Mwakyembe awapongeza Serengeti Boys

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewapongeza wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana waliochini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, makocha na viongozi wote kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Angola katika mashindano ya Vijana vya Afrika yanayofanyika nchini Gabon.

Katika ujumbe aliomtumia Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara, Dk Yusuf Singo ambaye yupo Gabon, Dk. Mwakyembe amemwagiza kuwaeleza wachezaji, makocha na viongozi kuwa, Taifa limejawa na furaha kutokana na ushindi huo.

“Ushindi wetu wa timu ya Taifa ya vijana wa mabao 2-1 dhdi ya Angola umepokelewa na watanzania kwa furaha isiyokuwa na kifani na kwa ari mpya ya kuiombea na kuitakia Serengeti boys ushindi mnonio dhidi ya Niger Jumapili wiki hii,” alisema Dk. Mwakyembe.

“Vijana wetu wameonesha dunia kandanda safi na la kiwango cha juu na wameweza kuwathibitishia watanzania wenzao dhamira ya kauli mbiu ya Gabon hadi Kombe la Dunia,” alisema Dk. Mwakyembe.

Pia alisema vijana wanatakiwa kujua kila wawapo uwanjani hawapo peke yao bali na Baraka za watanzania wote ambao wanafuatilia mashindano hayo kwa karibu kupitia radio, runinga, mitandao ya kijamii na magazeti.

Aidha alisema wanatakiwa kutambua taifa zima lipo nyuma yao kwa maombi ya heri ya mafanikio. Kila la heri Serengeti boys. Serengeti boys ilicheza juzi na Angola katika Uwanja wa Uwanja wa Stade de l’Amitié mjini Libreville baada ya mchezo wa ufunguzi kutoka suluhu na bingwa mtetezi Mali.