Yanga: Wiki inatosha kuiua Simba Agosti 23

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Yanga, George Lwandamina amesema wiki moja inatosha kukinoa kikosi chake tayari kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 23 Uwanja wa Taifa.

Pia Lwandamina alisema jana Dar es Salaam wiki moja inamtosha kuandaa kikosi chake kwa msimu mpya wa ligi na Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo imepangwa kuanza Agosti 26 mwaka huu.

Programu ya Lwandamina ilianza kwa mazoezi ya wachezaji kutanua misuli ya miili kwa wiki moja katika Gym City Mall. Juzi wachezaji waliingia hatua ya pili ya mazoezi ya uwanjani kufundishwa vitu mbalimbali ikiwemo mbinu na mifumo.

Alisema kitu alichopanga kuanza nacho ni kutengeneza mfumo wa uchezaji ambao ni muhimu kuipa timu matokeo mazuri. Alisema ataiunganisha timu kiuchezaji kwani baadhi ya wachezaji ni wageni hivyo wanatakiwa kuelewana na msimu uliopita.

Yanga leo wanaenda Morogoro kupiga kambi ya wiki moja kujiandaa dhidi ya Simba mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 23. Katika kujiimarisha zaidi jana wamemsajili kipa wa Serengeti boys, Ramadhan Kabwili ambaye ataungana na makipa wengine wawili.

Watacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United Agosti 6 Uwanja wa Taifa. Msemaji wa Yanga, Dismas Ten alisema Lwandamina amepania kuweka rekodi hivyo anahitaji mazingira yaliyotulia. Simba wako Afrika Kusini kujiandaa na msimu tangu wiki iliyopita.