Usajili Kagera Sugar hadharani wiki ijayo

KLABU ya Kagera Sugar imesema itaweka wazi usajili mwingine mpya wiki ijayo baada ya kunasa saini za baadhi ya wachezaji sita wiki iliyopita.

Kagera Sugar hivi karibuni ilitangaza baadhi ya wachezaji iliowasajili akiwemo mkongwe Juma Nyoso, mlinda mlango wa JKT Ruvu Said Kipao, mshambuliaji wa African Lyon Omari Daga, Japhary Kibaya wa Mtibwa Sugar, Peter Mwalyanzi na Ludovic Venance wote wa African Lynon.

Akizungumza na gazeti hili jana Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Hamis Madaki alisema usajili wao unaendelea na hadi katikati ya wiki ijayo, watakuwa na kikosi kilichokamilika. “Tunaendelea na usajili tutaweka wazi wiki ijayo majina yote tulioingia nao mkataba,” alisema.

Katibu huyo alisema usajili huo unatokana na mapendekezo ya Kocha wao, Mecky Maxime katika kuhakikisha msimu ujao wanafanya vizuri zaidi. Alisema kuna mazungumzo yanafanyika dhidi ya wachezaji inaowahitaji na mambo yakiwa mazuri watamalizana nao.

Timu hiyo msimu uliopita ilifanya vizuri na kushika nafasi ya tatu na sasa imedhamiria kuendelea kuwa katika kiwango bora msimu ujao wa Ligi Kuu Soka Tanzania bara. Tayari Kagera Sugar imempoteza mshambuliaji wake, Mbaraka Yusuf aliyeingia mkataba na Azam FC hivi karibuni. Mchezaji huyo aliisaidia Kagera Sugar kumaliza ya tatu msimu uliopita baada ya kuifungia mabao 12.