Mayanga awapeleka vijana nusu fainali

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema asilimia 75 Serengeti Boys imefuzu kucheza Kombe la Dunia kwa vijana waliochini ya miaka 17. Akizungumza na gazeti hili, Mayanga alisema kiufundi, kimbinu na kisaikolojia wachezaji wa Serengeti Boys wapo vizuri kwa sababu walipata maandalizi mazuri.

“Imepata maandalizi ya kutosha na wachezaji na makocha wameonesha kile walichokipata tofauti na watu wengine walivyokuwa wakibeza,” alisema Mayanga “Wamecheza mechi ya pili wamepata pointi nne na naamini wataenda hadi fainali kwani mchezo wa mwisho tutashinda kwani kimbinu Angola walikuwa wazuri kuliko Niger,” alisema Mayanga Pia Mayanga alisema katika mchezo wa mwisho dhidi ya Niger, Serengeti boys wapo vizuri kimbinu na ufundi na uwezekano wa kushinda na mkubwa ila utulivu na kujiamini kunahitajika.

Aidha, Mayanga amewaomba wadau na makampuni waendelee kuichangia timu yao ili iendelee kufanya vizuri. Unaweza kutoa mchango kupitia akaunti ya benki ya TFF Football Development Fund Na. 0086628003 ambayo ipo Dimond Trust Benki Tawi la barabara ya Nyerere au Airtel Money 0687333777 Kwa mara ya mwisho Tanzania ilishiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 wakati timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars, ilipotolewa katika hatua ya makundi nchini Nigeria.

Mashindano hayo ya 12 yanashirikisha timu nane ambazo zipo kwenye makundi mawili, kundi A lina timu za wenyeji Gabon, Guinea, Camroon na Ghana na kundi B lina timu za Tanzania, Mali, Niger na Angola.