Mavugo aipa raha Simba

MSHAMBULIAJI wa Burundi, Laudit Mafugo aliifungia timu yake ya Simba bao 1-0 dhidi ya Madini FC ya hapa na kuipeleka timu hiyo nusu fainali za michuano ya Kombe la Shirikisho, FA.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa, Madini ilionesha soka safi kuizidi Simba inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu bara kwa tofauti ya pointi mbili.

Iliichukua Simba mpaka dakika ya 60 kupata bao hilo pekee kwenye mechi hiyo ambapo Mavugo alilifunga kwa kichwa baada ya kuuwahi mpira uliomshinda beki wa Madini Hamisi Hamisi.

Katika mechi hiyo Simba ilipata wakati mgumu hasa kipindi cha kwanza ambapo wenyeji walicheza mchezo wa kujilinda zaidi hali iliyowapa wepesi wa kuwadhibiti vinara hao wa Ligi Kuu.

Kuingia kwa bao hilo la Mavugo ni kama kuliwaamsha wachezaji wa Madini kwani sasa walionekana kufunguka na kuliandama lango la Simba kusaka bao la kusawazisha lakini haikuwa rahisi kwao kwani Simba nao wakafanya mashambulizi kwa wenyeji wao ambapo katika dakika ya 70 beki Hamisi alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la Shiza Kichuya lililokuwa likielekea wavuni.

Matokeo hayo ni faraja kwa Simba ambayo msimu uliopita ilitolewa robo fainali na Coastal Union ya Tanga. Bingwa wa michuano hiyo anaiwakilisha nchi kwenye kombe la Shirikisho Afrika na Simba inawania nafasi ya uwakilishi wa kimataifa kwa mwaka wa tano sasa.

Simba sasa inaungana na Mbao FC ya Mwanza kutinga nusu fainali baada ya timu hiyo ngeni kwenye Ligi Kuu bara kuiondosha mashindanoni timu kongwe ya Kagera Sugar kwa kuifunga mabao 2-1 kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba juzi.

Simba na Mbao zinasubiri washindi wa mechi kati ya Azam FC na Ndanda FC na Yanga SC na Prisons ambazo zitapangiwa tarehe baadae kutokana na Yanga na Azam kuwa kwenye michuano ya kimataifa ya Caf.

Kikosi cha Simba: Daniel Agyei, Janvier Besala Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Juuko Murshid, James Kotei, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin/ Jonas Mkude dk58, Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib/Pastory Athanas dk70, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/ Said Ndemla dk46.

Madini FC: Ramadhani Chalamanda, Lazaro Constantine, Makiwa Feruzi, Hamisi Hamisi, Priscus Julius, Edward Eliau, Gibson Joseph, Shaaban Imamu, Athumani Dennis, Awesu Awesu/Rajab Mwaluko dk72, Mohammed Athumani/ Mohammed Athumani dk56.