Yanga yakata pumzi

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga imeaga mashindano hayo baada ya kushindwa kutamba ugenini ikitoka sare ya bila kufungana 0-0 katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Mashujaa, Zambia.

Kutokana na matokeo ya awali katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ya sare ya bao 1-1, Zanaco wanasonga mbele hatua ya makundi kwa faida ya bao la ugenini, huku Yanga ikiangukia Kombe la Shirikisho Afrika.

Kipindi cha kwanza timu zilikuwa zikishambuliana kwa zamu na kutengeneza nafasi za kufunga, lakini hakuna aliyefanikiwa kuchungulia lango la mwenzake na kufanya matokeo kuwa 0-0 hadi timu zinakwenda mapumziko.

Wachezaji kama Chirwa, Niyonzima, Thaban Kamusoko na Haji Mwinyi walitengeneza nafasi kwa nyakati tofauti kipindi cha kwanza na kushindwa kuzitumia ipasavyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuongeza mashambulizi huku Zanaco ikionekana kucheza bila kutumia nguvu nyingi wakionekana wazi kuwa wanataka sare ili waweze kusonga mbele.

Kocha George Lwandamina alijaribu kufanya mabadiliko kwa kumtoa Geofrey Mwashiuya na kumuingiza Emanuel Martin lakini bado hakukuwa na matokeo chanya.

Wachezaji waliendelea kutengeneza nafasi za kufunga kama Simon Msuva, Martin na Chirwa bado walishindwa kuzitumia ipasavyo.

Hadi dakika 90 za mchezo zinamalizika hakuna aliyefumania nyavu ya mwezake na kufanya matokeo hayo kuishia kwa sare ya kutokufungana huku Yanga ikiaga rasmi mashindano hayo na kujipanga kwa Kombe la Shirikisho.