Yanga haizuiliki

YANGA jana imezidi kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu bara baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Yanga kurejea tena kileleni mwa msimamo wa ligi kwa uwiano mzuri wa mabao baada ya kufikisha pointi 65 sawa na Simba iliyo nafasi ya pili. Yanga sasa imejisafishia njia ya ubingwa kwani ikishinda mechi yake ijayo dhidi ya Toto Africans keshokutwa itaipa Simba kazi ya kushinda mabao mengi dhidi ya Mwadui na huku ikiomba Yanga ipoteze mechi ya mwisho kwa Mbao.

Mabingwa hao watetezi wanatambia wingi wa mabao yao ya kufunga ambapo mpaka jana wamepachika mabao 56 kulinganisha na Simba yenye mabao 50 na kwa matokeo ya kila upande kushinda, huenda bingwa akaamuliwa kwa uwiano mzuri wa mabao.

Sasa ni dhahir kwamba njia imezidi kuwa nyeupe kwa Yanga kutetea ubingwa kutokana wepesi wa mechi yake inayofuata dhidi ya Toto Africans keshokutwa ambapo mara nyingi huifunga. Toto haipo kwenye nafasi nzuri, na ikifungwa na Yanga itakuwa imejichimbia kaburi kwenye ukanda wa kushuka daraja.

Simon Msuva aliiandikia Yanga bao la kuongoza katika dakika ya nane akiunganisha krosi ya Hassan Kessy. Hata hivyo Msuva hakuendelea na mchezo baada ya kufunga bao hilo kwani aliumia kichwani na hivyo kulazimika kutoka uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Abdul.

Katika kipindi cha kwanza jana, Yanga walikuwa vizuri zaidi wakipeleka mashambulizi kuanzia nyuma lakini hawakuwa makini katika umaliziaji hali iliyosababisha wakose mabao mengi.

Mbeya City ilibadilika kipindi cha pili na kuanza kuliandama lango la Yanga ambapo dakika ya 58 Haruna Shamte aliifungia bao la kusawazisha baada ya kutumia vizuri makosa ya Haji Mwinyi Ngwali.

Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana kwani Obrey Chirwa aliiandikia Yanga bao la pili akiunganisha mpira wa adhabu iliyopigwa na Abdul nje ya 18. Kwenye uwanja wa Kaitaba Bukoba, Mbao imezidi kujiweka kwenye wakati mgumu baada ya kufungwa mabao 2-0 hivyo kushuka mpaka nafasi ya 14 na pointi zake 30.

Majimaji huenda ikajinasua baada ya kumfunga kibonde JKT Ruvu bao 1-0 kwenye uwanja wa Majimaji Songea, sasa timu hiyo imepanda mpaka nafasi ya tisa ikiwa na pointi 32.