Stars kambini kesho kujiandaa COSAFA

TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars inaingia kambini kesho, Dar es Salaam kujiandaa na michuano ya soka ya Baraza la soka la nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA). Kikosi cha wachezaji 22 kitaingia kambini Dar es Salaam kujiandaa na michuano hiyo ya Kombe la Castle Cosafa Juni 25, 2017.

Kocha wa timu hiyo, Salum Mayanga alisema anatarajia watafanya vizuri katika michuano hiyo kwa kuwa kikosi kinaundwa na wachezaji wenye damu changa zaidi. “Michuano ya COSAFA takuwa sehemu ya maandalizi ya kikosi kitakachoshiriki michuano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani(CHAN),” alisema.

Kikosi hicho kinaundwa na makipa Aishi Manula (Azam FC), Benno David Kakolanya (Yanga) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar). Walinzi wa pembeni kulia ni Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Ramadhan ‘Kessy’ (Yanga) na kushoto ni Gadiel Michael (Azam FC) na Amim Abdulkarim (Toto Africans).

Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons). Viungo wakabaji ni Himid Mao (Azam FC) na Salmin Hoza (Mbao FC). Viungo washambulia ni Mzamiru Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Kichuya (Simba).

Washambuliaji ni Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC). Tanzania imepangwa kundi A na Mauritius, Malawi na Angola.

Kundi B lina Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Timu 14 zinashiriki michuano hiyo. Stars itacheza na Malawi Juni 25 kabla ya kukutana na Angola Juni 27 na kumalizia na Mauritius Juni 29. Botswana, Zambia, Afrika Kusini, Namibia, Lesotho na Swaziland zitamenyana kuingia robo fainali ya mashindano yaliyoanzishwa 1997.