nkrumah (Ghana), Mwalimu Julius Nyerere (Tanzania), Gamal Abdel Nasser (Misri), Nelson Mandela (Afrika Kusini), Ahmed Sékou Touré (Guinea), Thomas Sankara (Burkina Faso), Muammar Gaddafi (Libya) na Patrice Lumumba (DR Congo)